Tuesday, October 25, 2011

Gaddafi azikwa kwa siri jangwani

Best Blogger Tips
MISRATA, Libya
MWILI wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Kanali Maummar Gaddafi umezikwa katika sehemu ya siri jana, baada ya kuuawa kwake na wapiganaji waliokuwa wakimpinga wiki iliyopita.

Mmoja wa waopiganaji hao alijitokeza kwa mara ya kwanza jana kupitia mkanda wa video akieleza kwamba yeye ndiye aliyechukua uamuzi wa kufyatua risasi na kumuua Gaddafi, kwa kuwa hakuona haja ya kumshikilia akiwa hai.

Maziko hayo yamefanyika baada ya kuwapo kwa mvutano baina ya wanafamilia wa Kanali Gaddafi na uongozi wa sasa wa Libya ambao ni Baraza la Mpito la Nchi hiyo (NTC) ambalo lilitangaza kuzika mwili huo kwa siri, ili kuficha mahali lilipo kaburi la kiongozi huyo wa Libya kwa miaka 42.

Mwili huo ulichukuliwa na kupelekwa kuzikwa kusikojulikana, baada ya ndugu na watu wake kadhaa wa karibu kuruhusiwa kushiriki katika sala maalum na taratibu zote za Kiislamu.

Mmoja wa wasemaji wa NTC alisema jana kuwa mwili wa Gaddafi, mwanae Mutassim pamoja na mmoja wa wasaidizi wake imezikwa, licha ya kuwapo kwa utata kuhusu pale ilipostahili kuzikwa.

Mvutano uliokuwapo ulitokana na ombi la ndugu wa kabila la Kanali Gaddafi ambao walikuwa wakitaka wapewe mwili wa kiongozi huyo ili wauzike mjini Sirte, alipozaliwa, lakini viongozi wa baraza la kitaifa la mpito walipinga ombi hilo.

Taarifa nyingine zinamnukuu msemaji wa NTC, Ibrahim Beitalmal akisema ndugu wachache wa familia ya Gaddafi walishiriki katika taratibu za ibada ya mazishi ya kiongozi huyo na dua, vilivyofanyika kwa kuzingatia taratibu za dini ya Kiislamu.

Hata hivyo, habari zaidi zinadai kuwa, baada ya sala hiyo, ndugu wa Gaddafi hawakuruhusiwa kuona sehemu ambayo kiongozi huyo amezikwa ambako kunadaiwa kuwa ni katikati ya jangwa.

Baadhi ya watu mjini Misrata wanasema miili ya watu hao watatu iliondolewa usiku kutoka sehemu ilipokiuwa imehifadhiwa katika harakati za kupanga mazishi hayo.

Raia wa Libya wamekuwa wakitembelea eneo hilo la bucha katika mji wa Misrata ambako miili hiyo ilipelekwa na kuhifadhiwa baada ya tangazo la kifo cha kiongozi huyo na baadhi ya walinzi wake, kujionea mwili wake ili kuthibitisha ukweli kuwa ameuawa.

Viongozi wa NTC walikuwa wanahofia kuwa huenda Kanali Gaddafi akizikwa katika sehemu ya wazi, kaburi lake litabadilishwa kuwa pahali patakatifu na wafuasi wake.

Pamoja na hilo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishinikiza uchunguzi ufanyike kubainisha jinsi alivyouawa Kanali Gaddafi, kwani picha za awali zilionyesha kuwa alikamatwa akiwa hai.

Kiongozi wa NTC, Mustafa Abdul Jalil, ametangaza kuwa uchunguzi utafanyika kuhusu hilo. Hata hivyo, kuna wale wanaohoji ikiwa kweli uchunguzi huo utakuwa wa wazi ikiwa mashirika ya kujitegemea hayakuhusishwa.

Katika video iliyotolewa jana, kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, kijana mpiganaji anayedai kumuua Kanali Gaddafi baada ya kukamatwa akiwa hai kwenye mtaro wa majitaka, alisema hakuona sababu ya kumuacha aendelee kuwa hai na kumkabidhi kwa uongozi wa NTC.

“Tulimkamata, nilimpiga katika paji la uso. Baadhi ya wapiganaji wenzangu walikuwa wakilazimisha kutaka tumpeleke na kumkabidhi akiwa hai. Niliamua kumpiga risasi mbili. Moja kichwani na nyingine kifuani,” alisema.

Katika kutaka kuthibitisha hilo, kijana huyo alionyesha kipande cha nguo ya Gaddafi kikiwa kimetapakaa damu na pete ya dhahabu ambayo alimvua baada ya kumuua.

Jaji Mkuu Tanzania awania nafasi ya Ocampo

Best Blogger Tips
Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman
 Jaji mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman ni mmoja kati ya watu wanne muhimu wanaoweza kushika nafasi ya Mwendesha Mashtaka katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa iliyoko The Hague, nchini Uholanzi.

Nafasi hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na Luis Moreno-Ocampo itakuwa wazi hapo mwakani baada ya Bw Ocampo kumaliza kipindi chake cha utumishi wa miaka tisa mwakani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AF, wagombea wengine ni pamoja na Naibu Mwendesha Mashtaka wa sasa Fatou Bensouda wa Gambia, ambaye wengi wanamwona kuwa analeta ushindani mkali.

Anaungwa mkono na Umoja wa Afrika ambao mara nyingi umemkosoa Moreno-Ocampo kwa kufungua uchunguzi wa mataifa ya Afrika pekee.

Katika orodha hiyo pia yupo Andrew Cayley, mwendesha mashtaka mwenza katika mahakama maalum ya Khmer Rouge nchini Cambodia anayetokea Uingereza.

Mwingine ni Robert Petit, ambaye ni mshauri kuhusu uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita katika Kitengo cha Mahakama nchini Canada.

Kamati ya iliyoundwa na nchi wanachama wa mahakama hayo awali ilikuwa na orodha ya majina 52 ya wagombea walioomba kupendekezwa katika nafasi hiyo ya juu. Kamati hiyo iliwahoji wanane kabla ya kupata wagombea wanne.

Kwa mujibu wa Kamati hiyo ‘
Wote wana uzoefu mkubwa katika kuendesha kesi za kimataifa.

Wasifu wa Wagombea

Jaji Othman ameshika nafasi muhimu mbalimbali za uandamizi katika mfumo wa sheria nchini Tanzania na alikuwa mwendesha mashtaka mkuu katika mahakama maalum ya mauaji ya Rwanda na pia mwendesha mashtaka katika Utawala wa Mpito wa Umoja wa Mataifa katika Timor Mashariki.

Kabla ya kujiunga na mahakama maalum ya Khmer Rouge , Bw Cayley alikuwa mwendesha mashataka mshauri mwandamizi wa ICC, Wakili wa Utetezi katika mahakama maalum za vita vya Sierra Leone na Yugoslavia na pia mwendehsa mashtaka katika mahakama ya Yugoslavia.

Petit alikuwa wakili mwandamizi katika kesi kwenye Mahakama ya Sierra Leone, afisa wa sheria katika mahakama maalum ya Rwanda na mshauri wa sheria kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kosovo.

Bensouda ni waziri wa zamani wa sheria nchini Gambia ambaye pia aliwahi kufanya kazi kama mshauri mwandamizi wa sheria na wakili katika kesi kwenye Mahakama maalum ya Rwanda.

"Ni orodha nzito kabisa," Alisema Param-Preet Singh, Mshauri Mwandamizi katika kitengo kinachoshughulikia Haki za Binadamu cha Human Rights Watch's International Justice Program.
Chanzo: BBC

Monday, October 24, 2011

Gaddafi dikteta mwenye mafanikio, wosia wake waanikwa

Best Blogger Tips
SIKU chache baada ya  kuuawa kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, walibya na dunia kwa ujumla imeingia katika mitizamo tofauti kuhusu kiongozi huyo huku wengi wakikumbuka mafanikio aliyoleta kwa taifa hilo tofauti na viongozi wengine waliong’olewa kwa udikteta.Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikimtangaza na kutafuta namna zote za kujenga picha ya udikteta bila kuangalia upande wa pili wa Libya iliyooachwa  na Gaddafi.

Baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakizungumziwa ni iwapo Libya ya sasa itaweza kuneemeka na kile ambacho ilikuwa ikipata kutoka kwa kiongozi huyo, ambaye  hivi karibuni  aliuawa na wapinzani wake.

Gaddafi, tofauti na viongozi wengine waliowahi kutajwa kuwa madikteta  duniani,  ana mengi ya kukumbukwa na kusifiwa kwayo.Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuongozi wamekuwa wakieleza kusikitishwa kwao na kutotambua aina ya demokrasia ambayo baadhi ya watu wa Libya wanaililia kwa sasa na iwapo itaboresha au kuharibu kabisa maisha yao.

Hii inawekwa wazi kwamba  pamoja na kwamba Gaddafi ametumia fedha nyingi za Libya katika masuala binafsi,  lakini je, kwa wastani Libya ni maskini? Wapo viongozi waliozitumia nchi zao na kuziharibu kabisa, Gaddafi aliwahi kuifilisi Libya?

Haya ni baadhi ya mambo ambayo Gaddafi  aliyasimamia na kuyatekeleza katika utawala wake wa miaka 42 kwa Libya.Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na tovuti za mawasiliano za Libya na Zimbabwe zimeeleza kuwa nchini Libya hakuna mwananchi aliyewahi kulipa bili ya umeme, umeme ulikuwa bure kwa raia wake wote.

Hakukuwa na riba katika mikopo, benki zote Libya zilikuwa chini ya Serikali,  mikopo ilitolewa kwa wananchi bila riba ya kiasi chochote .
Taarifa hizo zikafafanua kuwa makazi ni haki ya msingi nchini Libya, Gaddafi aliwahi kusisitiza kwamba wazazi wake hawawezi kupata makazi hadi kila raia apate makazi. Baba wa Gaddafi alifariki dunia wakati yeye, mama yake wakiwa wanaishi katika hema.

Wanandoa wote wapya nchini humo walipata Dola 50,000 kwa Serikali kwa ajili ya kununua makazi yao kuwasaidia kuanzisha familia mpya.Elimu na huduma za  kiafya vilitolewa bure. Wakati Gaddafi nachukua nchi  asilimia ya waliokuwa na elimu ilikuwa 25, kwa sasa inafikia  83.
Kwa waliotaka kuwa wakulima, walipewa ardhi bure, nyumba katika shamba lao, vifaa, mbegu na mifugo kwa ajili ya kuanzisha miradi.Iwapo kuna waliokuwa hawawezi kupata huduma za elimu na afya wanazostahili, Serikali iliwalipia kwa ajili ya kuzipata nje ya nchi, hizi hazikuwa bure, walitakiwa kuchangia, walipata Dola2,300 kwa mwezi kwa ajili ya makazi na usafiri.

Kwa waliokuwa wakitaka kununua magari,  Serikali ililipia kwa asilimia 50 ya bei. Bei ya petroli ilikuwa karibu na bure, lita ililipiwa kwa Dola 0.4.
Libya haidaiwi nje, pia ina akiba inayofikia Dola150 bilioni nje ambayo kwa sasa imezuiliwa.Kwa waliomaliza vyuo,  Serikali iliwapatia posho sawa na mshahara wa maofisa hadi watakapopata ajira yenye uhakika. Sehemu ya mauzo ya mafuta ya Libya iliwekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya raia wake.

Kila mwanamke aliyejifungua alipata posho ya Dola5000, mikate 40 iliuzwa kwa dola0.15,  asilimia 25 wa Walibya, wana shahada ya chuo kikuu.Kama hiyo haitoshi taarifa hizo zimeeleza kuwa alisimamia mradi mkubwa kabisa wa umwagiliaji, uliopewa jina la Great Man-made River, kuhakikisha maji yanakuwepo kwenye maeneo yote ya nchi yenye jangwa.

Wakati wa vikwazo kwa Serikali yake miaka ya 1980, Libya ilikuwa miongoni mwa nchi tajiri kabisa kwa msingi wa pato la ndani, ikwa na kiwango cha juu cha maisha kuliko Japan. Ilikuwa ni nchi tajiri kuliko zote kabla ya vuguvugu la mapinduzi.
Wastani wa kiwango cha maisha kwa pato la kichwa ni Dola11,314 . Gaddafi amewahi kutumia fedha nyingi kwa ajili ya safari zake na miradi yake, lakini amefanya mabo makubwa ambayo hakuna dikteta aliyewahi kuyafanya kwa watu wake. Alirejesha pato kwa watu wake, aliwajali.

          Wosia wa Gaddafi kabla ya kifo
Katika wosia wake, Kanali Gaddafi aliwaasa wafuasi wanaomuunga mkono kuendelea kupambana.
Alielezea msimamo wake kuwa amechagua kupambana hadi hatua ya mwisho na kufia katika ardhi ya Libya kuliko kuchagua njia nyepesi, ambayo kwa mtizamo wake,  ni kitendo cha kujidhalilisha kisichokuwa na heshima, kukimbilia uhamishoni nje ya nchi yake, ambapo tayari alishapata ahadi nyingi za ulinzi.

Katika lugha ya Kiingereza, waraka wake wa wosia umetafsiriwa ukisomeka: “Hii ni hiyari yangu. Mimi Muammar bin Mohammad bin Abdussalam bin Humayd bin Abu Manyar bin Humayd bin Nayil al Fuhsi Gaddafi, ninaapa kwamba hakuna Mungu mwingine zaidi ya Allah na Muhammad ni Mtume wake, amani iko kwake. Ninaahidi nitakufa nikiwa Muislamu.

 “Iwapo nitauawa, nitapenda kuzikwa kwa mujibu wa taratibu za kiislamu, nikiwa nimevaa mavazi nitakayokuwa nimevaa wakati kifo change kikitokea, bila mwili wangu kuoshwa, katika makaburi ya Sirte, jirani na familia na jamaa zangu.

“Nitapenda kwamba familia yangu, hasa wanawake na watoto, watunzwe vyema baada ya kifo changu. Watu wa Libya wana wajibu wa kulinda wasifu, mafanikio, historia na heshima ya waasisi na mashujaa wake.

“Watu wa Libya hawatakiwi kupuuza kujitapa na lazima wawe  watu huru wa kuthaminiwa. Ninawataka wale wanaoniunga mkono kuendelea kupambana, kuwakabili wote wanaosimama kutoka nje dhidi ya Libya, leo, kesho na siku zote.

 “Hata kama hatutashinda mapema, tutatoa funzo kwa vizazi vyetu vijavyo, kwamba kuchagua kulinda utaifa ni heshima na kuliuza ni uasi mkubwa ambao historia haitausahau milele, pamoja na juhudi za wengine kuwaeleza kinyume cha hayo”.
Endelea kusoma habari hii.....................

Thursday, October 20, 2011

Wasifu wa Kanali Muammar Gaddafi

Best Blogger Tips

Kanali Muammar Gaddafi
Alikuwa mtoto wa wafugaji wa Kibedui, mwenye maisha ya utata, lakini ambaye alitukuzwa sana, huku mataifa ya Magharibi yakimuona mtu wa hatari wakati wote.

Muammar Muhammad Gaddafi aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 40. Hadi mwanzoni mwa Machi 2011, alikuwa akiamini ndani ya moyo wake kwamba watu wake walikuwa wakimpenda na kwamba walikuwa tayari kumlinda hadi kufa kwa ajili yake.

Lakini wakati huo, tayari Gaddafi alikuwa ameshatumia njia za kikatili kuyazima maandamano dhidi yake, maandamano ambayo baadaye yaligeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mujibu wa taarifa, watu zaidi ya 30,000 waliuawa kwenye vita hivyo. Mara nyingi sana, Gaddafi alitoa matamko makali wakati wa vita hivyo, ila linalojuilikana zaidi ni lile la kuwaita wapinzani wake kuwa ni panya.

Kwa kila hali, yaliyotokea ni mambo ambayo Gaddafi hakuyatarajia asilani. Mtoto huyu wa wafugaji wa Kibedui aliyezaliwa mwaka 1942, alikuja kuibuka kama mkombozi wa Walibya, alipompindua Mfalme Idriss hapo mwaka 1969.

Kuanzia hapo akaanza kujenga kile alichokiona mwenyewe kuwa ni mfumo wa kidemokrasia wa moja kwa moja. Alianzisha kamati za umma zilizoamua juu ya mustakabali wa umma na wa Serikali. Aliuita mfumo wake wa kisiasa na kiuchumi kuwa ni wa kisoshalisti, alioufafanua kwenye kijitabu chake cha Kijani.

Historia yake kiufupi

Alizaliwa mwaka 1942 katika eneo la Jangwa, kwenye mji wa Sirte, katika familia ya baba Mohamed Abdulsalama Abuminiar na mama Aisha Ben Niran. Alijiunga na Jeshi la Libya  mwaka 1965.
Alifanya mapinduzi ya Serikali yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa mfalme Idris katika utawala wake mwaka 1969 na kuwa mtawala wa Libya akiwa na umri wa miaka 27.

Alikuwa maarufu kwa nguo anazopenda kuvaa na walinzi wa kike wenye kubeba silaha, kiongozi huyo wa Libya pia anadhaniwa kuwa na mbinu nzuri za kisiasa kwa kuweza kuirejesha Libya kutokana na kutengwa kidiplomasia duniani.
Baada ya miongo miwili ya kutengwa katika jamii ya kimataifa, mwaka 2003, Tripoli ilikiri kuwa walifanya shambulio la Lockerbie kwa kuiangamiza kwa mabomu ndege ya Pam Am. Umoja wa Mataifa (UN) ulikubali kuondoa vikwazo dhidi ya Libya.

Baada ya miezi kadhaa, Serikali ya Kanali Gaddafi ilisitisha mipango yake ya kuunda silaha za maangamizi na hii ikarejesha ushirikiano na nchi za Magharibi.

Gaddafi ni mtu wa kipekee katika kauli zake, mienendo yake, tabia zake na mikakati yake, kwa mujibu wa Saas Djebbar, mtaalam wa siasa za Libya.
Alipokuwa kijana alivutiwa na kiongozi mzalendo wa Misri, Gamal Abdel Nasser, alipokuwa akishiriki katika maandamano dhidi ya Israel wakati wa mtafaruku wa Suez mwaka 1956.

Alipanga njama ya kupindua utawala wa kifalme alipokuwa mwanafunzi wa kijeshi alipokuwa mafunzoni Uingereza kabla ya kurejea nyumbani Libya. Alipanga mapinduzi ya Septemba 1, 1969 akiwa katika mji wa Benghazi.

Alianza kujenga itikadi zake za kisiasa mwaka 1970 na kuziandika katika kitabu chake cha kijani kibichi.
Alikitumia kitabu chake kuanzisha mfumo wa kisiasa uliojumuisha kanuni za Kiislamu na mfumo ulio tofauti na siasa za ujamaa au ubepari.
Mwaka1977 aliasisi mfumo ujulikanao kama 'Jamahiriya' au 'Taifa la Umma' ambapo raia ndio wanaoendesha uongozi wa nchi yao kupitia 'kamati za umma'.

Mfumo huo wa Gaddafi umevuka mipaka na hauhusishi mambo ya siasa tu, bali pia mambo mengine.
Akiwa safarini ng'ambo, alikuwa akitumia makazi maalum kwenye kambi iliyojengwa na hema yake ya kifahari ya Kibeduwi akiwa amefuatana na walinzi wanawake ambao, inasemekana, huwa hawapotezi umakini kazini kama walinzi wanaume.Hema hiyo pia ilitumiwa kuwalaki wageni wa Libya na Kanali Gaddafi huendesha mikutano na mahojiano yake humo humo akipepea usinga au tawi la mitende.

Rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan alimwita Gaddafi 'mad dog' yaani 'mbwa kichaa' na Marekani ililipiza kisasi dhidi ya Libya kwa madai ya kuhusika na mashambulio ya anga barani Ulaya kwa kuvamia miji ya Tripoli na Benghazi mwaka 1986.Aliposhindwa katika jitihada zake za kuzipatanisha nchi za Uarabuni katika miaka ya 90, Kanali Gaddafi alielekeza nguvu zake barani Afrika na kupendekeza 'Muungano wa Nchi' za bara la Afrika.

Alianza kuvaa mavazi yake binafsi, sare za michezo zilizo na ngao za Bara la Afrika au picha za viongozi kutoka bara hilo.Aliwahi kuvunja na kufuta Wizara za nchi hiyo pamoja na bajeti zao, isipokuwa Wizara chache ikiwemo ya Ulinzi, Fedha na Mambo ya Nje.Licha ya uchumi wa Libya kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje, mabadiliko bado yanakwenda taratibu.

Vuguvugu la mageuzi dhidi yake lilipoanza mwanzoni mwa mwaka huu, aliapa kuwafuata wanaompinga nyumba hadi nyumba, mlango kwa mlango, hatua iliyoibua hasira na kuchochea harakati za kijeshi dhidi yake.

Baada ya baadhi ya askari kutangaza kujitoa katika jeshi lake na kuanzisha uasi, aliapa kwamba atapambana hadi tone la mwisho la damu litakapomwagika. Alisisitiza kwamba kamwe hatakimbia kutoka katika ardhi ya Libya, atafia katika ardhi ya mababu zake.

Taarifa zilieleza jana kwamba aliuawa baada ya kukutwa akiwa amejificha katika daraja dogo kwa ajili ya kupitisha maji barabarani (karavati).
Mara baada ya kuuawa, wapiganaji wa Baraza la Mpito waliokuwa katika mapambano dhidi yake walibaini kwamba alikuwa na bastola iliyotengenezwa kwa dhahabu tupu.

Muammar Gaddafi auawa

Best Blogger Tips
Muammar Gaddafi
KIONGOZI wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi  ameuawa. Habari zilizotangazwa na waasi wa majeshi ya serikali walitoa taarifa hiyo muda mfupi baada ya kutangaza kuushikilia mji wa Sirte, alikozaliwa Gaddafi.

Wapiganaji wa waasi walifanikiwa kupiga picha kwa kutumia simu na kusambaza kwa baadhi ya vyombo vya habari. Walidai kuwa  alionekana katika karavati akitambaa  kujaribu kujificha katika kati mwa mji wa Sirte. Hata hivyo walimpiga risasi mguuni.

Mpiganaji wa waasi, Mohammed al Bibi aliwaambia waandishi wa habari kuwa  baada ya kumwona Gaddafi alisikika akiwaambia askari hao: "Usipige risasi, usipige risasi," huku akiwa katika harakati za kujisalimisha. Kumekuwa na habari za utata kwamba  alifariki dunia baada ya maumivu makali ya majeraha miguuni, huku wengine wakisema  bado yu hai.

Waasi hao walidai kuwa alikutwa akiwa na bastola ya dhahabu  huku akiwa amevalia sare ya jeshi rangi ya  khaki. Ofisa mmoja wa  Baraza la Mpito la Taifa,  Abdel Majid  Mlegta alisema Gaddafi alipigwa pia kichwani.

Alisema alipigwa risasi alipokuwa akijaribu kukimbia  huku mpiganaji mwingine akidai kuwa alipigwa risasi tumboni. Gaddafi na familia yake walikuwa mafichoni tangu  Umoja wa Majeshi ya  Kujihami ya nchi za Magharibi, (NATO), na majeshi ya waasi  kuanza kuishambulia Tripoli  katika kati ya Agosti mwaka huu. Tukio hilo limetokea siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton  kufanya ziara nchini Libya na kusema kuwa ana imani Gaddafi atakamatwa au kuuawa.

WAASI WAMALIZA KAZI SIRTE

MAJESHI ya waasi  Libya yametangaza kumaliza kazi baada ya kufanikiwa kuuteka mji wote wa Sirte, nyumbani alikozaliwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Mummar Gaddafi. Askari hao walisema walifanya mashambulio ya nguvu yaliyodumu kwa muda wa dakika 90 jana asubuhi.

Hata hivyo baadhi ya askari wanaomtii Gaddafi bado wapo katika mji wa Bani Walid, kusini mashariki mwa Tripoli. "Hii ni siku ya mwisho ya mapigano," alisema Luteni Kanali Hussein Abdel Salam wa kikosi cha Misrata. Alisema  katika awamu ya mwisho ya mapambano, waliweza kuwaona askari wa Gaddafi wakiwa wamejificha ndani ya nyumba kadhaa wakiwa na bunduki na silaha nyingine za kivita.

Serikali mpya ya Baraza la Mpito lilisema kuwa litatangaza Libya kuanguka baada ya kuuchukua mji wa Sirte. Wakati huo huo, Uingereza imeitaka Algeria kutoa ushirikiano dhidi ya Libya kuhusu familia ya Gaddafi ambayo imeomba hifadhi nchini humo. Waziri wa Mambo ya Nje wa  Uingereza, William Hague alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara nchini humo.

Mtoto wa kike wa Gaddafi, Aisha, kaka yake Hannibal na mama yao  Safiya  wamehifadhiwa  nchini Algeria. Katika mkutano huo wa pamoja  na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria Mourad Medelci,  Hague alisema  Agleria haipaswi kusita iwapo hata mahakama ya uhalifu wa Kimataifa ukiomba lolote ni lazima isikilizwe.

Alisema ni vema Agleria ikafanya kazi kwa karibu na serikali ya mpito ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza baadaye.

Hata hivyo kwa upande wake, Medelci alisema watu hao wamepewa hifadhi kwa sababu za kibinadamu  na hata serikali ya mpito ya Libya inatambua hilo.

Wednesday, October 19, 2011

Hotuba ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kwa Waandishi wa habari Monduli, Octoba 19, 2011

Best Blogger Tips

NDUGU wana habari nimewaita katika mkutano huu leo kwa sababu moja kubwa, kutoa ufafanuzi kuhusu matukio ambayo yamekuwa yakitokea huku yakinihusisha mimi binafsi kwa namna ambayo sasa yanatishia ustawi na mshikamano wa kimaadili, kihistoria na kikazi miongoni mwa viongozi na baina ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Ndugu wana habari, naamini mmekuwa mkifuatilia kwa karibu habari zinazoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari zinazolihusisha jina langu na harakati kadha wa kadha chafu ambazo hata mimi mwenyewe ninayehusishwa nazo huwa nazisikia na kuzijua baada ya kuwa zimesharipotiwa katika vyombo hivyo vya habari," alisema.

Alisisitiza kwamba uamuzi wake wa kukutana wanahabari haukuwa na nia ya kuzozana na vyombo vya habari wala kwenda kinyume cha utamaduni wa kimaadili wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaotaka viongozi kujadili masuala yanayokihusu chama chao ndani ya vikao rasmi vya kimaamuzi, bali kutoa ufafanuzi na angalizo kwa pande zote hizo mbili ambazo zinaguswa na matukio yanayoendelea kutokea.

Moja ya mambo ambayo yameligusa jina langu kwa namna hiyo ni lile linalonihusisha eti na kundi moja la wanasiasa ambao wamekuwa na mikakati ya kumhujumu mwenyekiti wetu wa chama, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete. Hakuna shaka ni madai ya kipuuzi, kizushi na yenye malengo machafu.
Hawakuishia hapo sasa wamefikia hatua ya kuvitumia vyombo hivyo hivyo vya habari na kufikia hatua ya kudai kwamba nimeanza kuandaa orodha ya kile wanachokiita madhambi ya Rais Kikwete ambayo wanadai nimepanga kuyasoma wakati wa kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (CCM).

Ninaamini kwa dhati kabisa kwamba, waandishi wa habari wanaofuatilia kwa karibu na kwa umakini mwenendo wa masuala ya kisiasa nchini wanatambua kwamba, watu wanaopenyeza taarifa hizi katika vyombo vya habari wanafanya hivyo kwa malengo ya kufikirika ya kujisafishia njia kisiasa.

Ni jambo lisiloingia akilini kunihusisha na kile kinachoitwa mikakati ya kumhujumu rais au chama ambacho mimi ni kada wake wa muda mrefu, mbunge anayetokana na chama hicho hicho na mtu ninayeiongoza Kamati nyeti ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na zaidi ya yote kiongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa na kiserikali nilizowahi kushikilia.

Kuhusu hili napenda kusema kwa uwazi kwamba, mbali ya ukweli kuwa sijapata kufikiria hata mara moja kuhusu hicho wanachokiiita mabaya au madhambi ya rais, sina na wala siijui hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete.

Saturday, October 15, 2011

Man United yalazimisha sare na Liverpool

Best Blogger Tips
Steven Gerrard akishangilia bao na wenzake
Javier Hernandez aliisawazishia Manchester United zikiwa zimesalia dakika tisa kabla mchezo haujamalizika na kuisaidia timu yake kuambulia angalao pointi moja katika pambano kali dhidi ya Liverpool.

Mshambuliaji huyo anayechezea pia timu ya taifa ya Mexico, aliingizwa mchezaji wa akiba kipindi cha pili, alitumia akili ya haraka baada ya mpira uliochongwa na Danny Welbeck na kufanikiwa kuisawazishia kwa kichwa timu yake ya Manchester United na kuinyima ushindi Liverpool kutokana na bao lililofungwa awali na Steven Gerrard.

Nahodha huyo wa Liverpool alifunga bao katika dakika ya 68 kwa aina ya mikwaju anayofunga sana ya adhabu ndogo na mpira ukaingia langoni na kumuacha mlinda mlango wa Manchester United David De Gea asijue la kufanya.

Jordan Henderson alikosa nafasi nzuri mbili za kuipatia ushindi Liverpool katika dakika za nyongeza kabla mpira haujamalizika, lakini walinzi wa Manchester United walikaa imara na kuokoa hatari zote na hasa mlinda mlango David De Gea.

Kwa matokeo hayo Liverpool wamefikisha pointi 14 wakijikita nafasi ya tano ya msimamo wa ligi ya soka ya England.
Chanzo: BBC

Friday, October 14, 2011

Watanzania tunamkumbuka Mwalimu Nyerere

Best Blogger Tips


Matatizo kwa wateja wa Blackberry

Best Blogger Tips
Simu ya Blackberry
Mwanzilishi wa kampuni ya Blackberry Mike Lazaridis amesema huduma zake zitarejea kama kawaida baada ya kukumbwa na matatizo makubwa kwa kipindi cha siku tatu duniani kote.

Mamillioni ya wateja duniani kote walikuta mawasiliano yao ya ujumbe mfupi na barua pepe yakikatizwa nawengi wao walielezea hasira zao kupitia mtandao wa Twitter.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video kwenye tovuti ya kampuni hiyo, Bw Lazaridis hakutangaza tarehe yoyote kuhusu ni lini huduma kamili zitarudishwa.

Pia alionya kwamba huenda kukazuka matatizo zaidi baadae.

"Hivi sasa tunafikia viwango vya kawaida katika Ulaya, Mashariki ya Kati, India na Afrika" alisema ,ingawa huenda kukazuka "matatizo" wakati kampuni inaendelea kutanzua malimbikizo ya ujumbe mfupi na barua pepe.

Wakuu wa shirika la RIM ambalo ndilo linalomiliki Blackberry limekua likijibu kwa haraka zaidi manun'guniko ya wateja baada ya malalamiko kwamba hawakuwa na mawasiliano mazuri baada ya kujitokeza kwa matatizo haya.

"Tunajua tumewavunja moyo wateja wetu wengi. Mulitraji mengi kutoka kwetu.Nataraji mengi kutoka kwetu "alisema.

Wateja walianza kuarifu kupoteza huduma kuanzia Octoba 10 na matatizo yakaanza kusambaa duniani kote.

Kampuni ya Blackberry ina hamu kubwa kutaka ionekane inalitatua tatizo hili kwa haraka baada ya matatizo ya mapema wiki hii ambapo ilisema huduma zilirejea kama kawaida kauli iliyopingwa vikali na wateja walioghadhibika.
Chanzo: BBC

Wednesday, October 12, 2011

Mwinyi-Viongozi wa dini mnanuka

Best Blogger Tips
RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi, amesema viongozi wa dini kutoka Tanzania wanatia aibu na kuchangia Watanzania kunuka nje ya nchi kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.

Mzee Mwinyi alitoa kauli hiyo jana mbele ya viongozi hao na kusimulia mkasa uliomkuta yeye binafsi wa kupekuliwa kupita kiasi katika kiwanja cha ndege nje ya nchi, akishukiwa kuwa kiongozi wa dini kutoka Tanzania anayesafirisha dawa za kulevya.

Alikuwa akizindua Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Athari za Dawa za Kulevya jana Dar es Salaam katika hafla iliyoandaliwa na asasi ya kiraia ya American International Health Alliance (AIHA).

“Ninachokisema kuna maneno mengi ya aibu yanasemwa kuhusu Watanzania, aibu zaidi hata kwa wacha Mungu wa Tanzania sasa hawaaminiki, wanatumia fursa walizonazo kuficha na kusafirisha dawa za kulevya.

“Nilikuwa naenda Ujerumani hivyo nililazimika kubadili ndege katika moja ya nchi huko ughaibuni, wakati wa kupanda ndege ya pili tukaanza kukaguliwa. Ilipofika zamu yangu, nilikaguliwa sana, lakini hawakutosheka, nikaingizwa kwenye chumba cha pembeni, nikavuliwa viatu na koti wakanikagua kwa mashine na mwisho wakanipapasa mwili mzima,” alisema Mzee Mwinyi.

Alisema alikumbana na kadhia hiyo pamoja na hadhi yake ya kidiplomasia kwa vile tu alikuwa ameshikilia tasbihi (rozari) mkononi, jambo lililofanya ahisiwe kuwa ni kiongozi wa dini anayesafirisha dawa za kulevya.

“Yule aliyenikagua alikuwa akifanya kazi yake, amenifundisha, lakini nataka mjue Watanzania wenzangu kuwa tunanuka huko nje,” alisema Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa wakati wa utawala wake.

Mzee Mwinyi alilazimika kutoa mkasa huo uliompata miaka mingi iliyopita bila kutaja mwaka wala uwanja husika mbele ya viongozi hao wa dini mbalimbali ili kufikisha ujumbe kwao kuwa Tanzania inanuka kwa kuhusishwa na dawa za kulevya.

Alisema mmoja wa wasaidizi wake alijaribu kumnusuru katika hali hiyo kwa kumtahadharisha ofisa wa uwanja huo wa ndege kuwa huyo anayemkagua ni mwanadiplomasia.

“Lakini bwana yule alimjibu tena kwa ukali ‘I don’t care’ (sijali), wakaendelea kunikagua wanavyotaka baadaye nikajiuliza kwani imekuaje wakanikagua vile, nikagundua kuwa ni kwa vile nimebeba tasbihi,” alisimulia Mzee Mwinyi.

Alisema alionekana kama mwanadini anayetumia alama ya tasbihi ili apitishe dawa za kulevya kirahisi, jambo ambalo lilimsikitisha na wakati anaondoka uwanjani hapo, alilazimika kumkabidhi yule ofisa aliyemkagua tasbihi yake kama zawadi.

Kauli hiyo ya Mzee Mwinyi, imetolewa baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka viongozi wa dini kukemea uhalifu huo na kutahadharisha kuwa sasa biashara hiyo imeaanza kuvutia viongozi wa dini.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwahutubia waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, kwenye ibada maalumu ya kupewa kuwekwa wakfu Mhashamu Askofu John Ndimbo wa Jimbo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha kunakuwa na sheria moja yenye nguvu itakayoziba mianya yote inayojitokeza katika sheria za dawa za kulevya.

