Askofu Malasusa apata ushindi wa kishindo KKKT- DMP
MKUTANO mkuu wa 30 wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) umemchagua Askofu Alex Malasusa kuingoza tena dayosisi hiyo hadi atakapostaafu utumishi wa kanisa hilo. Askofu Malasusa, ambaye pia ni mkuu wa KKKT nchini, alichaguliwa kwa kura ya imani iliyopigwa juzi jioni, mwanzoni mwa mkutano huo ambao ulitanguliwa na madai ya kuwepo njana za kumuhujumu kiongozi huyo.
Madai ya hujuma yalibainishwa Novemba 23 mwaka huu wakati Msaidizi wa Askofu, Mchungaji George Fupe alipowaeleza waandishi kuwa kuna kikundi cha watu wanaojiita waumini wa kanisa hilo ambao alidai kuwa walikuwa wakifanya njama za kuhujumu mkutano huo kwa kutumia magazeti.
Kwa mujibu wa Mchungaji Fupe, Halmashauri Kuu ya KKKT-DMP iliyokutana Novemba 18, 2010 iligundua kwamba hoja zinazoandikwa katika magazeti ya Kiswahili moja la kila siku (siyo Mwananchi) na jingine la kila wiki yanayomilikiwa na kampuni moja, “zinalenga kuvuruga na kuchafua maandalizi ya mkutano mkuu wa 30 wa Dayosisi”. Katika mkutano unaoendelea mjini Bagamoyo ambao una ajenda 14, uchaguzi ulikuwa ajenda ya mwisho lakini utarabu huo ulibadilika baada ya hoja iliyotolewa na mmoja wa wajumbe ya kutaka zipigwe kura za imani (uchaguzi) kabla ya kuendelea na ajenda nyingine.
Habari kutoka Chuo cha Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) mjini Bagamoyo ambako mkutano huo unafanyika, zinasema kuwa baada ya ajenda ya kwanza ya kuhakiki akidi ya wajumbe wa mkutano, mmoja wa wajumbe alitoa hoja kutaka mabadiliko ya mtiririko wa ajenda.
“Mjumbe aliyetoa hoja hiyo alitaka mkutano mkuu uthibitishe, kukubaliana au kutokubaliana na tamko la Halmashauri ya Dayosisi lililotolewa kwenye sharika na kwenye vyombo vya habari kuhusu kuwepo kwa njama za kuhujumiwa kwa mkutano,” kilieleza chanzo chetu kutoka ndani ya mkutano huo. “Hoja ya kutaka kura zipigwe mapema ilitolewa kwa maelezo kwamba ni kumwezesha mwenyekiti wa mkutano (ambaye ni Askofu Malasusa) kuendesha kikao akiwa na amani na wajumbe wote na kama kulikuwa na wanaompinga, pia wawe na amani baada ya uchaguzi kufanyika.” Kwa mujibu wa habari hizo, hoja hiyo ilizua mjadala miongoni mwa wajumbe kabla ya kuafikiana kufanya mabadiliko ya ajenda hivyo kura za imani zilipigwa na Askofu Malasusa kupata ushindi mkubwa. Katika uchaguzi huo, Askofu Malasusa alipata kura za imani 256 sawa na asilimia 96.6 ya wajumbe 265 waliokuwepo. Wajumbe nane hawakupiga kura na mjumbe mmoja alipiga kura ya kutokuwa upande wowote.
Soma habari zaidi katika Mwananchi
Monday, December 6, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment