Thursday, February 10, 2011

Best Blogger Tips
Mubarak agoma kujiuzuru

Rais wa Misri, Hosni Mubarak amesema atasalia madarakani na kukabidhi madaraka yote baada ya uchaguzi wa urais mwezi Septemba.

Matamshi yake katika hotuba kupitia televisheni ya taifa, yamepishana na taarifa za awali kuwa alikuwa akijitayarisha kujiuzulu.

Hasira

Bw Mubarak amesema atakabidhi baadhi ya majukumu kwa makamu wa rais Omar Suleiman, lakini taarifa kamili ya jambo hili haifahamiki vyema.

Maelfu ya waandamanaji katika eneo la wazi la Tahriri wamepokea kwa hasira tangazo lake hilo.

Walikuwa wakipiga kelele za "tumechoka na Mubarak", huku waandamanaji wengine 'wakipeperusha' viatu vyao kwa ghadhabu. Maelfu wameripotiwa kutembea kuelekea katika ikulu ya rais ambayo iko umbali mrefu.

Bw Mubarak alikwisha sema mapema kuwa hatogombea urais mwezi Septemba, na kusema atasalia kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba.

"Natangaza nia yangu ya kuendelea na kuitetea katiba na kuwalinda wananchi na pia mabadiliko kwa yeyote atakayechaguliwa mwezi Septemba katika uchaguzi huru na wa wazi," amesema Mubarak.

Kutoka Moyoni

Akiwahutubia moja kwa moja waandamanaji "waliopo Tahrir na kwingineko" katika kile alichoita "hotuba kutoka moyoni mwake", bw Mubarak,82, amesema: "Sioni aibu kusikiliza vijana wa nchi yangu na kuchukua hatua."

Ameomba radhi kwa familia za waandamanaji waliokufa katika mapigano na majeshi ya usalama katika wiki za hivi karibuni, na kusema waliohusika na vifo hivyo watachukuliwa hatua.

Bw Mubarak ameongeza kuwa sheria za hali ya dharura nchi humo zitaondolewa pale tu hali itakapokuwa sawa, na kusema atawapuuza "madikteta kutoka nje ya nchi".

Pia ameonekana kutoa wito wa kumalizika kwa maandamano dhidi ya utawala wake wa miaka thelathini, yaliyoanza Januari 25.

"Misri imepitia nyakati ngumu na hatuwezi kuruhusu hali hii kuendelea," amesema. "Hasara kwa uchumi wetu itasababisha hao vijana wanaotaka mabadiliko kuwa wa kwanza kuathirika."

Utengamano

Bw Suleiman, akizungumza baada ya hotuba ya Bw Mubarak, amesema maandamano hayo yamefikisha ujumbe, na mchakato wa mabadiliko ya katiba utaanza.

Ameongeza kuwa Rais Mubarak amemkabidhi madaraka ya kurejesha amani na utengamano nchini MIsri, na kurejesha hali ya kawaida, na kuwataka waandamanaji kurejea nyumbani.

"Vijana wa Misri: rudini nyumbani, rudini kazini, taifa la Misri linawahitaji kupata maendeleo. Msisikilize redio na televisheni, ambazo nia yake ni kuitia doa Misri," alisema.

Mwanaharakati Mustafa Naggar akijibu matamshi ya viongozi hao amesema: "Mitaani wamechoshwa na Mubarak. Iwapo MUbarak ataondoka nchini, atasaidia kumaliza mzozo huu. Akiendelea, atasababisha Wamisri kuingia katika janga.

"Mipango ya kesho inabakia palepale. Tutaandamana kwa mamilioni hadi eneo la Tahrir na maeneo mengine."

Rais wa Marekani Barack Obama amekutana na maafisa wake wa usalama wa taifa katika ikulu ya Marekani, baada ya hotuba ya Rais Mubarak. Serikali ya Marekani katika siku za hivi karibuni, imezidisha wito wake kwa sauti za waandamanaji kusikilizwa.

Kulinda taifa
 
Mapema, katibu mkuu wa chama kinachotawala cha Bw Mubarak - National Democratic Party - Hossam Badrawi alisema, jambo sahihi kwa rais kufanya ni kuondoka madarakani, na kuwa hakuwa akitarajia Bw Mubarak kuwa bado rais siku ya Ijumaa.

Wakati huohuo, jeshi la Misri limetangaza kuwa liko tayari "kulilinda taifa". Shirika la habari la Misri Mena, limeripoti kuwa baraza kuu la jeshi lipo katika hali ya "kulilinda taifa, na matakwa ya watu".

Mazungumzo kati ya serikali na makundi ya upande wa upinzani yamepiga hatua ndogo, huku waandamanaji wakitupilia mbali mipango ya mabadiliko iliyopendekezwa na serikali ya Bw Mubarak.
Source: BBC









 

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits