RAIS Jakaya Kikwete amemsimamisha kazi Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, ili Tume atakayoiunda Spika wa Bunge, Anne Makinda imchunguze.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameliarifu Bunge kuwa, Rais ameamuru Jairo aende likizo, na kwamba, Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kwa tume itakayoundwa.
Pinda ametoa taarifa hiyo kwa wabunge mjini Dodoma wakati anajibu maswali ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Mbowe alihoji kwa nini Jairo aendelee na kazi wakati Bunge limeamua kuunda tume kuchunguza kwa nini limedhalilishwa na pia kuchunguza mchakato wa kukusanya fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha.
Mbunge huyo alimuuliza Waziri Mkuu, uhalali wa kauli ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kwamba, suala la idara kuchangia fedha za kupitisha bajeti za Wizara ni la kawaida.
Kwa mujibu wa Mbowe, bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ilijadiliwa kwa siku tano, zilitumika shilingi milioni 174/- kwa ajili hiyo, lakini bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini imegharimu shilingi milioni 578/-.
Mbunge huyo wa Hai (Chadema) alimuuliza Pinda, waliohusika katika ubadhirifu wa fedha Wizara ya Nishati na Madini wamechukuliwa hatua gani za kinidhamu, na je kweli ni sera ya Serikali kuchangisha fedha kwa ajili ya bajeti za Wizara kama alivyosema Luhanjo?
Luhanjo juzi alimuamuru Jairo arudi kazini jana kwa kuwa uchunguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) haukumtia hatiani. Bunge jana lilisema, uamuzi alioutangaza Luhanjo umelidhalilisha na amemfedhehesha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Jairo jana alikwenda ofisini kwake wizarani jijini Dar es Salaam, wafanyakazi wakampokea kwa shangwe na vigelegele huku wakiimba kwamba wana imani naye.
Wabunge walisema jana bungeni kuwa, taarifa ya uchunguzi ya CAG kuhusu tuhuma kwamba, Jairo alichangisha Sh. Bilioni moja ili kuwezesha bajeti ipitishwe bungeni ilistahili kupelekwa bungeni waijadili kabla Serikali kutoa uamuzi.
Wabunge jana walijadili kauli ya Luhanjo kama jambo la dharura baada ya wabunge kukubali hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto aliyoitoa jana asubuhi kabla ya kipindi maswali na majibu na kuifafanua baada ya Kamati ya Bunge ya Uongozi kukutana katika ukumbi wa Spika.
Zaidi ya robo tatu ya wabunge waliokuwa ukumbini wakiwemo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliunga mkono hoja ya Zitto. Ndugai, alisema , hoja ya Zitto ni ya msingi kwa kuwa Bunge limedharauliwa.
“Kwa sababu Bunge ni mhimili, hatuwezi kudharauliwa kirahisi”alisema Ndugai na kusisitiza kwamba,Wabunge hawawezi kukaa kimya wakati Waziri Mkuu anadhalilishwa.
“Kama dharau inaweza ikatokea basi huko huko lakini sio ndani ya Bunge hili” amesema Ndugai baada ya wabunge kuijadili hoja ya Zitto na kusisitiza kwamba, kwa kuwa suala hilo lilianzia bungeni, taarifa ya CAG ingepelekwa kwanza kwenye mamlaka hiyo kabla ya uamuzi wa Serikali.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zainab Vullu, alisema, wabunge wamepewa jukumu la kuisimamia na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi hivyo kauli ya Luhanjo imewadhalilisha, na limepokwa mamlaka yake.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, alisema, suala hilo lina maslahi kwa Taifa, taarifa ya CAG ingepelekwa kwanza bungeni itendewe haki. Sendeka alisema, Waziri Mkuu amefedheheshwa kwa kuwa kiongozi huyo wa Serikali Bungeni alisema, kama angekuwa yeye angemchukilia hatua Jairo, na pia Bunge limedhalilishwa.
Kwa mujibu wa Sendeka, kauli ya Luhanjo imelilidhalilisha Bunge na imekiuka Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge na ibara ya 100 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Mbunge huyo alitumia Kanuni 117 ya Bunge kuomba iundwe kamati teule ya Bunge kuchunguza jambo hilo ukiwemo utaratibu wa Jairo kukusanya fedha za kupitishia bajeti hasa ikizingatiwa kuwa, kila Waziri huwa na fungu la kugharamia bajeti kila idara zikiwemo fedha za kununulia mafuta.
Sendeka aliomba wabunge waunge mkono hoja yake ili kulinda hadhi ya Bunge. Wabunge walikubali isipokuwa mawaziri na manaibu mawaziri.
Wakati anatoa hoja hiyo, Zitto alisema, kwa kuwa jambo hilo lilianzia bungeni wakati Mbunge wa Beatrice Shelukindo alipolieleza Bunge kuwa ana barua ya Jairo kuzitaka idara zichangie shilingi milioni 50 kila moja, wabunge walistahili kuijadili ripoti ya CAG kabla ya Serikali kufanya uamuzi.
Zitto alilieleza Bunge kuwa, kauli ya Luhanjo ni dharau kwa Waziri Mkuu, na imeingilia hadhi, kinga na madaraka ya Bunge kwa kuwa wabunge ndiyo wana mamlaka ya kuisimamia Serikali.
Zitto alipendekeza kwamba, shughuli na hoja zote za Serikali bungeni zisitishwe, kwanza wabunge waijadili taarifa za CAG kwa kuwa Bunge limepokwa nafasi yake.
Ndugai amewaeleza wabunge kuwa, Spika wa Bunge, Makinda, ataunda tume kuchunguza kudharauliwa kwa Bunge, na kukusanywa kwa fedha kwa ajili ya kupitishwa bajeti yaWizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Bunge tume hiyo itapaswa kufanya kazi haraka ili taarifa yake ijadiliwe katika mkutano ujao wa Bunge.
Chanzo: HabariLeo