Ghana yafuzu kucheza robo fainali
Gyan Asamoah akiachia mkwaju kutikisa nyavu za Marekani na kuipatia Ghana tiketi ya kucheza robo fainali.
Black Stars imezidi kuibeba Afrika, baada ya timu hiyo ya Afrika Magharibi kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini ilipoitandika Marekani mabao 2-1 katika uwanja wa Royal Bafokeng, mjini Rustenburg.
Mechi hiyo iliingia muda wa ziada baada ya kipindi cha kawaida kumalizika 1-1.
Wakishangiliwa na maelfu ya mashabiki waliofurika uwanja huo, vijana wa Ghana walianza kwa kasi huku wakionyesha mchezo wa hali ya juu na katika dakika ya nne ambapo Kevin-Prince Boateng alipopenya safu ya ulinzi ya Marekani na kuipatia Black Stars bao la kwanza.
Kipindi cha pili kilimalizika Ghana wakiongoza 1-0, na katika kipindi cha pili walilazimika kuimarisha safu ya ulinzi baada ya Marekani kurejea na mwamko mpya, hasa mshambuliaji wao hodari Landon Donovan.
Katika dakika ya 62 Jonathan Mensah alimwangusha Clint Dempsey kwenye eneo la hatari na hapo mwamuzi kutoka Hungary, Viktor Kassai akawapa Marekani penalti, ambayo Landon Donovan aliifunga, na kusawazisha.
Muda wa kawaida ulimalizika kwa matokeo hayo ya 1-1 na kulazimisha mechi kuingia muda wa ziada.
Dakika tatu tu baada ya muda wa ziada kuanza Asamoah Gyan alihimili kumbo la mlinzi wa Marekani, Carlos Bocanegra, na kuifikia pasi ndefu iliyotoka kwa Andre Ayew, na kusukuma mkwaju mkali hadi kwenye nyavu za lango la Marekani.
Sasa Ghana inasubiri kucheza na Uruguay kwenye robo fainali Ijumaa ijayo.
No comments:
Post a Comment