Serikali yanywea kwa Mchungaji Loliondo
SERIKALI imebadili msimamo wake wa kusitisha kwa muda huduma ya tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapile katika Kijiji cha Samunge, Loliondo na badala yake imeunda tume itakayoshirikiana na mchungaji kumwezesha kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi.Juzi, Serikali kupitia kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda ilimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kusitisha kwa muda utoaji wa huduma hiyo hadi itakapojiridhisha kwamba dawa inakidhi ubora na inatolewa katika mazingira safi.
Hatua hiyo ilipingwa vikali na wananchi, viongozi wa dini na hata Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Raymund Mushi ambaye alisema utekelezaji wake utakuwa mgumu kutokana na hali halisi na mazingira yaliyopo katika eneo hilo kwa sasa.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Serikali haina tena mpango wa kuzuia huduma hiyo kwa kuwa inahusisha imani za watu.
“Serikali haina mpango wa kuzuia huduma hiyo na badala yake imeunda kamati itakayofanya kazi kwa kushirikiana na mchungaji huyo ili kuhakikisha jamii inapata huduma hiyo kwa utaratibu unaostahili,” alisema Lukuvi.Alisema kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambayo imeanza kazi jana imezuia magari yote yanayokwenda kijijini hapo ili kutoa nafasi kwa Mchungaji Mwasapile kuhudumia wagonjwa waliopo hadi idadi yao itakapopungua.
Alisema kazi ya tume kwa sasa itakuwa kuratibu na kupanga idadi inayotakiwa kufika na kutibiwa kwa mchungaji huyo ili kupunguza msongamano na uwezekano wa kutokea kwa matatizo mengine.“Nimeambiwa hadi sasa katika kijiji hicho kuna magari zaidi ya 800 na watu wanakadiriwa kufikia 6,000. Idadi hii ni kubwa na serikali haiwezi kuacha suala hilo likabaki hivi lilivyo. Tumeunda kamati itakayofanya kazi ya kuratibu idadi ya watu watakaotakiwa kufika katika kijiji hicho,” alisema Lukuvi.
Alisema pamoja na kuunda kamati itakayoshirikiana na mchungaji huyo, pia serikali inaandaa utaratibu wa kupeleka gari la kubebea wagonjwa (ambulance) kijijini humo ili kutoa msaada wa haraka kwa watu watakaohitaji huduma hiyo.Alisema sambamba na hilo, serikali itatuma idadi ndogo ya wauguzi ambao watasaidia kutoa huduma kwa watu watakaohitaji ambazo zitakuwa nje ya zile zinazotolewa na Mchungaji Mwasapile.
Waziri huyo aliziomba taasisi nyingine zikiwamo Msalaba Mwekundu kutoa msaada wa mahema kwa watu waliopo katika eneo hilo.
Alisema maofisa wa Serikali waliokwenda katika kijiji hicho kufanya utafiti juu ya dawa hiyo walipata ushirikiano mzuri kutoka kwa mchungaji huyo...
“Maofisa wetu wamekwenda na wamepewa ushirikano mkubwa ukiwamo wa kuonyeshwa namna dawa inavyochimbwa, inavyochemshwa na mti unaotoa dawa hiyo. Sasa kazi wanayofanya ni kutafiti na baada ya hapo watatoa majibu ya kitaalamu kuhusu dawa hiyo.”Alisema baada ya kuondoka kwa wataalamu hao serikali pia imepeleka wengine ambao wanafanya kazi ya kufanya taratibu za kumsajili.
Wananchi wachangia
Wananchi na baadhi ya wamiliki wa kampuni binafsi wameanza kutoa misaada ya mahema na nguvukazi ili kuboresha huduma zinazolalamikiwa kuwa ndizo zinazokwamisha utoaji wa tiba.Magari mawili ya mizigo yakiwa yamesheheni mahema, magodoro, maji ya kunywa, mikate na viti yameonekana katika eneo la barabara kuu ya kuelekea Sonjo katika eneo la Engaruka. Mmoja wa madereva wa magari hayo alisema msaada huo umetolewa na Masista kutoka Parokia ya Kanisa Katoliki, Wilaya ya Karatu.Alisema misaada hiyo itapelekwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro ili uwe mchango wao katika kuboresha huduma za malazi na mlo kwa wagonjwa, hasa kwa wale wa kipato cha chini.
Kauli ya Mchungaji
Mchungaji Mwasapila baada ya kusikia tetesi zilizozagaa jana kwamba serikali ina mpango wa kusitisha huduma zake, aliwaambia waandishi wa habari kuwa suala la kuzuiwa utoaji wa dawa linahitaji muda kwa kuwa linagusa imani ya watu pia."Nitakuwa siwatendei haki hawa maelfu ya watu waliopo hapa labda wakiisha tunaweza kujua la kufanya," alisema Mchungaji Mwasapila na kuongeza kuwa hawezi kuwazuia wagonjwa ambao wanaendelea kufika kwake.
RC Arusha
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Raymond Mushi alisema jana kuwa ofisi yake inawasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kujua ni jinsi gani ya kukabiliana na hali ya Loliondo.Alisema serikali mkoani Arusha inaendelea kuhakikisha hali ya usalama na afya za watu zinakuwa bora kwani tayari vyoo vimechimbwa ili kuzuia magonjwa na pia ulinzi umeimarishwa.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye akizungumza na Mwananchi jana alisema wameongeza askari kulinda usalama katika kijiji hicho lakini imekuwa vigumu kuzuia watu kwenda.
"Sisi tunalinda usalama hatuzuii watu kwenda kwa sasa kwani bado taratibu zinapangwa na sasa hali ni nzuri," alisema Andengenye.Bado mamia ya watu kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi wanaendelea kumiminika katika kijiji hicho kupata dawa. Waliopata huduma hiyo jana ni wagonjwa waliokaa siku tatu katika kijiji hicho.
Viongozi wengine wa dini
Viongozi wa dini na siasa wameendelea kujitokeza kuitaka serikali imruhusu mchungaji huyo aendelee na tiba zake wakati huu ambao bado uchunguzi wa kimaabara unaendelea.Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamisi alisema Serikali inaweza ikaendelea kuichunguza dawa hiyo huku mchungaji huyo akiendelea na shughuli zake kwani ameonyesha kuwasaidia watu wengi.“Yule mchungaji ameonyesha nia ya kuwasaidia watu wapone na si kutaka kupata pesa hafanyi mambo yake kwa tamaa hivyo aachwe aendelee na shughuli zake,” alisema Sheikh Khamisi.
Endelea kusoma habari hii...............
Saturday, March 12, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment