TUKIO la kuuawa kwa mwandishi wa habari wakati polisi wakipambana na
wafuasi wa Chadema mkoani Iringa, limelitikisa jeshi hilo na jana Mkuu
wake (IGP), Said Mwema alilazimika kujifungia na vigogo wa polisi Mkoa
wa Iringa kujadili suala hilo.
Wakati IGP Mwema akifanya mkutano
huo, uliodumu kwa zaidi ya saa mbili na nusu, Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi amelazimika kukatisha ziara yake ya kikazi
Afrika Kusini na kurejea nchini kushughulikia suala hilo.
Mwema
alienda Iringa jana na kuitisha mkutano huo uliowahusisha pia viongozi
wa Chadema, akiwamo Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa katika mazingira
yaliyoelezwa kuwa na ulinzi mkali.
Hii ni mara ya kwanza IGP Mwema
kwenda mwenyewe kwenye mikoa kunakotokea vurugu kati na vyama vya siasa
na baadaye mauaji ya raia.
Julai 15, mwaka huu vurugu za aina
hiyo zilitokea mkoani Singida ambako Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa
CCM Kata ya Ndago wilayani Iramba, Yohana Mpinga aliuawa kwa kupigwa na
silaha za jadi.
Pia mkoani Morogoro, Ally Zona aliuawa katika
vurugu zilizoibuka baina ya polisi na wafuasi wa Chadema katika haraka
za jeshi hilo kuwasambaratisha wafuasi hao kwa kile ilichoeleza kuwa
maandamano yao yalipigwa marufuku.
Katika vurugu zote hizo, IGP amekuwa akituma wawakilishi au kutumia polisi kwenye mkoa husika kushughulikia matatizo hayo.
Makubaliano ya kikao
Taarifa
kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa polisi imekubaliana na
Chadema na Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)
kusitisha majadiliano yote yanayohusu kifo cha mwandishi huyo hadi
mazishi yake yatakapokamilika.
Mwenyekiti wa UTPC, Kenneth
Simbaya alisema baada ya mkutano huo kuwa wamekubaliana kuwa na mkutano
mwingine baada ya shughuli za mazishi kukamilika.
“Tulichoomba
kifanyike ni kwamba, tumzike mwenzetu halafu majadiliano mengine juu ya
ilikuwaje kwa nini na nini kifanyike kwa siku za usoni yatakuja,”
alisema Simbaya.
Alisema sasa wanasubiri mwili wa Mwangosi ufanyiwe
uchunguzi na wataalamu kutoka Dar es Salaam kabla ya kukabidhiwa kwa
ndugu kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.
Katibu wa Chama cha
Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Francis Godwin alisema
uchunguzi wa awali wa IPC unapingana kwa asilimia zote na taarifa ya
jeshi hilo kwa kuzingatia taarifa zilizotolewa na baadhi ya waandishi
waliokuwapo katika tukio hilo.
“Taarifa kutoka katika vyanzo
vyetu zinaonyesha kwamba Mwangosi alipigwa kwa virungu kabla ya
kulipuliwa na bomu hilo ambalo kwa vyovyote vile mhusika wake mkuu
anaweza kuwa jeshi hilo na ili taarifa hiyo potofu isiendelee kuugubika
umma, IPC imeamua kutoa tamko linalolenga kuviarifu vyombo huru
viingilie kati uchunguzi,” alisema Godwin.
Nchimbi akatisha ziara
Waziri
wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi jana alilazimika kukatisha ziara
yake ya kikazi, Afrika Kusini na kurudi nchini ambako pamoja na mambo
mengine, atazungumza na waandishi wa habari leo kuhusu tukio hilo.
Nchimbi anarejea nchini wakati Naibu wake, Pereira Ame Silima akikataa kulizungumzia akisema uchunguzi umeshaanza.
Silima
alisema tukio hilo linachunguzwa kwa pamoja kati ya Mkuu wa Upelelezi
wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba na IGP Mwema... “Mwema na
Manumba wanaelekea Iringa ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa tukio hilo na
baadaye ndipo jeshi la polisi litaweza kueleza ni kitu gani hasa
kimetokea.”
Alisema kwa sasa lolote litakalozungumzwa juu ya tukio
hilo litakuwa ni hisia tu na ukweli utajulikana baada ya uchunguzi huo
kukamilika.
Channel Ten yanena
Uongozi wa kampuni ya Africa
Media Group ambao wanamiliki Kituo cha Televisheni cha Channel Ten,
umeitaka Serikali kuanzisha uchunguzi huru ili kubaini sababu na
mazingira ya kuuawa kwa mwandishi huyo ambaye alijiunga na kampuni hiyo
mwaka 2006.
Taarifa iliyotolewa na kampuni na kusainiwa na
Mhariri Mkuu wa Channel Ten, Dina Chahali imetaka uchunguzi huru
kufanyika na kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanachukuliwa hatua kwa
mujibu wa sheria.
“Tunalaani vikali tukio hili ambalo halikubaliki
kwa jinsi yoyote ile, tunataka kuanzishwa uchunguzi huru na hatimaye
nguvu za kisheria zitumike,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Chanzo: Mwananchi
Monday, September 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment