Via Uhuru
UAMUZI kuhusu hatima ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, utajulikana baada ya Rais Jakaya Kikwete kurejea nchini kutoka Afrika Kusini. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari, baada ya kuzindua meza ya maabara inayohamishika katika viwanja vya Bunge mjini hapa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa awali kuhusu safari ya Rais Kikwete nchini Afrika Kusini, atarejea nchini leo. Pinda alisema ameshawasiliana na Rais Kikwete aliye nchini Afrika Kusini kikazi, ambaye ameahidi kutoa uamuzi atakaporejea nchini. "Nimeshawasiliana na rais, ameniambia atakuja kutoa uamuzi akifika nchini.
Mheshimiwa rais ameona si busara kutoa uamuzi wa jambo kama hilo akiwa kwenye mkutano, hivyo ameahidi kulitolea uamuzi akirejea," alisema. Akizungumzia tetesi zilizozagaa kuwa Jairo amejiuzulu wadhifa wake, Waziri Mkuu Pinda alisema hana taarifa rasmi. Waziri mkuu alisema endapo kungekuwa na taarifa hizo angezipata lakini kwa wakati huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hakuwa na taarifa yoyote.
"Mwenyewe nimesikia imeandikwa katika gazeti moja lakini kwangu sina taarifa, labda kama aliandika barua na kuipeleka huko sijui," alisema Waziri Mkuu Pinda. Gazeti moja nchini (si Uhuru) liliandika habari jana kuwa Jairo amejizulu.
Jairo aliingia matatani baada ya kudaiwa kuandika barua ya kuzichangisha fedha taasisi na idara zilizo chini ya wizara, ambapo kila moja ilitakiwa kuchangia sh. milioni 50 kufanikisha upitishwaji wa makadirio ya matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/2012.
Akizungumzia suala hilo bungeni juzi, Waziri mkuu alisema ameshindwa kutoa uamuzi wa kumtimua kazi kwa kuwa kufanya hivyo ni kuingilia madaraka ya rais.
Wednesday, July 20, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment