Michelle Obama akutana na Nelson Mandela
Michelle Obama mke wa Rais wa Marekani amekutana na kiongozi wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake katika nchi mbili za kusini mwa Africa.
Wakfu wa Mandela umesema kuwa Bi Michelle Obama, mama yake na binti zake wawili wamemtembelea Bw. Mandela na kuzungumza nae kwa muda mfupi.
Mwandishi wa BBC Karen Allen ambaye yuko Johannesburg anasema kuwa shujah huyo wa ukombozi dhidi ya ubaguzi wa rangi mwenye umri wa miaka 92 anaonekana hafifu na ni nadra yeye kuwapokea wageni.
Ziara hii ya Michelle Obama inanuiwa kupigia debe umuhimu wa vijana uwongozini.
Ziara hii ni ya pili rasmi ambayo Michelle Obama amefanya peke yake tangu mumewe achukuwe hatamu za uwongozi mwaka 2009.Anatarajiwa kukutana na kiongozi wa sasa wa Afrika Kusini Jacob Zuma kabla ya kuelekea Bostwana.
Bi Michelle Obama pia anatarajiwa kuyatembelea makumbusho ya enzi za utawala wa ubaguzi wa rangi na mji wa mabanda wa Soweto ambao ulikuwa katikati ya harakati za kukabiliana na utawala wa wazungu waliochache katika enzi hizo za ubaguzi wa rangi.
Ziara hii pia itajumuisha kutembelea kisiwa cha Robin ambako Bw. Mandela alihudumu 18 kati ya miaka 27 aliyokuwa gerezani.
Bi Obama alikaribishwa Afrika Kusini jumanne jioni baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa kijeshi mjini Pretoria ambako binti zake wawili Malia na Sasha walipewa blanketi kubwa zilizokuwa na rangi ya bendera ya Afrika Kusini kujikinga baridi.
Jumatano Michelle atakutana na viongozi vijana wa kike atakapotoa hotuba yake.
Source: BBC
Tuesday, June 21, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment