Mbunge wa CUF ajiunga CCM
MBUNGE wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Wananchi(CUF), Mercy Mussa Emmanuel ambaye pia alikuwa Katibu wa Wilaya ya Maswa kwa chama hicho, jana alikihama na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, ndiye aliyempokea Mercy na kumkabidhi kadi mpya ya uanachama wa CCM mjini hapa, muda mfupi kabla ya Rais Kikwete hajaagana rasmi na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uamuzi wa Mercy ambao bila shaka ni pigo kwa CUF, aliuchukua jana asubuhi saa 4:30 na alimkabidhi Rais Kikwete kadi ya CUF na Rais alimpa kadi mpya ya uanachama wa CCM.
Akizungumza na HABARILEO kwa hisia kali, mbunge huyo alisema kwamba, katika maisha yake hapendi unafiki, hivyo amefanya uamuzi kulingana na dhamira yake ilivyomtuma.
Alisisitiza kwamba, hakushawishiwa na yeyote, bali amevutwa na utendaji mzuri wa CCM inayotekeleza kwa vitendo Ilani zake, chini ya ujemedari wa Rais Kikwete.
Akifafanua, alisema alitamani kufanya hivyo siku nyingi, lakini alishindwa kutokana na kuwa kiongozi katika chama, hivyo alikata shauri na kuvuta subira hadi amalize miaka mitano ya ubunge.
“Nilipata wazo la kuihama CUF nikiwa bungeni, kikubwa kilichonisukuma ni woga wa unafiki. Unakuta kuna mambo ya msingi kabisa yanayostahili kuungwa mkono, lakini kwa kigezo cha upinzani, mengi hupingwa.
“Kwa kweli sikuifurahia hali hii kwa sababu kama mbunge, niliona kuna mengi mazuri yanayofanywa na CCM. Nilivumilia nikidhani kunaweza kuwa na mabadiliko, lakini mambo yakawa yale yale …,” alisema na kuongeza kwamba, hana ugomvi na CUF, chama alichokitumikia kwa moyo mmoja na hata kukiimarisha wilayani Maswa alikokuwa Katibu wake.
Aidha, alichukua fursa hiyo kuishukuru CUF kwa kumpa ushirikiano na heshima ya kuwa mmoja wa wabunge wake katika kipindi chote alichokuwa na chama hicho.
“Nawashukuru sana, tulipendana, kuheshimiana na kushirikiana, ila wakati umefika nimeamua kuondoka kwa hiari yangu. Naitakia CUF kila la heri,” alisema mbunge huyo ambaye hakuweka wazi kama atajitosa kuwania ubunge kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao, akidai anahitaji muda wa kutafakari.
Source: HabariLeo
Friday, July 16, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment