Thursday, June 30, 2011

Posho kumfukuza Shibuda Chadema

Best Blogger Tips
Via Mwananchi

KITENDO cha Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda kupingana na sera ya chama chake kuhusu suala la posho za vikao (sitting allowance), kimeichefua Chadema ambayo imemuita msaliti ikisema, "adhabu yake ni kufukuzwa.

"Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliliambia Mwananchi mjini Dodoma jana kuwa, alikerwa na kauli iliyotolewa na Shibuda ya kwenda kinyume na msimamo kambi hiyo kupinga posho za vikao kwa wabunge na wafanyakazi wengine wa umma.

Mbowe alisema kwamba kwa kauli yake ya juzi ya kuunga mkono posho ilidhihirisha kwamba mbunge huyo ni msaliti wa kambi hiyo, hivyo sheria zitafuata mkondo wake.

"Kutokana na tukio la jana (juzi) bungeni, Shibuda kutusaliti katika suala la posho za vikao, taratibu za kisheria zitafuata mkondo wake kwani utovu wa nidhamu haukubaliki katika kambi yetu, hata katika chama chetu,"alisema Mbowe na kuongeza:

"Suala la posho si la mtu binafsi, lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi wa 2010 ya chama chetu na kama kuna kiongozi hafahamu hili basi hakustahili kugombea ubunge kwa sababu naamini Ilani ya Uchaguzi, Shibuda anayo."

"Posho zilijadiliwa na kupitishwa katika vikao maalumu vya chama, kwa hiyo kama Katiba yetu ya chama inavyotuongoza, Shibuda alitakiwa kulipinga katika vikao hivyo sio kutoka nje ya kikao na kuanza kupingana na maamuzi yake,"alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.


Akinukuu kifungu katika Katiba ya chama chake kinachoeleza maadili ya viongozi, Mbowe alisema, "Kiongozi anatakiwa kutii na kutimiza maagizo anayopewa na viongozi wa ngazi ya juu au vikao halali na kama hakubaliani na maagizo hayo aeleze hivyo kwa kupitia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye kanuni."

Kauli ya Zitto
Kwa upande wake, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe, aliliambia gazeti hili jana kuwa mbunge kupingana na sera ya chama chake, ni kutokiamini chama hicho.

"Maana yake hakiamini chama, hivyo hafai kuendelea kuwa mwanachama na mbunge wa chama hicho,"alisema Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.

Aliendelea, "Hapa kuna mambo mawili; masuala ya kisera na masuala ya utaratibu. Mbunge anayepingana na taratibu adhabu yake ni kumwita na kumpa onyo, lakini mbunge anayepingana na sera, huyo hakiamini chama na dhabu yake ni kufukuzwa."

Kwa mujibu wa Zitto, suala la kupinga posho kwa Chadema ni sera kwa kuwa limo kwenye Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2010.

"Hili (suala la posho), lipo kisera. Kwenye Ilani yetu ya uchaguzi tulisema, tutapunguza mishahara ya wabunge na posho zao. Sasa kama mbunge anachaguliwa kwa sera hiyo halafu anaipinga haradhani, huyo hakiamini chama na chama hakipaswi kumwamini."

Aliendelea,"Sasa, adhabu ya juu kabisa ya mbunge asiyekiamini chama, ni kufukuzwa. Huu ni usaliti. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na mwenyekiti wa chama ameshalitolea tamko suala hilo halafu mbunge anakuja kumpinga hadharani maana yake nini,?" alihoji.

Tundu Lissu je?
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema kitendo cha Shibuda kupingana na sera ya chama chake, "ni uasi usiovumilika".

"Sasa nikiwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni nadhani ninahitaji kukaa naye. Nitamwita anieleze kulikoni. Aseme kulikoni ameamua kukiasi chama na upinzani kwa ujumla?"

Aliendelea, "Lakini kwa bahati mbaya sana, adhabu kubwa inayoweza kutolewa na kambi ya upinzani ni kumtenga na kambi. Lakini kwa mtu kama Shibuda ambaye tayari anaijua adhabu hiyo na kuitafuta kwa makusudi, inaonekana haitamtosha."

"Kwa sababu hiyo basi, kambi ya upinzani itaenda mbali zaidi baada ya kumtenga. Tutakiandikia chama barua kukijulisha usaliti huo wa mbunge wake halafu chenyewe kina taratibu zake za kinidhamu."
Endelea kusoma habari hii...........................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits