|
Jose Chameleone |
HAKUNA ubishi kwamba, unapotaja jina la Jose Chameleone, moja kwa moja
akili itakuelekeza kwa msanii anayeporomosha muziki wenye mvuto,
uliochanganywa na vionjo vya kiasili kutoka kwa nyota huyo raia wa
Uganda.
Amekuwa akikonga nyoyo za mashabiki wa ndani na nje ya Afrika Mashariki kwa takribani miaka 12 sasa.
Bila kutafuna maneno, yafaa kueleza kuwa, ndani ya kipindi hicho
Chameleone ambaye jina lake halisi ni Joseph Mayanja, hajachuja.
Na ndiyo maana kila kukicha, nyota ya msanii huyo inazidi kung’ara,
hali kadhalika kipato chake kikizidi kuimarika kiasi cha kumfanya mmoja
wa vijana wenye uwezo mkubwa kifedha nchini Uganda.
Nyota huyo aliyezaliwa miaka 33 iliyopita ameshavuka katika daraja la umasikini, sasa akiogelea fedha.
Ndiyo, kwa asiyeamini, hebu angalau baadhi ya mambo yanayothibitisha utajiri wa nyota huyo.
Anamiliki jumba la kifahari katika vilima vya Sekuku jijini Kampala,
pia ana nyumba huko Arizona, Marekani, achilia ile ya Kigali, Rwanda
aliyoinunua hivi karibuni kwa mamilioni ya shilingi.
Ukiachilia mbali gari la kisasa aina ya Cadillac Escalade
lililomgharimu zaidi ya Sh milioni 100, Chameleone ambaye ni baba wa
watoto watu, pia anamiliki Mercedes Benz, BMW na aina nyingine za
magari.
Kwa ujumla, anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Sh bilioni 1.5 kwa
fedha za Tanzania. Na anasema bado anazisaka, kwani bila ya kuwa na
tamaa ya kusaka mafanikio zaidi, ndoto huenda zisitimie.
Anayasema hayo akisisitiza kuwa, baada ya nyumba, magari na akaunti
nono benki, sasa ana ndoto za kumiliki helikopta yake, baada ya kuwa
amekuwa akikodi mara kadhaa ama kwenda katika matamasha au kama
alivyofanya wakati anamuoa mkewe Daniela Atim.
Je, ni nini siri ya mafanikio ya nyota huyu kipenzi cha wengi Afrika
Mashariki na Kati? Mwenyewe, amekaririwa mara kadhaa akisisitiza kuwa,
ni kujituma na kuuchukulia muziki kuwa ni kazi.
“Bila kujituma, hakuna maendeleo. Nimehangaika sana kuyatafuta
maendeleo, na hata baada ya kuyapata, sijabweteka. Nafanya kazi usiku na
mchana huku nikihakikisha kila shilingi ninayoingiza inazidi kuniinua
kimaisha,” anasema nyota huyo mwenye utitiri wa tuzo za ndani na nje ya
Uganda.
Ubora wa nyimbo kama Kipepeo, Mama Rhoda, Jamila, Mambo Bado, Mama
Mia, Shida za Dunia, Fitina Yako, Haraka Haraka, Ndivyo Sivyo
aliomshirikisha Joseph Haule `Profesa Jay’ wa Tanzania, ni baadhi ya
kielelezo cha kipaji cha kipekee cha muziki kwa Chameolen, msanii mwenye
umbo dogo lakini anayetajwa kuwa mkorofi.
Je, mwenyewe anazungumziaje kuhusu ukorofi? Anasema: “Hata wewe ukiniangalia utaamini kuwa mimi ni mkorofi?
Mara nyingi nasingiziwa ili watu wengine wafanye biashara…” Je,
alitokea wapi kimuziki? Ni historia ndefu, lakini kwa kifupi itoshe
kusema kwamba, alianzia mwaka 1994 akiwa mchezesha disko katika klabu ya
usiku ya Maganjo Mizuri, wakati huo akiwa mwanafunzi wa sekondari
jijini Kampala.
Na aliwahi kuajiriwa Rwanda katika klabu ya usiku ya Cadillac mara tu baada ya kuhitimu elimu ya sekondari.
Kwa umahiri wake , mbali ya kumwingizia fedha nyingi, amebahatika
pia kuzuru Ulaya, Marekani na hata Mashariki ya Mbali kwa shughuli za
kimuziki, achilia heshima ya kutumbuiza wakati wa fainali za Kombe la
Dunia zilizofanyika Afrika Kusini mwaka jana.
Katika familia yao, Jose ni mtoto wa nne kati ya saba ambayo ina
msichana mmoja. Anakumbuka alisoma Shule ya Msingi Nakasero, Sekondari
ya Mengo na Sekondari ya Kiislamu ya Kawempe.
“Ingawa nilifaulu kiasi cha kutakiwa kujiunga chuo kikuu, niliamua
kuzama katika muziki. Na sijakata tamaa au kuahirisha, ipo siku nitasoma
chuo kikuu na kuitwa msomi,” anasema nyota huyo ambaye wazazi wake
walitaka asome na kuwa daktari, lakini akakacha masomo kwa muda.
Hata hivyo anasema kuwa, ingawa aliwaudhi wazazi wake, bado
anashukuru kwamba yeye ni daktari wa muziki anayewakuna wengi, ikiwa
pamoja na wazazi wake.
“Hatuna uhasama tena kwa sababu kama ni maisha nimeyashika, kwa
hivyo nimewafuta machozi wazazi wangu ambao awali waliamini labda ndiyo
nilikuwa napotea kimaisha.”
Baadaye alihamishia makazi yake Nairobi, Kenya alikoishi maisha ya
kubahatisha, alilazimika kulala studio hadi alipookolewa na Dorotea
ambaye jina lake halisi ni Griet Onsia.
Anakumbuka akiwa na Bebe Cool na Redsun alipata fursa ya kutumbuiza katika shindano la kumsaka Mrembo wa Kenya.
Anakiri hapo ndipo milango ya neema ilipoanza kufunguka. Anasema
Dorotea, baada ya kuzoeana alimshawishi ahamie nyumbani kwake badala ya
kuendelea kulala studio, ushawishi ambao ulimchukua zaidi ya wiki moja
kumkubalia.
“Nilipohamia tulikuwa marafiki, lakini mengine yaliibuka tukiwa
katika nyumba moja. Mara nyingi kila akitoka, alinikuta nimetulia
naandika nyimbo, huku akihoji ni lini nitarekodi. Nilikosa jibu kwa kuwa
siku wa na fedha.
“Siku moja akiwa safarini huko Afrika Magharibi aliniachia bahasha
yenye dola za Kimarekani 1,000 (karibu Sh milioni 1.8 za Tanzania kwa
sasa), akaniambia niingie studio.
“Huo ukawa mwanzo wa kibao Mama Mia na sikuamini kama fedha ile
ingebadilisha maisha yangu na kunifikisha hapa nilipo. Mengine yanabaki
kuwa historia,” anasema.
Pamoja na utajiri aliovuna kupitia muziki, nyota huyo anasema
historia ya kushuhudiwa `Live’ na watu zaidi ya bilioni 9 akitumbuiza
wakati wa Kombe la Dunia kwake ni kitu cha kipekee.
“Mtoto wa Afrika tena Afrika Mashariki kupewa heshima ile haikuwa
kitu kidogo. Najiona mwenye bahati na ni mastaa wachache wanaweza
kuingia katika kundi la bahati hata wangeishi kwa miaka 1000.”
Anasema kutokana na baraka alizopata maishani, ameamua kuanzisha taasisi ya Chameleone ili aweze kuwasaidia wasiojiweza.
“Nikiwa mdogo sikuwa na maisha mazuri, sikutoka katika familia bora,
kwa hiyo ninajiona mwenye wajibu wa kuwasaidia wengine wakianzia katika
misingi mizuri ya kielimu. “Nimeshanunua eneo kwa ajili ya kujenga
kituo.
Nataka jamii siku moja inikumbuke kwamba niliwika na kuitangaza nchi
yangu, lakini pia sikuwa mchoyo, bali niliyatumia vyema matunda ya
muziki.
Kwa kufanya hivi, naamini ipo siku nitawashawishi wengi kufanya mambo makubwa kwa ajili ya jamii wanayotoka.”
Huyo ndiye Joseph Mayanja ambaye pamoja na misukosuko ya maisha
tangu akiwa shule hadi sasa akiwa staa, bado nyota yake inang’ara.
Je, atazidi kupata mafanikio? Bila shaka ni jambo la kusubiri na
kuona, hasa ikizingatiwa kuwa, mwenyewe amejijengea falsafa ya kutolewa
sifa, bali kazi kwa kwenda mbele.
Pamoja na yote, Chameleone anapaswa mfano wa kuigwa kwa wasanii
wengi wa Kitanzania ambao huvuma kwa muda mfupi, lakini wakishazikamata
fedha hupotelea kwenye ulimwengu wa anasa na baadaye kujikuta wakiwa
`choka mbaya’, tena wakiwa hawana akiba benki wala hawajawekeza.
Chanzo: HabariLeo