MADAKTARI waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo ambao Serikali iliwafutia
vibali vya kazi, wamesalimu amri na kuamua kumuangukia aliyekuwa
mwajiri wao ili awarudishe kazini.
Serikali iliwafukuza kazi madaktari hao baada ya
kutangaza mgomo usio na kikomo Juni mwaka huu, hadi madai yao
yatakapofanyiwa kazi ambapo mgomo huo ulisababisha vifo kwa baadhi ya
wagonjwa waliokosa huduma za matibabu.
Akizungumza na waandishi
wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
walioathirika na mgomo, Bw. Paul Swakala, alisema wameamua kuomba
msamaha kwa Rais Jakaya Kikwete na Watanzania wote baada ya kubaini
kuwa, wagonjwa wengi waliathirika na mgomo huo.
Alisema
walishindwa kuuepuka mgomo huo kutokana na mazingira ya wao kufanya kazi
na Madaktari Bingwa kwani mikataba yao, haikuwaruhusu kufanya kazi ya
kutoa matibabu peke yao.
“Tunafahamu kuwa, Watanzania wengi
waliathirika mgomo ule, tunawaomba radhi sana kwa usumbufu walioupata na
tunakiri kuwa kila mmoja wao alichokizwa na uamuzi wetu.
“Japo
nchini kwetu utamaduni wa kuomba radhi hadharani haupo, sisi tumeamua
kufanya hivi kwa sababu tumekosa na hakuna binadamu aliye kamili wote
tunakasoro,” alisema Bw. Swakala.
Aliongeza kuwa, wanatambua na
kuunga mkono juhudi za Rais Kikwete katika kuboresha huduma za afya
nchini licha ta changamoto nyingi zinazoikabili sekta hiyo.
“Tunamuomba
radhi sana Rais Kikwete na Serikali yake kwa usumbufu uliosababishwa na
mgomo, pia tunatambua jitihada zake za kutafuta suluhu ya mgomo
uliopo,” alisema.
Aliwahakikishia Watanzania kuwa, kuanzia sasa
hawako tayari kushiriki mgomo kwa namna yoyote kwabni kufanya hivyo ni
kuweka rehani maisha ya wagonjwa.
Bw. Swakala alisema wanajutia
kosa hilo na wako tayari kulejea kazini ili kuwahudumia Watanzania kwa
moyo mweupe na wanayo dhamira ya kounana na Rais Kikwete ana kwa ana ili
kumuomba radhi.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Bw.
Swakala alisema madaktari ambao wamesaini fomu za kuomba radhi ni 200
kati ya 364 waliofutiwa vibali vya kazi.
“Mimi nimesoma kwa
gharama za sh. milioni 35, sioni faida ya kukaa mtaani wakati Watanzania
wakiendelea kupata shida ya matibabu,” alisema Bw. Swakala.
Akizungumzia
suala la vifaa ambalo ni moja ya sababu iliyowafanya wagome, Bw.
Swakala, wao wanaamini Rais Kikwete na Serikali yake itaboresha
mazingira ya huduma za afya.
“Chama cha Madaktari nchini (MAT) ni
cha hiari, hatuungani na msimamo wao, wanachama walionao ni madaktari
wenye usajili wa kudumu si kama sisi, hatulazimishwi kujiunga nao,”
alisema.
Madaktari hao walifanya mgomo huo ili kuishawishi
Serikali iboreshe mazingira ya kazi, nyongeza ya mishahara na marupurupu
mengine.
Source: Tanzania Daima
Tuesday, September 18, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment