TANZANIA imesema ipo tayari kukosa misaada yote kutoka Serikali ya
Uingereza na kamwe haiwezi kuruhusu sheria inayotambua mashoga na
kuhalalisha ndoa za jinsia moja.Msimamo huo mzito wa serikali umekuja
siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutamka
kwamba nchi yake ina mpango wa kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo
sheria na katiba zao, hazitambui mashoga na ndoa za jinsia moja.
Cameron
alikaririwa akithibitisha kuwa tayari amewajulisha juu ya suala hilo
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola waliokuwa wakihudhuria
mkutano wa Jumuiya hiyo uliomalizika siku nne zilizopita, mjini Perth ,
Austaralia ambao pia ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete.
Waziri
Mkuu huyo kutoka chama cha Conservative ambacho kilishinda uchaguzi Mei
mwaka jana, alisema suala hilo la mashoga na ndoa za jinsi moja ni
moja ya mambo yanayoongoza sera ya serikali yake kuhusu misaada kwa
mataifa mbalimbali na kwamba tayari imeanza kutekelezwa katika maeneo
kadhaa duniani.
Kauli ya Cameron imechukuliwa kama kielelezo cha
ukoloni mamboleo ambao Uingereza inajaribu kuupandisha daraja kwa
mataifa yanayoendelea kwa kigezo cha misaada
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alisema pamoja na umasikini
wake, Tanzania kamwe haitaruhusu upuuzi huo kwa kigezo cha misaada.
“
Tanzania ni nchi maskini lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti
kwa sababu ya misaada yake na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni
wetu, hata sheria zetu zinakataa,” alisema Membe.
Alifafanua kuwa
katika kuonesha msimamo wa kutokukubaliana na masharti hayo, Tanzania
imeshikilia msimamo thabiti kupinga upuuzi huo ambapo Januari mwaka
huu, ilimkataa balozi shoga ambaye aliteuliwa na nchi yake kuja
kuiwakilisha hapa nchini. Hata hivyo Waziri Membe hakutaja jina la
balozi huyo wala nchi anayotoka.
“Niwape siri moja ambayo
tuliificha lakini leo ngoja niwaambie, mwanzoni mwa mwaka jana
nililetewa barua kunijulisha ujio wa balozi mmoja anayekuja
kuiwakilisha nchi yake, mwanamume mwenye ndoa ya jinsia moja. Nilikwenda
kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuhusu wasifu wa balozi huyo mtarajiwa
naye akajibu kwa maneno matatu, yarabi toba! Mkatae!”
Waziri
Membe alifafanua kuwa serikali ilimkataa balozi huyo kwa kuwa ni kinyume
cha utamaduni wetu na sheria za nchi kuwa na watu wenye tabia hizo.
Alisema
alimjulisha waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kwamba balozi huyo
haruhusiwi kuja kufanya kazi nchini kwa kuwa ni kinyume na utamaduni
wetu. “ Waliendelea kuniomba kwamba balozi huyo akija hatatoka kwenye
makazi yake akiwa na mwenza wake hivyo watu hawatamuona lakini
tulimkataa kabisa, wakatuelewa,” alisema Membe.
Alieleza kuwa
tamko hilo la Waziri Mkuu Cameron linaweza kusababisha hatari ya
kuvunjika kwa uhusiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola
na koloni mama Uingereza na waziri huyo atabeba lawama hizo
Akisisitiza
msimamo huo wa serikali, Membe, alisema Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971
kifungu cha tisa, kinatambua ndoa ya jinsia mbili tofauti, yaani mume
na mke. “ Sheria hizi tunazozitumia hivi sasa tumezirithi kutoka
Uingereza ambako leo wanatukuza ndoa za jinsia moja na ushoga,” alisema
Membe.
Suala la kile kinachoitwa haki za binadamu kuhusu ushoga
ilikuwa moja ya ajenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana
katika mkutano Perth .
Hoja ya kukomesha vizuizi dhidi ya
ushoga na ndoa za jinsi moja lilikuwa moja ya mapendekezo yaliyokuwamo
katika ripoti ya ndani kuhusu matarajio ya baadaye ya Jumuiya hiyo ya
Madola.
Itakumbukwa kwamba, Malawi tayari imeathirika na
mpango huo wa Uingereza kwa sehemu ya misaada yake kusitishwa kutokana
na msimamo wa nchi hiyo kuhusu kile Uingereza na nchi za Magharibi
zinazokiita haki za mashoga. Ikumbukwe pia kuwa, mjadala mzito ulioibuka
katika Bunge la Uganda mwaka 2009 kuhusu ndoa za jinsi moja ilikuwa
sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo ya Uingereza na washirika wake.
Ajenda zingine Mkutano wa Perth Waziri Membe alisema viongozi wa
Jumuiya ya Madola walikubaliana suala la mabadiliko ya tabia nchi kuwa
ajenda kuu katika nchi hizo.
Alisema ajenda hiyo sasa inakuwa
muhimu kutokana na nchi nyingi wanachama wa jumuiya hiyo kuwa katika
tishio kubwa la uharibifu wa mazingira.
Aidha, Membe alisema nchi hizo zimekubaliana kuandaa kanuni na mwongozo ambao utatakiwa kufuatwa na nchi za jumuiya hiyo.
“
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Jumuiya ya Madola tutakutana Aprili
mwakani kuandaa miongozo na kanuni hizo,” alisema Membe.
Source: Mwanachi