Baraza la usalama la Umoja wa mataifa linakutana kuangalia uwezekano wa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi serikali ya Kanali Muammar Gaddafi.
Baraza hilo linategema kuweka vikwazo vya kiuchumi na pia kutaifaisha mali za serikali hiyo.
Pia baraza hilo linapendekeza Kanali Gaddafi kufikishwa katika mahakama ya kimaifa ya makosa jinai kwa makosa ya kukiuka haki za binadamu.
Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani, kwa mara ya kwanza amesema, Kiongozi huyo wa Libya anatakiwa kuachia madaraka na kuondoka katika nchi hiyo mara moja.
Ikulu ya Marekani imesema, Rais Obama aliweka msimamo wake wazi wakati akizungumza na kiongozi wa Ujerumani Kansela Angela Merkel wakati wa mazungumzo yao kwenye simu siku ya jumamosi jioni.
“ Rais amesema, kama umefika wakati kiongozi unawaongoza watu wako kwa kutumia nguvu na unyanyasaji, ni kwamba umepotea maana halisi ya utawala na inatakiwa uitendee haki nchi yako kwa kuachia madaraka na kuondoka mara moja,” imesema taarifa hiyo.
Mapema, mmoja wa watoto wa Kanali Gadaffi, anayeitwa Saif al-Islam, alisisitiza kwamba maisha yanaendelea kama kawaida kwa robo tatu ya Libya. Taarifa yake inapingana na ya waandamanaji wanaompinga Gaddafi ambao wanadai wameshikilia asilimia 80 ya nchi hiyo.
Ni vigumu kuthibitisha madai ya pande zote mbili, lakini inaaminika kwamba upande wa upinzani unashikilia mji wa pili wa Benghazi, wakati Kanali Gaddafi bado anashikilia mji mkuu Tripoli, ambao unakisiwa kuwa na watu milioni mbili. Nchi ya Libya inakisiwa kuwa na jumla ya watu milioni sita na laki tano.
Umoja wa Mataifa unakadiria zaidi ya watu 1,000 wamekufa katika uasi huo ambao umeingia siku ya kumi leo hii.
No comments:
Post a Comment