Alisema kwa sasa sheria zilizopo zina mianya mikubwa ambayo inasababisha mapapa wa biashara hiyo na vipapa vidogo vinavyokamatwa kuishia kulipishwa faini ya Sh. milioni moja na kutoka.

“Sheria inasema wazi ukikamatwa na dawa za kulevya unalipishwa mara tatu ya gharama ya mzigo wa dawa hizo, kifungo cha miaka 30 au maisha lakini hivi kweli mmeshawaona watu wakifungwa kwa kosa hilo, lazima kuwe na marekebisho katika sheria hizi,” alisema

Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo, alisema kikosi kazi maalumu kilichopo chini ya Tume hiyo kimekamata watu wengi wanaotuhumiwa kufanya biashara hiyo.

Takwimu zinaonesha mwaka 2008 hadi mwaka huu, watuhumiwa 22,814 walikamatwa nchini na 67 nje ya nchi huku idadi ya dawa zilizokamatwa ikiongezeka.

Kwa mujibu wa Shekiondo, dawa zilizokamatwa zimeongezeka kutoka heroine kilo 100 kutoka mwaka 2000 hadi 2009 hadi kilo 154 mwaka jana na mwaka huu; na cocaine kilo 57 mwaka 2000 hadi 2009 hadi kufikia kilo 191 mwaka 2010 hadi mwaka huu.

Baraza hilo la Viongozi wa Dini kazi yake ni kuhamasisha vijana kuepuka biashara na matumizi ya dawa za kulevya na linaongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum.
Chanzo: HabariLeo

Monday, October 10, 2011

Mwakyembe apelekwa India

Best Blogger Tips
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe amepelekwa katika Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu baada ya hali ya afya yake kuwa tete kwa kuugua ugonjwa unaomsababishia kuvimba mwili wake.

Akizungumza na gazeti hili, Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), alikiri kuwa Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, anasumbuliwa na maradhi hayo na amesafirishwa jana kwenda India kwa matibabu zaidi.

“Ni kweli Mheshimiwa Waziri ameondoka leo (jana) mchana na ndege ya Qatar Airline kwenda India kwa matibabu zaidi,” alisema Mwambalaswa ambaye kama Dk. Mwakyembe anatoka mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa Mwambalaswa, hali ya Dk. Mwakyembe si mbaya sana kwa kuwa anaweza kula na kutembea vizuri ingawa bado amevimba baadhi ya sehemu mwilini.

Dk. Mwakyembe anadaiwa kusumbuliwa na ugonjwa wa ngozi unaojulikana kitaalamu kama Exfoliative Dermatitis na alianza kusumbuliwa na ugonjwa huo zaidi ya miezi mitatu iliyopita, lakini kwa sasa hali ya ugonjwa huo imezidi kuwa mbaya.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda alisema hana taarifa za kuugua kwa Dk. Mwakyembe kwa kuwa alikuwa safarini, lakini aliahidi kuzungumzia suala hilo baada ya kupata ripoti zaidi.

Mwakyembe alizungumza juzi na gazeti moja la kila siku na kukiri kuwa anaumwa na kwamba hata sura yake imebadilika huku akikanusha madai ya kulishwa sumu.

Ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe unadaiwa huathiri wanaume na wanawake wenye umri kuanzia miaka 55 na dalili zake ni kuwashwa, mwili kuishiwa nguvu na sehemu ya juu ya ngozi kupukutika.

Chanzo cha ugonjwa huo hakijajulikana, lakini kinahusishwa na magonjwa ya ngozi na madhara ya matumizi ya dawa mbalimbali. Hospitali ya Apollo aliyopelekwa Dk. Mwakyembe, ndiko alikolazwa Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya kwa muda mrefu sasa, baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo, ambaye kwa sasa hali yake imeelezwa kuendelea vizuri.

Juzi, Rais Jakaya Kikwete alikwenda kumjulia hali Dk. Mwakyembe nyumbani kwake Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Chanzo: HabariLeo

Pires wa Cape Verde ashinda Mo Ibrahim

Best Blogger Tips
Bw Pedro Veroan Pires wa Cape Verde
Aliyekuwa rais wa Cape Verde Pedro Verona Pires ametunukiwa dola za kimarekani milioni tano inayotolewa na wakfu wa Mo Ibrahim kwa ajili ya utawala bora barani Afrika.

Kamati inayoshughulikia zawadi hiyo ilisema Bw Pires, aliyeachia madaraka mwezi Agosti, amesaidia kuifanya nchi hiyo kuwa " yenye demokrasia, utulivu na kustawi zaidi".

Tuzo hiyo intakaiwa kutolewa kila mwaka kwa kiongozi anayechaguliwa kidemokrasia na kuondoka madarakani kwa hiari.

Hapajakuwa na mshindi kwa miaka miwili iliyopita.

Kamati hiyo ilisema hakukuwa na mgombea anayestahili.

Tuzo hiyo ya dola za kimarekani milioni tano, inayotolewa kwa zaidi ya miaka 10, ni zawadi yenye thamani kubwa duniani inayotolewa kwa mtu binafsi.

Washindi wa awali ni aliyekuwa rais wa Botswana Festus Mogae na wa Msumbiji Joaquim Chissano.
Chanzo: BBC

Sunday, October 9, 2011

Dk Mwakyembe mgonjwa

Best Blogger Tips
Rais Kikwete alipomtembelea Dr Mwakyembe
AFYA ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, ni tete baada ya kuugua ugonjwa uliomsababisha kuvimba mwili wote.Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na yeye mwenyewe zinaeleza kuwa, alianza kuwashwa ngozi miezi mitatu iliyopita kabla ya hali kubadilika siku za karibuni na hatimaye kuvimba sehemu kubwa ya mwili wake.

Mwakyembe alilieleza gazeti hili jana kuwa, baada ya  hali yake kubadilika alianza kupata matibabu katika hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam akiwa nyumbani kwake Kunduchi Beach.Akizungumza na gazeti hili kwa shida, Dk Mwakyembe alisema hajui chanzo cha ugonjwa huo wa ngozi, daktari wake ndiye anaweza kuelezea kwa usahihi.

“Ni kweli naumwa nipo nyumbani, hata sura yangu imebadilika. Sasa hivi namsubiri daktari wangu, nilisikia natakiwa kupelekwa India kwa matibabu, nasubiri kauli yake si mimi niamue,” alisema na kuongeza;
“Siwezi kusema nimelishwa sumu, ninachosema mimi nimevimba kweli mwili mzima naumwa kweli hapa nimelala na sijui umenipataje kwa simu kwa sababu huwa siiwashi muda huu una bahati kweli”.

Mke wa Dk Mwakyembe  Mkewe Linah Mwakyembe alipozungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Jumapili, alisema kwa mujibu wa daktari wake, Dk mumewe  anasumbuliwa na ugonjwa wa ngozi unaojulikana kitaalamu kama Exfoliative Dermatitis.
 “Alianza kuugua muda mrefu kidogo, kama miezi mitatu iliyopita, hali hiyo ilikuwa inatokea na kupotea hadi sasa ambapo hali imekuwa mbaya zaidi,” alisema.

Alisema madaktari waliomfanyia uchunguzi kwa nyakati tofauti katika kipindi hicho walitoa majibu tofauti na kuongeza kuwa wapo waliosema hali hiyo ilisababishwa na kisukari na mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kulikuwa na chembechembe za sumu katika damu yake.

“Baada ya ngozi yake kubadilika sana na hali kuwa mbaya, tulienda hospitali na madaktari walitupa majibu tofauti, wapo waliosema ni kisukari na kuna mwingine alisema kuna chembechembe za sumu,” alisema Linah na kufafanua  kuwa daktari aliyedai hivyo hakuwapa maelezo zaidi.
Kwa mujibu wa Linah, ngozi ya Dk Mwakyembe inawasha na inakuwa kama inatoa mba mwili mzima hadi kichwani.

Aliongeza kuwa daktari wake ameshauri ufanyike uchunguzi wa kina zaidi ili kujua kama atahitajika kupatiwa matibabu nje ya nchi.
“Walipendekeza afanyiwe uchunguzi zaidi, hivyo kama kutakuwa na ulazima wa kupatiwa matibabu zaidi nje ya nchi basi watatueleza,” alisema Linah.
Alisema kuwa leo ndio watapata  jibu kama atahitajika kwenda nje au kuendelea  na matibabu hapa nchini.

Alisema kumekuwa na uvumi mwingi juu ya ugonjwa wa Dk Mwakyembe na kusisitiza kuwa wao kama familia wanasikiliza kinachosemwa na madaktari na kile watakachoshauri.
“Sisi tunaendelea kusubiri kile kitakachogundulika baada ya uchunguzi huo na kama kutakuwa na mengine tutajulishwa na kujua hatua itakayofuata,” alisema Linah.

Exfoliative Dermatitis Kwa mujibu wa maelezo ya kitabibu, ugonjwa huu huweza kusababisha madhara makubwa ya mwili na matatizo mengine hivyo kuhitaji uangalizi wa karibu wa kitabibu.
Ugonjwa huu ukikomaa husababisha ngozi ‘kuwaka moto’ na huathiri wanawake na wanaume  lakini zaidi wanaume wenye umri kuanzia miaka 55.
Dalili  Dalili za ugonjwa huu ni kuwashwa, mwili kuishiwa nguvu pia sehemu ya juu ya ngozi hupukutika.

Chanzo  kwa mujibu wa maelezo ya kitabibu, sababu za ugonjwa huo bado hajizulikani, hata hivyo matukio ya ugonjwa huu mara nyingi yanahusishwa na magonjwa mbalimbali ya ngozi, madhara ya dawa kama penicillin, sulfonamides, isoniazid na phenytion.

Rais Kikwete amtembelea Baadaye mchana Rais Jakaya Kikwete alifika nyumbani kwa Dk Mwakyembe Kunduchi Beach kumjulia hali.
Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela mwaka 2008, aliongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Mkataba wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond.

Katika baraza jipya la mawaziri ambalo Rais Kikwete aliliunda mwaka jana, alimteua Dk Mwakyembe kuwa Naibu waziri wa Ujenzi akimsaidia Dk John Magufuli.

Mikasa ya Mwakyembe

Mei 21 mwaka 2009  Dk Mwakyembe alinusurika kufa katika  ajali mbaya ya gari eneo la Ihemi kilomita 40 kutoka Iringa mjini akiwa safari kutokea Mbeya kwenda Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za Polisi, gari alilokuwa akisafiria Toyota Landcruiser T362ACH,   liliacha njia  saa moja asubuhi baada ya kukanyaga shimo na tairi ya upande wa kulia kuchomoka na dereva wake, Joseph Msuya (30), kupoteza mwelekeo kabla ya gari hilo kutoka nje ya barabara upande wa kushoto na kuparamia mti kisha kupinduka.

Ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa Dk Mwakyembe akijaribu kulipita lori kabla ya kukanyaga shimo hilo.

Dk Mwakyembe na abiria wengine waliokolewa na Wasamaria wema pamoja na trafiki wawili  waliokuwa kwenye basi dogo wakisafiri kutoka Iringa kwenda Njombe.

Baada ya ajali hiyo alilazwa  katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa. Ilifahamika kuwa aliumia taya kisha alihamishiwa Dar es Salaam kwa matibabu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)  aliunda tume iliyoongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakati huo, Kamanda James Kombe,  kuchunguza chanzo cha ajali hiyo. Matokeo yalionesha kwamba ilisababishwa na uzembe wa dereva wake, Msuya.
Chanzo: Mwananchi

Saturday, October 8, 2011

Wabrazil waahidi kuitoa nchi gizani

Best Blogger Tips
MATUMAINI ya Watanzania kuwa na umeme wa uhakika, yameanza kuonesha nuru, baada ya Ijumaa, kampuni ya Odebreicht ya hapa kukubali kuwekeza katika umeme wa maji kwenye maporomoko ya maji ya Stiglers Gorge yaliyopo ndani ya Bonde la mto Rufiji, umbali wa kilomita 374 kutoka jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ilifikiwa Ijumaa katika mazungumzo kati ya wawakilishi wa kampuni hiyo kubwa ya uwekezaji katika sekta hiyo duniani kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo jijini hapa, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema mradi huo utakaoanzishwa katika Bonde la Rufiji, ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2,100.

Mahitaji ya nchi hayazidi megawati 1,000 ingawa kwa sasa umeme unaozalishwa kutoka
mitambo ya vyanzo vya maji na mafuta unafikia megawati 500, hivyo kufanya upungufu wa kati ya megawati 300 na 500 ambazo zikipatikana zitaiondoa kabisa nchi gizani.

Hivyo, kupatikana kwa umeme wa Brazil kutakuwa kumeandika historia mpya, kwani tatizo la umeme linaweza lisionekane kwa miaka mingi ijayo.

Alisema kampuni hiyo ilisema imeridhishwa na mradi huo baada ya kutembelea Tanzania
Agosti 17, mwaka huu na kuthibitisha kuwa mradi huo unawezekana.

"Hawa watu wana uwezo mkubwa, kwani huu hautakuwa mradi wao wa kwanza, walishakuwa na mradi kama huo nchini mwao hapa ambao unazalisha megawati 3,150...tunaamini watafanya vizuri," alisema Ngeleja.

Alisema mradi huo ambao umekuwa ukipigiwa kelele muda mrefu na wananchi, ukikamilika utaiwezesha Tanzania kujitosheleza kwa nishati hiyo na kuuza mwingine nje ya nchi na kuipatia nchi fedha za kigeni.

Aliongeza kuwa mbali na kuuza nje, lakini pia utakuwa wa bei nafuu kwa wananchi. Hata hivyo Ngeleja alisema Serikali haitakaa na kubweteka ila itaendelea kutafuta vyanzo zaidi vya umeme ili kuhakikisha kuwa tatizo linalojitokeza hivi sasa la umeme halijirudii.

Aliongeza kuwa licha ya hivyo bado Tanzania haitategemea vyanzo vya umeme wa maji pekee bali itaendelea kutafuta vingine jinsi itakavyowezekana.

Kabla ya kujitokeza kwa mwekezaji huyo wa Kibrazil, serikali ilikuwa katika juhudi za kuendeleza mradi wa Stigler’s Gorge tangu miaka ya 1970, kwa kufanya upembuzi yakinifu kwa msaada wa serikali ya Norway, lakini hakuna uendelezaji wowote uliokuwa umefanyika katika mradi huo wa kufua umeme.

Kuhusu mafuta, alisema Kampuni ya Petrobras ya hapa ambayo ilitoa meli kubwa ya
kutafuta mafuta Tanzania inaendelea na juhudi zake katika mwambao wa Bahari ya Hindi
na mpaka sasa haijapata mafuta wala gesi lakini matarajio ni makubwa.

Alisema Petrobras ambayo pia ni kampuni kubwa ya mafuta nchini hapa inatarajia kutoa taarifa ya awali ifikapo Desemba.

Kuhusu juhudi za Serikali kutafuta wabia wa miradi hii, Ngeleja alisema Serikali inafanya hivyo kwa kuwa haina fedha za kutosha yenyewe kuiendeleza na ndiyo sababu inashirikisha sekta binafsi.
Chanzo: HabariLeo

Friday, October 7, 2011

Wanawake watatu washinda tuzo ya Nobel

Best Blogger Tips
Bi Tawakul Karman, Rais Ellen Johnson Sirleaf na Bi Leymah Gbowee
Tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka huu imewatunuku kwa pamoja wanawake watatu- Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, Leymah Gbowee wa Liberia na Tawakul Karman wa Yemen. 

Wametambulika kutokana na "harakati zao bila kutumia vurugu kwa usalama wa wanawake na haki za wanawake katika kushiriki kikamilifu kwenye kujenga amani".

Bi Sirleaf ni rais wa kwanza mwanamke barani Afrika, Bi Gbowee mwanaharakati wa amani Liberia na Bi Karman kiongozi wa harakati za kidemokrasia Yemen.

Tuzo hiyo ikitangazwa Oslo, mwenyekiti wa kamati ya Nobel Thorbjorn Jagland alisema: " Hatuwezi kufanikiwa kupata demokrasia na amani ya kudumu katika dunia hii mpaka wanawake wafanikiwe kupata fursa sawa na wanaume ili kuweza kuchochea maendeleo katika viwango vyote vya jamii."

Taarifa hiyo ilisema "ni matumaini ya kamati ya Nobel ya Norway kuwa tuzo hiyo itasaidia kumaliza ukandamizaji wa wanawake ambao bado unaendelea katika nchi nyingi, na kutambua uwezo mkubwa wa demokrasia na amani ambao wanawake wanaweza kuwakilisha."

'Mwanamke Ngangari'

Bi Karman anaongoza shirika la Yemen la Women Journalists without Chains, yaani waandishi wa habari wa kike wasio na mipaka na amefungwa jela mara nyingi kutokana na kampeni zake za kutaka uhuru wa habari na upinzani wake kwa rais wa serikali ya Ali Abdullah Saleh.

Alitambuliwa kwa kuchukua nafasi kubwa kwenye harakati za haki za wanawake katika machafuko ya kuunga mkono demokrasia huko Yemen "katika hali ngumu sana".

Bi Karman, mama mwenye watoto watatu, ameiambia idhaa ya Kiarabu ya BBC kuwa anatunukia tuzo yake kwa "wote waliojitoa mhanga na kujeruhiwa na machafuko ya nchi za kiarabu"- wimbi la ghasia lililoenea Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kwa " watu wote wanaopigania haki zao na uhuru wao".

Ni mwanamke wa kwanza wa kiarabu kushinda tuzo ya amani ya Nobel.
Bw Jagland amesema ukandamizwaji wa wanawake ndilo "jambo muhimu sana" katika dunia ya kiarabu na kumtunukia Bi Karman ni "kutoa ishara kwamba kama itafanikiwa katika jitihada za kuleta demokrasia, lazima iwahusishe wanawake".

Bi Sirleaf, mwenye umri wa miaka 72, ambaye tetesi kwa kiasi kikubwa zilikuwa zikimwelekeza yeye, alisema tuzo hiyo ni " kwa Waliberia wote" na kutambuliwa kwa " miaka mingi ya harakati za kupata haki".

Alichaguliwa mwaka 2005, kufuatia kumalizika kwa miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 250,000, na kusababisha wengi kukimbilia nchi za nje na kuvuruga uchumi wa nchi hiyo.

Alipoingia madarakani, mchumi aliyepata elimu yake Marekani na aliyekuwa waziri wa fedha- anayejulikana kama "mwanamke Ngagari" wa Liberia aliahidi kupambana na rushwa na kuleta "hisia za kimama kwenye urais" kama njia ya kuponyesha majeraha yaliyotokana na vita.

Ni maarufu sana miongoni mwa wanawake na wasomi wachache nchini humo, lakini anachukiwa na jamii za kimila zinazoongozwa zaidi na wanaume.

Bi Sirleaf anagombea tena urais wiki ijayo, licha ya kusema kuwa atashikilia nafasi hiyo ya urais kwa mhula mmoja tu.

Bi Gbowee alikuwa kinara wa kupinga vurugu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe Liberia, akiwashawishi wanawake wa makabila na dini zote katika harakati za amani- wakati fulani hata "kugoma kufanya ngono"- na kuwahimiza kushiriki kwenye uchaguzi.

Taarifa kuhusu tuzo hiyo ilisema, " Tangu wakati huo amaefanya kazi ya kuwashawishi wanawake Afrika Magharibi wakati na baada ya vita."

Wanawake hao watagawana zawadi yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 1.5.
Chanzo: BBC

Thursday, October 6, 2011

Steve Jobs wa Apple afariki dunia

Best Blogger Tips
Steve Jobs
Steve Jobs, mwanzilishi msaidizi na aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni kubwa ya kimarekani ya Apple, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 56. 

Apple imesema "uhodari wake, hisia zake na uwezo wake ulikuwa chanzo cha ubunifu usiohesabika uliostawisha na kuimarisha maisha yetu sote.

Joba alitangaza kuugua saratani ya kongosho mwaka 2004.

Rais wa Marekani Barack Obama alisema kutokana na kifo chake, dunia "imempoteza mtu mwenye upeo"
Bw Obama alisema, " Steve alikuwa miongoni mwa wabunifu muhimu Marekani- mwenye ujasiri wa kutosha wa kufikiri tofauti, shujaa wa kutosha wa kuamini anaweza kubadili dunia, na mwenye kipaji cha kutosha cha kuweza kufanya hivyo.

Taarifa kutoka kwenye familia ya Bw Job imesema walikuwa naye alipofariki dunia kwa amani siku ya Jumatano.

"Katika maisha yake ya kikazi, Steve alijulikana mwenye upeo; katika maisha yake ya binafsi, aliipenda familia yake," walisema, wakiomba faragha na kuwashukuru wale "waliomwombea" katika mwaka wake wa mwisho.

Tim Cook, aliyerithi nafasi yake katika kampuni ya Apple baada ya Bw Job kuachia madaraka mwezi Agosti, amesema aliyemtangulia aliacha "kampuni ambayo yeye pekee ndiye angeweza kuijenga, na nafsi yake maisha itakuwa msingi wa Apple".

Bendera zimeshushwa nusu mlingoti nje ya makao makuu ya Apple huko Cupertino, California, huku mashabiki wa kampuni hiyo wakiacha rambirambi nje ya maduka ya Apple duniani kote.

Cory Moll, mfanyakazi wa Apple wa San Fransisco alisema, "Alichotufanyia ni kama utamaduni, inauma kwa namna ya kipekee kwa kila mtu".
Chanzo: BBC

Sunday, October 2, 2011

Shoga 'Anti Suzy' afichua siri nzito

Best Blogger Tips
SHOGA maarufu jijini Dar es Salaam, Ibrahim Mohamed ‘Anti Suzy’ (25) ameibuka na kutoa siri nzito kuhusu mambo yanayofanywa na mashoga kwa kushirikiana na baadhi ya vigogo
nchini kuwaharibu watoto wadogo wa kiume.

Ametoa tahadhari huku akidai kuwa kama Serikali kwa kushirikiana na watu wengine
haitachukua hatua, kizazi cha kiume cha Watanzania siku zijazo kitapotea katika dunia hii kutokana na ukweli kwamba wimbi la uwepo wa mashoga linazidi kuongezeka kwa kasi.

Anti Suzy ambaye ni mkazi wa Jangwani, pia amejitangaza kuwa ni muathirika anayeishi na Virusi vya Ukimwi kwa zaidi ya miaka 10 sasa na akasema mashoga wengi wameshaambukizwa virusi vya Ukimwi kama yeye na wanaishi kwa matumaini, hivyo kwa kuwa nao ni binadamu, wasingependa kuona watoto wadogo wa kiume wakiharibiwa kama walivyofanyiwa wao.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi katika ofisi za gazeti hili zilizopo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Anti Suzy alisema hivi sasa wanaume wenye fedha akiwataja kwa jina maarufu la ‘mapedejee’ wanatumia fedha zao kuharibu watoto wadogo huku wengi wao wakijijua kuwa ni waathirika wa Ukimwi.

“Najua kuwa na Ukimwi si mwisho wa maisha lakini si vizuri mtu ukijijua kuwa umeathirika,
ukamwambukiza mwenzako kwa makusudi, kwa kweli sasa hivi hali ni mbaya, wanaume wenye pesa ‘mapedejee’ wanapenda sana watoto wadogo wa kiume,” alisema na kuongeza:

“Wazazi wawe macho sana, sasa hivi mashoga wa rika langu ukienda ukumbi wa starehe au baa, wakijua wewe ni shoga, anakutafuta mtu anakuomba simu ili umtafutie mtoto
mdogo kwa gharama yoyote.

“Mashoga watu wazima hivi sasa hawana soko, wanasakwa watoto wadogo walioko mitaani na hata shuleni,kama Mwalimu hana utu anaweza hata kuuza mtoto wako kwa sababu ya fedha, mtu yuko radhi kukupa pesa yoyote umtafutie mtoto mdogo wa kiume.

“Wanawapenda pia watoto wa kiume wanaochipukia kwenye ushoga ambao siku hizi ndiyo wapo kibao (wengi), watoto wanaharibika sana, wanaowatafuta wanapewa mpaka laki mbili hata zaidi kwa mtoto mmoja”.

Huku akiwataja kwa majina (yanahifadhiwa), Anti Suzy alisema mapedejee hao wana fedha nyingi hivyo wana ushawishi mkubwa, lakini alitoa angalizo kuwa si watu wote wanaoitwa pedejee wana mchezo huo, ingawa alikiri kuwa wengi wao hujitangaza kwa jina hilo wanapotaka kutafutiwa watoto au mashoga wapya kutoka nje ya mkoa kwa wanaoishi Dar es Salaam.

Akizungumzia ongezeko hilo sambamba na maambukizi ya Ukimwi, Anti Suzy aliyezaliwa
Bugando mkoa Mwanza mwaka 1986 akiwa kitinda mimba kwenye familia yao ya watoto watano, alisema hivi sasa mashoga wengi wameambukizwa ugonjwa huo na wengi wao wanafanya biashara ya kujiuza hivyo wanaendelea kuambukiza watu wengine.

Alisema mwanaume akimkuta shoga baa au katika ukumbi wa starehe kwenye Casino, na pembeni ikiwa kuna mwanamke anayejiuza, humchukua shoga jambo linalofanya
kuendelea kuathirika na kuharibiwa vibaya viungo vyao vya siri.

Alidai yeye alizaliwa akiwa na homoni nyingi za kike na wazazi wake walihangaika hospitali bila mafanikio na alipofika darasa la tatu alianza mchezo huo na mfanyabiashara wa kiarabu (jina tunalo) aliyekuwa akifanya kazi za ndani nyumbani kwake akitoka shule ili apate
fedha za mahitaji ya shule, ikiwemo sare.

Anti Suzy alidai mfanyabiashara  huyo alimtorosha kutoka nyumbani kwao Mwanza na kumpeleka Zanzibar ambako alikaa naye nyumba ya wageni (jina tunalo) kwa zaidi ya mwezi mmoja usiku na mchana akimwingilia jambo alilokuja kubaini baadaye kuwa ameharibu maumbile yake ya kiume.

Alisema pamoja na kuwa na wanaume wengine, alihisi ndiye aliyemuambukiza Ukimwi. “Siwezi kusema ni nani kaniambukiza Ukimwi lakini nahisi ni yule mwarabu, maana mashoga wengi nawafahamu wenye Ukimwi amewachezea sana yeye na pia ameharibu watoto wengi sana, sijui hivi
sasa yuko wapi lakini kweli ameharibu watoto sana na kama yupo hai basi huenda anaendelea kuwaharibu,” alibainisha Anti Suzy.

Siri nyingine aliyoitoboa Anti Suzy alidai, akiwa Dar es Salaam alifanya biashara ya kujiuza na kutembea na waume za watu wakiwemo vigogo nchini wanaopenda kutembea na mashoga kuliko wanawake na alikuwa na uwezo wa kutembea na wanaume watano hadi sita kwa siku wakati mwingine bila kinga, kutegemea na uwezo na matakwa ya wanaume hao na mara nyingine aliwalisha
dawa za kulevya na kuwaibia.

“Kweli nilikuwa naiba sana, kuna jamaa nilimlisha dawa, nikaiba na kugeuza mkono wa simu ya chumbani, simu zikapigwa hazipatikani, wakaja kabla sijatoka, wakamkuta jamaa amelala anakoroma mimi nimeshika baadhi ya vitu na pesa, jamani nilipigwaaa! nilipigwaaa! Lakini sikujali maana aibu ilikuwa kwake, ameshachukua malaya (shoga) watu walimjalia mpaka waandishi wa habari walimpiga picha,” alisema.

Aliwataka wanawake wafuatilie mienendo ya waume zao kwa kuwa japo baadhi yao wamejitangaza kuwa na Ukimwi, lakini wanaume wamekuwa wakiwataka na wengine wanawakimbia wake zao na kuwalazimisha mashoga wawalelee watoto wao kama alivyoletewa yeye mtoto wa mwaka mmoja na nusu na mwanaume aliyekuwa akiishi naye kama mume wake ingawa sheria za nchi haziruhusu.
Source: HabariLeo

Saturday, October 1, 2011

Hukumu ya Igunga leo

Best Blogger Tips
MACHO na masikio ya Watanzania, leo yanaelekezwa Jimbo la Igunga mkoani Tabora, ambako wananchi watapiga kura kumchagua mgombea mmoja kati ya wanane wanaoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge, kuwa mbunge wao.Mgombea atakayechaguliwa atamrithi Rostam Aziz, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, ambaye alijiuzulu katika tukio lililohusishwa na mchakato wa kujivua gamba ndani ya chama hicho.

Rostam alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 15 mfululizo kuanzia mwaka 1994 hadi alipojiuzulu Julai 13, mwaka huu.Wagombea wanaowania nafasi hiyo ni Leonard Mahoma wa CUF Joseph, Dk Dalaly Kafumu wa CCM na Kashindye wa Chadema.

Wagombea wengine wanaoshiriki uchaguzi huo na vyama vyao kwenye mabano ni Said Cheni (DP), Heme Dedu (UPDP), Hassan Rutegama (Chausta), John Maguma (Sau), na Steven Mahuyi (AFP).
 
Wagombea wote mbali na kujinadi kwa sera za kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo tangu kampeni hizo zilipoanza Septemba 7, mwaka huu walikuwa wakipigana vijembe wakati wote wa kampeni.

Kazi ya wagombea hao na vyama vyao kunadi sera imekamilika jana na leo wakazi wa Igunga, wataamua nani awawakilishe bungeni kama mbunge wao.

Polisi waimarisha ulinzi Igunga

Msemaji wa Jeshi la Polisi katika uchaguzi huo, Isaya Mngulu aliliambia gazeti hili kuwa, jeshi hilo limejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakamilika katika mazingira ya amani.

“Hadi leo (jana) tunapozungumza hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani na tunaamini hali itaendelea kuwa shwari na tunavitaka vyama viwaelimishe wanachama na mashabiki wao umuhimu wa amani,” alisema.

Mngulu alisema wapo polisi wa kutosha Igunga, kikiwamo Kikosi Maalumu cha Kutuliza ghasia (FFU) na kuonya watu kujaribu kuvuruga akisema watapambana na mkono wa dola.

“Nataka niwahakikishie wapiga kura kuwa wajitokeze kwa wingi na waende kupiga kura, ulinzi ni imara hakuna mtu atakayeletewa vurugu au kuzuiwa kupiga kura… kwa kweli tuko kamili,” alisisitiza Mngulu.

Alisema katika kuimarisha ulinzi huo, polisi wamefungua komandi ndogo nane, maeneo yenye wananchi wengi ya Simbo, Mwisi, Nkinga, Sungwisi, Ziba, Mwanshimba, Igurubi na Itumba ambazo zitakuwa katika utayari wa kukabiliana na chokochoko yeyote.

Polisi wapeperusha  bendera nyekundu
Magari ya polisi yanayotumika kusimamia ulinzi na usalama katika uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga, yameonekana yakirandaranda mitaani usiku na mchana huku yakipeperusha bendera nyekundu.

Mengi ya magari hayo aina ya Toyota Land Cruicer rangi ya bluu yameonekana yakizunguka mitaani na askari wa FFU, hali inayotafsiriwa kuwa ni kudhihirisha kuwa, atakayeleta chokochoko atakiona cha moto.

Juzi gari lililosheheni lita 80,000 za maji ya kuwasha, nalo lilionekana likitoka mafichoni katika kituo cha polisi Igunga na kuzunguka mitaani, katika kile kinachotafsiriwa kuwa ni kutoa ujumbe wa kuzatiti kwa jeshi hilo.

Msimamizi wa uchaguzi anena
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Igunga, Protas Magayane, alilsema jana kuwa vifaa vyote vya kupigia kura vilianza kusambazwa jana asubuhi.

Magayane alisema jimbo hilo lina kata 26 na wapigakura waliojiandikisha 170,077 na kwamba ili kuharakisha usambazaji wa vifaa unaenda vizuri, wamekodi malori 52 yatakayokwenda kila kata mawili kusambaza vifaa hivyo.

Magayane aliwataka wapigakura wafike mapema vituoni wakiwa na vitambulisho halali vya kupigia kura na si fotokopi na kwamba, watakapomaliza kupiga kura waondoke maeneo hayo wakisubiri matokeo.

“Kuna wapigakura wali-scan vitambulisho vyao au kutengeneza fotokopi, Hivyo havitaruhusiwa bali waje na vitambulisho 'original' (halisi) na waepuke kuvaa sare yoyote ya chama au kufanya kampeni vituoni,” alisema.

Hekaheka zatawala Igunga
Kumekuwa na hekaheka katika Jimbo la Igunga kwa siku mbili mfululizo sasa huku magari makubwa na madogo, baiskeli, bajaji, pikipiki na hata mikokoteni, ikipeperusha bendera za vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo.

Lakini kubwa ni magari ya viongozi na wafuasi wa vyama vikubwa vitatu vinavyoonekana kukabana koo vya CUF, Chadema na CCM ambayo yamekuwa yakiporomosha muziki unaosifu vyama na wagombea wao.

Tambo za hapa na pale baina ya wafuasi wa vyama vya Chadema CCM na CUF zinaonekana wazi kwenye vijiwe, nyumba za burudani na makazi ya watu.

Mbali pilikapilika hizo, helikopta za vyama hivyo nazo zilipasua anga kuanzia asubuhi jana kuelekea maeneo ya mikutano ya hadhara ya kuhitimisha kampeni hizo zilizodumu takribani siku 25.

Igunga yaelemewa na wageni
MJI wa Igunga unaelekea kulemewa na wageni wengi wakiwa ni viongozi na makada wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo mdogo wa ubunge.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa nafa za kulala katika nyumba za kulala wageni sasa hivi zimekuwa adimu kutokana na wingi wa wageni hao huku baadhi ya wamiliki wakipandisha gharama za malazi kwa siku.

Kila nyumba ya wageni utakayopita sasa utakutana na kibao chenye maandishi “hakuna nafasi” kutokana na vyumba kujaa kunakochangiwa na kuwapo kwa nyumba hizo chache ikilinganishwa na idadi ya wageni waliopo.

Inakadiriwa kuwa wageni kati ya 3,000 na 6,000 wako Jimboni Igunga hivi sasa. Wengi wao ni viongozi wa kisiasa wakiwamo viongozi wa kitaifa, wabunge, makada, wapiga debe wa vyama na wanahabari.

Ujio huo wa wageni unaonekana kuwanufaisha zaidi wamiliki wa nyumba hizo ambao baadhi wamelazimika kupandisha gharama za malazi kwa kati ya asilimia 10 na 20 ikilinganishwa na bei za awali.

Baadhi ya madereva na wapiga debe wa vyama vya siasa hivi sasa wanalazimika kulala kwenye magari na wengine wa jinsia moja kulala wawili kwenye chumba kimoja kutokana na upungufu wa vyumba.

Lakini ujio huo wa wageni umeongeza mzunguko wa fedha katika jimbo hilo ambapo mama lishe mmoja alisema: “Kimsingi, uchaguzi huu ni neema kwetu, tunatamani ufanyike kila mwezi.”

Wafanyabiashara wote, awe mama lishe, mmachinga, maduka ya nguo, migahawa na nyumba za starehe kama baa na kumbi za muziki wanaonekana kunufaishwa na ongezeko hilo la mzunguko wa fedha wilaya humo hivi sasa.
Source: Mwananchi

Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits