Monday, December 12, 2011

Raia wa Afrika Kusini 'auliwa' China

Best Blogger Tips
China imempa adhabu ya kifo mwanamke mmoja raia wa Afrika kusini kwa kufanya biashara haramu ya kusafirisha dawa za kulevya, ikikataa ombi la Rais Jacob Zuma la kumwachia. 

Janice Bronwyn Linden, mwenye umri wa miaka, 38, aliuliwa zaidi ya miaka mitatu baada ya kukamatwa.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu tayari yamekuwa yakilaani China mara kwa mara kwa kutekeleza sheria ya hukumu ya kifo, yakisema mfumo wake wa sheria hauna haki.

Serikali ya Afrika Kusini imesema hatua hiyo haitoathiri mahusiano ya karibu ya kidiplomasia na China.

Serikali ya China iliwaruhusu dada zake wawili Bi Linden kukaa naye kwa saa nzima kabla ya kutekeleza hukumu hiyo kwa sindano ya sumu, gazeti binafsi la Afrika Kusini e. News, likimnukuu mwandishi kutoka China.

'Haijashughulikiwa vya kutosha'

Bi Linden alikamatwa Novemba 2008 baada ya kukutwa na kilogramu tatu za methamphetamine alipowasili uwanja wa ndege mjini Guangzhou kusini mwa nchi hiyo.

Aliendelea kutetea nafsi yake, akisema dawa hizo za kulevya zilitumbukizwa kwenye sanduku lake bila yeye kujua.

Hata hivyo, mahakama kuu ya Guangdong na ya rufaa huko Beijing zilikataa rufaa yake.

Msemaji wa idara ya uhusiano wa kimataifa, Clayson Monyela, aliiambia BBC kuwa Bw Zuma aliingilia kati kutaka hukumu hiyo ibadilishwe na apewe kifungo cha maisha.

Bw Monyela alisema, "Tumefanya kila namna kumnusuru hata katika nyanja zote za juu."

Alisema, serikali ya China itakabidhi majivu yake kwa familia yake, kufuatia kuchomwa maiti yake, kulingana na makubaliano yaliyofanywa baina ya mataifa hayo mawili.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa upinzani wa chama cha Democratic Alliance (DA) wa Afrika Kusini, Stevens Mokgalapa, amesema serikali haikufanya vya kutosha kuokoa maisha ya Bi Linden , gazeti binafsi la Afrika kusini Times Lives limeripoti.


No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits