Monday, July 11, 2011

Kikwete amjenga Zitto

Best Blogger Tips
Via Tanzania Daima

SHEREHE za kuzaliwa upya kwa taifa la Sudan Kusini zilizofanyika juzi mjini Juba, ziliibua hisia mpya katika siasa za Tanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe, kuandamana kuhudhuria tukio hilo la kihistoria.

Ziara hiyo ilifanyika baada ya Rais Kikwete kumaliza safari ya kikazi mkoani Kigoma wiki iliyopita, ambako alizindua miradi kadhaa, ikiwamo ya Barabara ya Mwandiga – Manyovu inayopita katika Jimbo la Kigoma Kaskazini linalowakilishwa na Zitto.

Wakiwa Sudan, Kikwete na Zitto walipata fursa ya kusalimiana na kuzungumza na viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo, akiwamo Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir.

Safari hiyo ya Zitto na Kikwete imezua maswali miongoni mwa wadadisi wa siasa wanaofuatilia mwenendo wa rais anayekaribia kuondoka madarakani na mwanasiasa kijana katika harakati za mageuzi nchini.

Ingawa inajulikana kuwa Kikwete na Zitto wamekuwa na uhusiano mzuri kikazi, licha ya kupingana kiitikadi, ziara yao ya juzi iliongeza minong’ono, hasa baada ya Zitto kuvujisha sehemu ya mazungumzo kati ya rais na yeye (Zitto) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, walipokuwa kwenye hafla ya uzinduzi wa barabara mkoani Kigoma.

Kwa mujibu taarifa zilizobandikwa na Zitto katika ukurasa wake wa facebook siku chache zilizopita, Rais Kikwete aliwanong’oneza yeye na Kafulila kwamba asingependa baada ya kustaafu kwake nchi iongozwe na rais ‘mzee’ kama yeye.

Rais Kikwete, ambaye aliingia madarakani kwa kampeni ya “ujana” huku akiwa na umri wa miaka 55 mwaka 2005, aliwaambia kina Zitto:
“Msikubali atakayenirithi awe wa rika langu, sasa kizazi chenu kijiandae.”

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kauli hiyo, kama ilitolewa na Rais Kikwete kweli, ililenga kuhamisha mjadala wa kisiasa kuhusu mrithi wa Kikwete nje na ndani ya CCM.

Inafahamika kwamba wanasiasa “wakali” ambao Rais Kikwete anawaogopa, na ambao wameonyesha nia ya kuutaka urais baada yake, ni watu wa makamo kama yeye.

Vile vile, wananchi wanapokuwa wanajadili mustakabali wa nchi, suala la umri, dini, jinsia na eneo analotoka mtu, havijawahi kuwa vigezo vinavyotumika kumuunga mkono mgombea.

Lakini kwa taifa lililoshuhudia siasa zenye mrengo wa kijinsia katika kumpata Spika wa Bunge, na kauli za udini kwenye kampeni mara baada ya Uchaguzi Mkuu, haliwezi kupuuza kauli hizi za kigezo cha umri.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wamekuwa wakisisitiza kuwa ujana au uzee si hoja.
Wapo pia wanaosema kwa msisitizo mkubwa kwamba mgombea yeyote wa CCM atakayebebwa na Rais Kikwete ataanguka. Wanatoa sababu kadhaa.

Kwanza, wanasema nguvu yake ndani ya mfumo inalegalega kiasi cha kumnyima uwezo wa kushinikiza wanachama wakubaliane naye katika chaguo atakalowaletea.

Na kwa msingi wa makundi ndani ya CCM, kuna watu wamejipanga kwamba yeyote atakayeonekana kubebwa na JK lazima “apigwe chini.”

Pili, wachunguzi wanasema historia inaonyesha kuwa hakuna aliyebebwa na rais anayeondoka madarakani, akashinda.

Wanatoa mifano ya jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1985, alivyomtaka Dk. Salim Ahmed Salim, lakini akazidiwa kete na wajumbe waliomtaka mzee Ali Hassan Mwinyi. Hata mwaka 1995 alimtaka Dk. Salim, ikashindikana baada ya Dk. Salim mwenyewe kukataa kwa kutazama upepo wa kisiasa wa wakati huo.
Endelea kusoma habari hii...........................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits