Dk Slaa atajwa Urais Chadema
KAMATI kuu ya Chadema jana ilikutana jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mkakati wa kumpata mgombea urais wa chama hicho baada ya mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kuamua kugombea ubunge.
Habari kutoka kwa viongozi wa chama hicho zinasema kuwa mbunge wa Karatu, Dk Wilbroad Slaa ndiye anayeangaliwa zaidi kushauriwa kujitosa kwenye nafasi hiyo baada ya mjumbe wa kamati kuu, Profesa Mwesiga Baregu kugoma kugombea urais.
Tayari Dk Slaa ameshachukua fomu za kutetea kiti chake cha ubunge cha Karatu, lakini habari zinasema kuwa Chadema inamtaka katibu huyo mkuu kugombea urais baada ya kulichangamsha Bunge kwa hoja nzito katika vipindi vyake alivyolitumikia jimbo hilo.
Chadema, ambacho kimeongezeka nguvu katika kipindi cha miaka mitano baada ya kuingiza wanachama machachari ndani ya Bunge, imekuwa ikisaka mgombea urais ambaye ataweza kuendeleza umaarufu wa chama hicho na vyombo vya habari vimekihusisha chama hicho na mipango ya kumshawishi waziri mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye na Spika wa Bunge, Samuel Sitta kuingia kwenye mbio za urais kwa tiketi ya chama hicho.
Hata hivyo, taarifa za vyombo vya habari zimeeleza kuwa vigogo hao wawili wa CCM wamekataa kukiasi chama chao.
No comments:
Post a Comment