Via New Habari
VIONGOZI wawili, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba; na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, wanaumwa.
Wamelazwa katika Hospitali ya Apollo iliyopo katika mji wa Hyderabad, nchini India.
Profesa Lipumba alifika hospitalini hapo siku tano zilizopita kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Kwenye uchunguzi huo, kwa mujibu wa watu walio karibu naye, ilibainika kuwa anasumbuliwa na maradhi ya figo.
Juzi, Profesa huyo wa uchumi alifanyiwa upasuaji. Alipoombwa azungumzie maendeleo ya afya yake, hakuwa tayari kufanya hivyo kwa maelezo kwamba bado alikuwa akikabiliwa na ‘ulevi’ wa dawa.
Aliahidi kuzungumza leo au kesho kadri afya yake itakavyoruhusu. Baadhi ya watu walio karibu na mwanasiasa huyo walisema maendeleo yake kiafya yanaridhisha.
Kwa upande wake, Profesa Mwandosya amelazwa hospitalini hapo kwa zaidi ya wiki mbili sasa.
Imeelezwa kwamba waziri huyo aliugua ghafla wakati akishiriki Mkutano wa Bajeti mjini Dodoma. Alikodishiwa ndege kwa dharura na kupelekwa Muhimbili. Hata hivyo, hali yake iliendelea kuwa mbaya na kulazimika kupelekwa nchini India.
Watu walio karibu na Profesa Mwandosya walisema kwamba anasumbuliwa na maradhi ya uti wa mgongo.
“Mheshimiwa Waziri anasumbuliwa na uti wa mgongo, kuna pingili imelika,” kilisema chanzo chetu.
Ilielezwa kwamba Waziri Mwandosya ilikuwa arejee nchini jana ili awahi kusoma bajeti ya wizara yake, lakini hali yake ilibadilika ghafla kabla hajaondoka.
Kubadilika kwa hali yake kuliwalazimu madaktari wamshauri aendelee na matibabu.
“Hali ilibadilika ghafla, ikalazimu apelekwe katika chumba cha x-rays, ana maumivu makali, lakini wananchi wasiwe na wasiwasi,” kilisema chanzo chetu.
Watanzania wengi wamekuwa wakienda kutibiwa nchini India. Hatua hiyo inatokana na upungufu wa vifaa uliopo nchini. Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha vifaa na wataalamu wanapatikana ili kupunguza mzigo kwa Serikali wa kugharimia matibabu ya raia wake.
Tayari mipango madhubuti imeshakamilika kwa ajili ya kufanya upasuaji wa moyo na usafishaji figo hapa hapa nchini.
Friday, July 1, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment