Thursday, July 7, 2011

Andrew Chenge kikaangoni

Best Blogger Tips
Via Majira

SAKATA la ununuzi wa rada ya ulioingizia serikali hasara, limechukua sura mpya baada timu ya wabunge iliyotumwa Uingereza kufuatilia malipo ya
fedha hizo kutoka Kampuni ya BAE kupendekeza kuangaliwa uwezekano wa kuwafikisha wahusika hao mahakamani.

Pendekezo la timu hiyo iliyokuwa chini ya Naibu Spika, Bw. Job Ndugai na wenzake Bw. Azan Zungu, Bi. Angela Kairuki na Bw. John Cheyo yamefanana na yaliyotolewa na Kambi ya upinzani bungeni juzi, kuwa wahusika katika kesi hiyo washtakiwe.

Kamati ya Ndugai ilisema kuwa pamoja na kesi hiyo kufungwa au kumalizika nchini Uingereza lakini Tanzania inayo nafasi ya kuwaburuta mahakamani watuhumiwa wa kashfa hiyo.

Ingawa timu hiyo haikutaja majina ya wahusika, miongoni mwa waliokuwa wanachunguzwa na Taasisi ya Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO), ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa sakata hilo, Bw. Andrew Chenge, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Idris Rashid na mfanyabiashara Sailesh Vithlan.

Lakini baadaye jioni, akijibu hoja za wabunge kwenye kuhitimisha mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma jana, Waziri wa Utawala Bora, Bw. Mathias Chikawe alimkingia kifua Bw. Chenge akisema Uingereza ilikwishamsafisha na hivyo hastahili kushtakiwa.

Mbali na wabunge hao kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka kwa watuhumiwa hao zikiwemo za kuwafikisha mahakamani, pia wamelitaka bunge kutenga muda wa kujadili suala hilo ili wajue undani wake.

Akikabidhi taarifa ya safari hiyo kwa Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda jana, Bw. Ndugai alisema kuwa baada ya kamati hiyo kujadiliana na SFO, wameona bado kuna uwezekano wa kuchukua hatua zaidi kwa wahusika wote.

“Wakati tukiwa huko, moja ya changamoto ambayo tulikumbana nayo ni pale tulipohojiwa ni hatua gani tulizochukua kama nchi kuhusiana na suala hilo,” alisema Bw. Ndugai.

Alisema kuwa wao walijibu kwamba wamekwenda kwa nia ya kushinikiza kulipwa fedha zilizoamuriwa na Mahakama ya Uingereza kama chenji ya rada iliyouzwa kwa Tanzania kwa bei ya kuruka, kupitia serikalini badala ya asasi za kiraia za nchi hiyo, kwa kuwa ni za wananchi na wao ni wawakilishi wao, hivyo suala la kufungua kesi ni suala la serikali.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia alikuwa miongoni mwa timu hiyo, Bw. Mussa Zungu, alisema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika ziara hiyo, ni pamoja na bunge la Uingereza na Serikali kutambua mchezo mchafu uliofanywa na Kampuni ya kuuza zana za kijeshi iliyouza rada hiyo, BAE Sustem, kwa kuiba na kuidhalilisha Tanzania kwa kutaka kulipa fedha hizo kupitia asasi za kiraia.

Hata hivyo alisema kuwa Julai 19 mwaka huu, timu hiyo imekaribishwa kwenye mjadala wa wazi ambao utakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo SFO, BAE, Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Kimataifa, Wizara ya Sheria ya Uingereza kwa lengo la kuweka mambo wazi kuhusiana na kitendo kilichofanywa na BAE, pia hiyo itakuwa ni fursa kubwa kwa timu ya bunge la Tanzania kuhoji maswali mbalimbali kuhusiana na mchakato huo.

Timu hiyo inataka fedha hizo zilipwe kwa riba inayoendelea kupatikana kutokana na fedha hizo kuwa katika akaunti ya BAE ambako zimehifadhiwa.

Kutokana na hali hiyo, wameitaka serikali kushirikiana na bunge kuhakikisha fedha hizo zinarudi na kuwa endapo hazitarudi mpaka Septemba 2011 hatua zaidi zichukuliwe kwa kampuni ya BAE.

Bw. Musa Zungu alisema kuwa hata baada ya kukutana na wahusika wa kampuni ya BAE, bado wamebaki na msimamo wao kuwa fedha hizo si tozo bali ni msaada.

Aidha timu hiyo pia ilikutana na Mkurugenzi wa SFO ambaye aliomba radhi kwa Serikali ya Tanzania kutokana na kushindwa kuishirikisha katika kesi hiyo wakati ikiendeshwa.

Mara kadhaa, Chenge amekuwa akikana kuhusika kwa namna yoyote na ufisadi huo wa rada na mara ya mwisho alijitokeza hadharani na kutangaza usafi wake baada ya SFO kuitimisha kesi hiyo bila kutaja chochote juu yake.

Utetezi wa Chikawe

Waziri Chikawe jana aliweka msimamo kwa niaba ya serikali kuwa
haiko tayari kumchukulia hatua yoyote Bw. Chenge kwa tuhuma za ununuzi wa rada hiyo.

Ilisema kuwa haina ushahidi wowote dhidi ya Bw. Chenge kuhusiana na tuhuma zinazoelekezwa kwake hasa kwenye sakata la ununuzi wa Rada ambao unadaiwa ulighubikwa na rushwa.

Hata hivyo, Bw. Chikawe alisema kuwa kama kuna mbunge yoyote au mtu yoyote mwenye ushahidi dhidi ya Bw. Chenge autoe na serikali itafanyia kazi siku hiyo hiyo.

“Suala la Rada limezungumzwa sana na limepotoshwa kwa kiasi kikubwa, SFO kwa kushirikiana na TAKUKURU walifanya uchunguzi wa kashfa hiyo na kubaini kuwa kwa hapa Tanzania hakuna mtu hata mmoja aliyehusika bali waliobainika katika makosa hayo ni watuhumiwa watatu kutoka nchini Uingereza,” alisema Bw. Chikawe.

Alisema kuwa waliohusika na kashfa hiyo, ni Bw. Sailesh Vithlan ambaye alikuwa dalali wa rada hiyo, Meneja Biashara wa Kampuni ya BAE, Bw. Jonathan Calman na mwingine aliyetajwa kama Bw. Christopher.

“Tutafanya kama kanisani kuwa mwenye ushahidi alete na asipoleta  hatutakwenda mahakamani kwa kuwa hatuna ushahidi, mahakamani huwezi ukaenda mikono mitupu ni lazima uwe na ushahidi wa kutosha...Chenge hatuna ushahidi naye na hili suala sasa nadhani mngeliacha,” alisema Bw. Chikawe.

Msimamo wa Upinzani

Juzi, Kambi ya Upinzania ilipinga fedha za rada kulipwa kupitia serikalini kwa madai kuwa haiaminiki na hasa ikizingatiwa kuwa fedha hizo zilipotelea mikononi mwake.

Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Sazan Lyimo alisema, "Kambi ya upinzani tunaona kuwa bila watuhumiwa hao kuchukuliwa hatua, ni dhahiri kuwa taifa haliwezi kuwa na uhakika wa kuzilinda vizuri fedha hizo za rada pindi zikilipwa pamoja na fedha zingine za umma ambazo zinaendelea kupotea kwa kuwa umekuwa ni utamaduni wa serikali kutochukua hatua.

“Tunataka Bunge lako tukufu lijadili na liazimie kuanzishwa kwa akaunti ya muda ya fedha za rada, itakayosimamiwa kwa pamoja na wawakilishi wa Asasi zisizo za kiserikali za Tanzania, wawakilishi wa sekta binafsi na mwakilishi wa serikali na tunataka fedha hizi zilipwe haraka iwezekanavyo kupitia akaunti hiyo,” alisema Bi. Lyimo.
Endelea kusoma habari hii.........................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits