Lowasa apata kikombe Loliondo
Via Mwananchi
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa juzi alipata tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile katika Kijiji cha Samunge, Tarafa ya Sale, Loliondo, mkoani Arusha.
Lowassa alifika katika eneo hilo mchana akiwa na viongozi kadhaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Serikali kisha kupata kikombe kimoja chenye dawa kinachotolewa na mchungaji huyo kwa ajili ya tiba.
Tofauti na viongozi wengine, Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM), Jimbo linalopakana na Kijiji cha Samunge, alikwenda huko akiwa na viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na baadhi ya wapigakura wake.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Lowassa alithibitisha kwenda Loliondo na kuwataja viongozi wa dini alioambatana nao katika msafara wake kuwa ni Askofu Msaidizi wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Dk Frederick Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Dayosisi ya Kaskazini Kati (Arusha), Mchungaji John Nangole.
Katika ramani ya utendaji kazi ya KKKT, Jimbo la Masai Kaskazini ndipo kilipo Kijiji cha Samunge ambako ni makazi ya Mchungaji Mwasapile.“Ni kweli, nimekwenda pale na wapigakura wangu pamoja na viongozi wa dini, Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Mchungaji Nangole,” alisema Lowassa na kuuliza: “Kwani hiyo nayo ni habari jamani?”
Baada ya Lowassa kufika katika kijiji hicho akiwa na ujumbe wake, aliongoza moja kwa moja hadi kwa Mchungaji Mwasapile na kuzungumza naye kisha akapata kikombe cha tiba na kuondoka.
Kabla ya Lowassa kwenda kupata tiba, amekuwa akitoa msaada wa nauli kwa wagonjwa mbalimbali wa jimbo lake kwenda kwa mchungaji huyo ambaye dawa yake inadaiwa kutibu magonjwa ya saratani, kisukari, pumu, shinikizo la damu na Ukimwi.Lowassa ni miongoni mwa wanasiasa maarufu nchini ambao wameshafika kwa mchungaji huyo kupata tiba hiyo wakiwamo mawaziri, naibu mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya.
Katika jitihada za kudhibiti usalama na kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma kwa mchungaji huyo bila matatizo, Serikali imeimarisha ulinzi kwa kuweka askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), katika kijiji hicho na kusimamia magari. Pia imepeleka wauguzi kusaidia wagonjwa mahututi kabla ya kumfikia mchungaji na imetoa pia jenereta kwa ajili ya kufua umemeKaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Raymond Mushi alisema jana kuwa, sasa walau hali ni nzuri kwani msongamano umepungua.
"Ni kweli sasa hali inaridhisha na jana watu wamekwenda kupata tiba na kurejea makwao mapema hili ndilo serikali inalolitaka. Tunaomba watu wanaopeleka wagonjwa wawe wanauliza kwanza hali ya msongamano," alisema Mushi.Mushi alisema inawezekana watu wanaokwenda katika kijiji hicho kusubiriana katika Mji wa Mto wa Mbu ambako kuna huduma nyingi muhimu kuliko wote kwenda huko kwa wakati mmoja.
Endelea kusoma habari hii.............................
Tuesday, March 15, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment