Askofu RC atishiwabastola madhabahuni
MWANAMKE ambaye jina lake halikufahamika, amevamia madhabahuni na kuchomoa bastola kisha kutishia kumwua askofu wa Jimbo Kuu la Njombe, Alfred Maluma aliyekuwa akiendesha ibada katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jimboni humo.
Jaribio hilo la mauaji lililozua tafrani kubwa kanisani hapo na hata kuvuruga kwa muda mwenendo wa ibada, lilidhibitiwa na padri mmoja aliyekuwapo madhabahuni hapo ambaye alimrukia mama huyo na kuikamata bastola hilo.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa tukio hilo la kwanza kutokea katika Kanisa la Mtakatifu Joseph lililoko Jimbo Kuu la Njombe, lilitokea Alhamisi iliyopita wakati wa ibada ya kusimika mashemasi.
Kwa mujibu wa habari hizo, mwanamke huyo awali alikuwa ameketi kwenye mabenchi kama mumini wa kawaida aliyekuwa akifuatilia ibada hiyo, lakini ghafla alisimama na kufuata askofu huyo na kumnyoshea bastola hiyo.
"Wakati wa kipindi cha mageuzo, mwanamke huyo alienda altareni na kumnyoshea bastola Askofu huyo akitaka kumuua," mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, alilieleza gazeti hili na kuongeza. Baada ya kutoa bastola hiyo huku askofu akiendelea na mageuzo, padri aliyefamika kwa jina la Ngiri, alimrukia kwa haraka na kumpokonya bastola hiyo."
Hata hivyo, habari zaidi zilieleza kuwa baada ya kuikagua bastola hilo ilikuwa haina risasi, lakini mwanamke huyo alikutwa na risasi kwenye begi lake la mkononi.
Mashuhuda wengine walilieleza gazeti hili kuwa bastola hiyo ilifahamika kuwa ya mmoja wa mapadre wa parokia za Jimbo la Njombe (jina la parokia na padre vimehifadhiwa), lakini haikufahamika mwanamke huyo aliipataje. “Ni Mungu tu aliyesaidia kwa kuwa huyo mtuhumiwa alikuwa amedhamiria kuja kuua na akasahau kuweka risasi hivyo inatakiwa polisi litupe ufafanuzi zaidi,” alisema shuhuda mwingine wa tukio hilo.
Jumapili iliyopita, baadhi ya mapadre walielezea tukio hilo kwenye ibada zao na kufafanua kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa mwanamke huyo ana matatizo ya akili. Katibu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe, Erasmo Mligo alithibitisha tukio hilo, lakini akaeleza kuwa hawawezi kuzungumza chochote kwa kuwa suala hilo sasa liko mikononi mwa polisi. "Suala hilo sasa liko kwa mkuu wa upelelezi Wilaya ya Njombe hivyo sisi kama kanisa hatuwezi kuzungumza chochote zaidi ya kuthibitisha kuwa tukio limekuwapo," alisema Mligo.
Kamanda wa Polisi wa Iringa, Everist Mangara aliliambia Mwananchi jana kuwa ana taarifa ya tukio hilo, lakini bado anafuatilia taarifa zake. "Tukio hilo nimelisikia, lakini sijalipata vizuri ila ninaendelea kulifuatia kwa karibu," alisema Mangara.
Source: Mwananchi
Monday, January 10, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment