BUNGE jana lilisitisha kwa muda shughuli zake za kawaida kujadili hatua ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kumrejesha kazini Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kabla ya Bunge kujadili Ripoti ya uchunguzi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Luhanjo kukutana na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi na kuutangazia umma kwamba kutokana na matokeo ya uchunguzi huo kutomtia hatiani anaamuru Jairo arejee ofisini mara moja.
“Kutokana na matokeo haya ya uchunguzi wa awali, mimi kama Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu Mkuu Nishati na Madini, sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma. Ninaamuru David Jairo arejee kazini kuanzia siku ya Jumatano.”
Hata hivyo, uamuzi huo wa Luhanjo jana uliamsha hasira za wabunge bila kujali itikadi zao za kisiasa ambao ambao walitaka Bunge lisitishe kujadili shughuli zozote kutokana na hatua hiyo ya Katibu Mkuu Kiongozi wakisema ni kudharau Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Hoja ya Zitto
Hoja hiyo iliwasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) muda mfupi kabla ya kuanza kwa kipindi cha maswali na majibu. Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni alitoa hoja kutaka Bunge lisitishe kujadili hoja zote za Serikali hadi hapo ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyomsafisha Jairo itakapofikishwa bungeni na kujadiliwa.
Zitto alianzisha moto huo mnamo saa 3:17 asubuhi ikiwa ni dakika moja tu baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kutangaza taratibu za safari ya wabunge kwenda Zanzibar kwa ajili ya mazishi ya Mbunge Mussa Khamis Silima aliyefariki juzi.
Alitumia kanuni ya 51 kulieleza Bunge kuwa kitendo kilichofanywa na Luhanjo kilikiuka haki, maadili na madaraka ya Bunge na hivyo akataka wabunge wenzake wamuunge mkono ili wagome kufanya shughuli zozote za Serikali hadi hapo ripoti ya CAG kuhusu tuhuma dhidi ya Jairo itakapowasilishwa rasmi bungeni.
“Mheshimiwa Naibu Spika, jana kupitia vyombo vya habari tulimsikia Katibu Mkuu Kiongozi kupitia vyombo vya habari akieleza kuwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili Jairo si za kweli na kwamba anatakiwa kurudi kazini kuanzia leo (jana),’’ alisema Zitto na kuongeza:
“Mheshimiwa Naibu Spika unafahamu ya kwamba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizungumza ndani ya Bunge hili ya kwamba angekuwa ni yeye angeshamchukulia hatua Ndugu Jairo kuhusu vitendo alivyofanya, hivyo basi naomba nitoe hoja kwamba Bunge lisitishe hoja yoyote ya Serikali mpaka itakapoleta bungeni taarifa ya CAG kuhusiana na uchunguzi huo.”
Baada ya kutoa hoja hiyo, Zitto aliungwa mkono na wabunge zaidi ya nusu waliokuwamo ndani ya ukumbi, hali ambayo ilimlazimisha Naibu Spika wa Bunge, Ndugai, kuitisha Kamati ya Uongozi kwa dharura kujadili suala hilo.
Hoja ya Lukuvi
Baada ya hoja ya Zitto, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama kupinga hoja hiyo akisema Mbunge huyo hakufuata taratibu zilizotakiwa ambazo ni kuwasilisha kusudio kabla ya kutoa hoja rasmi.
“Mheshimiwa Naibu Spika, najua jambo hili lina public interest (masilahi ya umma), lakini kanuni zinasema kuwa mbunge anayetaka kuwasilisha jambo lolote linalohusiana na shughuli za Bunge atafanya hivyo wakati unaofaa na uliowekwa na kanuni na atakuwa amemwarifu Spika mapema kuhusu kusudio lake, hivyo ulitakiwa kuwasilishiwa mapema ili uweze kuamua,’’ alisema Lukuvi.
Akijibu hoja hiyo, Ndugai alisema: “Wakati nasoma matangazo mbalimbali kuhusiana na kifo cha Mbunge, nilipata taarifa kutoka kwa Zitto kuhusu kunitaarifu juu ya jambo hilo, hivyo basi, hoja iliyotolewa na Zitto imetolewa kwa wakati na ilifuata utaratibu unaotakiwa.’’
Endelea kusoma habari hii.................
Thursday, August 25, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment