Wednesday, November 30, 2011

Wahusika wa kashfa ya BAE TZ kushtakiwa

Best Blogger Tips
Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza
 Kundi la wabunge kutoka vyama mbali mbali vya siasa nchini Uingereza limetoa wito wa kufunguliwa mashtaka dhidi ya mtu yeyote aliyehusika katika kashfa ya ufisadi na rushwa kuhusiana na mauzo ya rada yaliyofanywa na kampuni ya vifaa vya ulinzi ya BAE Systems ya Uingereza.

Kampuni ya BAE Systems tayari imekubali kulipa takriban dola millioni 46 kama fidia kwa Tanzania kwa kukosa kuweka kumbukumbu zake za mahesabu kuhusiana na mauzo hayo yenye utata.

Lakini kamati ya maendeleo ya kimataifa ya bunge la Uingereza imeishutumu kampuni hiyo kwa kuchukua muda mrefu kurejesha kiasi cha fedha ilichozidisha katika mauzo ya rada hiyo.

Kiasi kikubwa cha fedha kilichotozwa na kampuni ya BAE system ya Uingereza iliyoiuzia Tanzania rada ya kijeshi kilichochea kufanyika kwa uchunguzi dhidi ya kampuni hiyo.

uchunguzi

Uchunguzi huo ulifanywa na Shirika la Kupambana na Ufisadi la Uingereza, Serious Fraud Office.

Mwaka jana, baada ya BAE kukiri kushindwa kutunza kumbukumbu zake kuhusu mauzo hayo, kampuni hiyo ilikubali kulipa kiasi cha dola milioni 46 kwa Tanzania kama fidia ya mauzo kutokana na ulaghai uliofanyika.

Fedha hizo zilikubalika zitumike kununulia vitabu vya shule na vifaa vingine.

Lakini bunge la Uingereza limesikitishwa kuwa fedha hizo bado hazijalipwa.

BAE systems inasema kwa sasa inawasiliana na shirika la misaada la kimataifa la Uingereza kuona namna fedha hizo zitakavyotumika.

Japokuwa BAE systems haikupatikana na hatia ya rushwa, lakini watu binafsi waliohusika na kashfa hiyo wanaweza kushitakiwa.

Wabunge wa Uingereza wamesema wako tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania katika mahakama zake kuendesha mashtaka dhidi ya watu wanaohusika na ulaghai huo.
Chanzo: BBC

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits