MAPENDEKEZO ya Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake
(UWT) wa CCM ya majina ya wagombea nafasi ya uenyekiti wa jumuiya hiyo
ngazi ya taifa, yameibua mlolongo wa tuhuma kuwa yalifikiwa kwa
upendeleo, rushwa na woga.
Tuhuma hizo zimetolewa na baadhi ya walioomba kuteuliwa kuwania nafasi
hiyo, ambao majina yao hayakupendekezwa na kamati wanayodai kuwa
ilifanya kazi kwa woga na kuwapendelea baadhi ya wagombea baada ya
kushawishiwa kwa rushwa.
Mbali ya malalamiko ya wagombea, taarifa kutoka ndani ya UWT zinaeleza
kuwa, uteuzi wa majina yaliyopendekezwa na kamati ya utekelezaji na
kupelekwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM umeibua ufa baina ya
wanajumuiya hiyo kwa kile kinachoelezwa baadhi yao kujiona wanatengwa
kwa sababu hawana watu wa kuwapigania dhidi ya wake wa vigogo wanaodaiwa
kuogopwa na kutetewa na waume zao.
Mmoja wa wagombea ambaye jina lake halikupendekezwa, Hamida Thabit,
katika mahojiano yake na gazeti hili kuhusu mwenendo wa mchakato wa
uteuzi alisema ulikuwa wa hovyo kwa sababu haukuzingatia sifa na uwezo
wa waombaji.
Alisema waombaji wenye sifa majina yao hayakupendekezwa kwa sababu
hawakuwa na pesa za kuwafurahisha wajumbe, na majina ya waombaji ambao
waume zao wana sauti ndani ya chama yalipitishwa kwa woga.
“Sijaridhika na mapendekezo ya kamati. Siyo kwamba nina uchu wa
madaraka, lakini wakati mwingine ukiona mambo yanakwenda kombo kiasi cha
kutisha ni lazima kusema. Na ninasema ili NEC ilione hili, itende haki
kwa sababu UWT ni waoga.
“Baadhi yetu majina yetu hayakupendekezwa kwa sababu hatuna pesa,
hatuna watu wa kututetea, hatuna wanaume wenye nyadhifa au sauti ndani
ya chama. Ni aibu kwa jumuiya iliyokomaa kama UWT kuchagua watu kwa
kuwaogopa, eti wasipochaguliwa watapiga kelele.
“Wabunge wenye majimbo, wana kazi za kila siku za kusimamia majimbo
yao, bado wanataka na kazi ngumu ya kuongoza umoja huu na majina yao
yanapitishwa, hiyo maana yake nini? Wanaachwa watu wenye sifa, wanaoijua
UWT,” alisema Hamida.
Alisema mwenendo wa sasa wa CCM unaonekana kuwa wa kifamilia zaidi kwa
sababu licha ya kuwa na wanachama wengi wenye sifa na uwezo wa kushika
nafasi za uongozi, bado nafasi hizo zinatolewa kwa kujuana na hasa kwa
kuangalia wake wa vigogo.
Alitolea mfano wa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, kuwa ni
mbunge wa jimbo ambaye ana jukumu la kuwatumikia wapiga kura wake, hivyo
hapaswi kukabidhiwa jukumu lingine la kuongoza UWT kwa sababu majukumu
yote ni mazito.
Pia alisema Maryrose Majinge hakupaswa kupendekezwa kwa sababu hana sifa zinazostahili kuwa kiongozi wa juu wa umoja huo.
“Anne Kilango ni mbunge wa jimbo, anawajibika kwa karibu sana kwa
wananchi wa jimbo lake, lakini bado anataka uenyekiti wa jumuiya.
Majukumu yote ni mazito, kwanini yeye tu majukumu hayo?
“Sophia Simba ni sawa kwa sababu yeye ni mwenyekiti hivyo anatetea
kiti chake na anao uzoefu wa uongozi ndani ya jumuiya, lakini hata huyu
Maryrose, ametokea umoja wa vijana moja kwa moja amerushwa hadi kwenye
uenyekiti, aanzie chini ajifunze na kupata uzoefu.
“Huu ni upendeleo wa wazi kabisa, unajua ukiwa na watoto watatu halafu
ukawa unampendelea mmoja tu, wengine lazima watalalamika na itafika
mahali watapachukia nyumbani, huko ndiko tunakokwenda.
“Kwa sababu lazima ieleweke kuwa kujua kupiga kelele siyo ujuzi wa
kiutendaji, kupiga kelele bungeni siyo kigezo cha kuwa kiongozi bora,”
alisema.
Alipoulizwa kama ana mpango wa kukata rufaa kupinga mapendekezo hayo,
alisema hana mpango huo kwa sababu anaamini hakuna kitakachofanyika
isipokuwa anabaki na matumaini NEC itatenda haki.
Mgombea mwingine aliyelalamikia mapendekezo ya kamati ya utekelezaji
ya UWT ni Hilder Kitana, ambaye alisema ingawa anayaheshimu maamuzi ya
kamati hiyo, amesikitishwa na kitendo chake cha woga.
Kitana alisema kamati hiyo imewaacha baadhi ya waombaji wenye sifa na
kuchukua majina ya watu ambao hawana rekodi ya uongozi ndani ya jumuiya,
lakini pia wenye majukumu ya kila siku kwa nafasi ambazo tayari wanazo.
“Wameamua wamependekeza majina hayo sawa, nayaheshimu. Lakini
nimesikitishwa na woga wa kamati hii. Tukienda kwa kuogopana kama
walivyokuwa wanasema ndani ya kamati hiyo hatutafika, tunaiua jumuiya.
“Mimi nimekuwa Mjumbe Kamati Kuu ya UWT, nimekuwa Mwenyekiti wa UWT
Mkoa wa Dar es Salaam, ninaijua jumuiya, sina jukumu kwa sasa
linalonibana moja kwa moja zaidi ya biashara zangu, halafu jina langu
linakatwa kwa sababu wanasema wakimuacha Kilango, anaongea sana na mke
wa mtu mkubwa itakuwa matatizo, atapiga kelele hadi kwenye vyombo vya
habari, huu ni udhaifu mkubwa,” alisema Kitana.
Kwa upande wake, Maryrose Majinge, alisema licha ya jina lake kupendekezwa, anasubiri maamuzi ya NEC.
Alisema nafasi za uongozi ndani ya CCM zinapaswa kuzingatia uwezo wa
utendaji badala ya kuchagua watu kwa sifa ya kuzungumza au kwa majina ya
wenzi wao.
Wiki iliyopita, kamati ya utekelezaji ya UWT iliyoketi mjini Dodoma
ilipendekeza majina ya wanachama wake watatu kwenda NEC ya CCM kwa ajili
ya kuwania uenyekiti wa jumuiya hiyo. Waliopendekezwa ni Mwenyekiti wa
sasa, Sophia Simba, Anne Kilango na Maryrose Majinge.
Chanzo: Tanzania Daima
Sunday, September 16, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment