Sunday, August 7, 2011

Kondoo mwenye Korani azaliwa

Best Blogger Tips
Via HabariLeo

KIJIJI cha Uduru wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kimegeuka eneo la utalii baada ya waumini wa madhehebu ya Kiislamu kutoka maeneo mbalimbali wilayani humo na maeneo jirani, kwenda kumshuhudia kondoo aliyezaliwa ameandikwa maneno mwilini kwa lugha ya Kiarabu.

Waumini hao walifurika kijijini hapo juzi baada ya sala ya Ijumaa kumshuhudia kondoo huyo aliyezaliwa wiki tatu zilizopita na kuacha watu midomo wazi kutokana na kuwa na maandishi yanayosomeka kiarabu ubavuni, yakitafsiriwa kwa Kiswahili kama Yasini.

Kondoo huyo aliyezaliwa katika familia moja ya waumini wa dini ya Kikristo, aliwavuta
waumini wengi kijijini hapo na kutoka nje ya wilaya na mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo la ajabu na la kihistoria ambalo halijawahi kutokea.

Akizungumza na HABARILEO Jumapili kijijini hapo, mmiliki wa kondoo huyo, Grace
Massawe (55) alisema kondoo huyo alizaliwa takribani wiki tatu zilizopita na hakuwahi kutambua kwamba beberu huyo alikuwa na maandishi hayo, kutokana na kutotolewa nje na mama yake.

Grace alisema baada ya kondoo huyo kuzaliwa, mama yake alibadilisha tabia na kukaa ndani ambapo awali alikuwa akila chakula nje na wenzake, lakini aligundua maandishi hayo baada ya kumtoa nje mwenyewe.

Alisema awali aliona herufi ya W yenye rangi ya dhahabu, lakini siku zilivyozidi kwenda neno hilo lilizidi kukua na kubadilika rangi na kuwa jeupe zaidi, hali iliyompa wasiwasi na kutafuta msaada ili kutambua maana ya maandishi hayo kutoka kwa waumini wa Kiislamu.

“Baada ya waumini wa Kiislamu kufika hapa nyumbani walibaini maandishi hayo ubavuni mwa kondoo huyo kuwa ya Kiarabu yanayosomeka kuwa Yasini,” alisema Grace.

Alisema waumini hao walimweleza kuwa neno hilo ni muhimu sana katika Kitabu Kitakatifu cha Korani, ambalo ni kama kitovu cha kitabu hicho, pia ni moja ya sura muhimu ndani ya kitabu hicho.

Katika hatua nyingine, Grace alisema katika ufugaji wake wa kondoo hakujawahi kutokea tukio la ajabu kama hilo na kueleza kuwa kondoo aliyemzaa alikuwa ni uzao wake wa mara ya pili ambapo awali alizaa kondoo wa kawaida.

Alisema kutokana na kondoo huyo kuvuta hisia za watu wengi, pia viongozi wakubwa wa dini hiyo walifika kushuhudia maajabu hayo, akiwamo Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu
Tanzania (Bakwata) wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shehe Rashid Mallya, na Shehe Mkuu wa Wilaya ya Hai, Juma Lyimo.

Baadhi ya waumini waliofika kumshuhudia kondoo huyo na kuzungumza na gazeti hili Aman Ramadhan na Yacoub Mushi wa Lyamungo, walisema tukio hilo ni muujiza wa Mungu uliojitokeza, hususan kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Juhudi za kumtafuta Shehe Mallya kuzungumzia tukio hilo, zilishindikana baada ya simu yake kuita bila kupokewa.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits