Muammar Gaddafi |
Wapiganaji wa waasi walifanikiwa kupiga picha kwa kutumia simu na kusambaza kwa baadhi ya vyombo vya habari. Walidai kuwa alionekana katika karavati akitambaa kujaribu kujificha katika kati mwa mji wa Sirte. Hata hivyo walimpiga risasi mguuni.
Mpiganaji wa waasi, Mohammed al Bibi aliwaambia waandishi wa habari kuwa baada ya kumwona Gaddafi alisikika akiwaambia askari hao: "Usipige risasi, usipige risasi," huku akiwa katika harakati za kujisalimisha. Kumekuwa na habari za utata kwamba alifariki dunia baada ya maumivu makali ya majeraha miguuni, huku wengine wakisema bado yu hai.
Waasi hao walidai kuwa alikutwa akiwa na bastola ya dhahabu huku akiwa amevalia sare ya jeshi rangi ya khaki. Ofisa mmoja wa Baraza la Mpito la Taifa, Abdel Majid Mlegta alisema Gaddafi alipigwa pia kichwani.
Alisema alipigwa risasi alipokuwa akijaribu kukimbia huku mpiganaji mwingine akidai kuwa alipigwa risasi tumboni. Gaddafi na familia yake walikuwa mafichoni tangu Umoja wa Majeshi ya Kujihami ya nchi za Magharibi, (NATO), na majeshi ya waasi kuanza kuishambulia Tripoli katika kati ya Agosti mwaka huu. Tukio hilo limetokea siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton kufanya ziara nchini Libya na kusema kuwa ana imani Gaddafi atakamatwa au kuuawa.
WAASI WAMALIZA KAZI SIRTE
MAJESHI ya waasi Libya yametangaza kumaliza kazi baada ya kufanikiwa kuuteka mji wote wa Sirte, nyumbani alikozaliwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Mummar Gaddafi. Askari hao walisema walifanya mashambulio ya nguvu yaliyodumu kwa muda wa dakika 90 jana asubuhi.
Hata hivyo baadhi ya askari wanaomtii Gaddafi bado wapo katika mji wa Bani Walid, kusini mashariki mwa Tripoli. "Hii ni siku ya mwisho ya mapigano," alisema Luteni Kanali Hussein Abdel Salam wa kikosi cha Misrata. Alisema katika awamu ya mwisho ya mapambano, waliweza kuwaona askari wa Gaddafi wakiwa wamejificha ndani ya nyumba kadhaa wakiwa na bunduki na silaha nyingine za kivita.
Serikali mpya ya Baraza la Mpito lilisema kuwa litatangaza Libya kuanguka baada ya kuuchukua mji wa Sirte. Wakati huo huo, Uingereza imeitaka Algeria kutoa ushirikiano dhidi ya Libya kuhusu familia ya Gaddafi ambayo imeomba hifadhi nchini humo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara nchini humo.
Mtoto wa kike wa Gaddafi, Aisha, kaka yake Hannibal na mama yao Safiya wamehifadhiwa nchini Algeria. Katika mkutano huo wa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria Mourad Medelci, Hague alisema Agleria haipaswi kusita iwapo hata mahakama ya uhalifu wa Kimataifa ukiomba lolote ni lazima isikilizwe.
Alisema ni vema Agleria ikafanya kazi kwa karibu na serikali ya mpito ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza baadaye.
Hata hivyo kwa upande wake, Medelci alisema watu hao wamepewa hifadhi kwa sababu za kibinadamu na hata serikali ya mpito ya Libya inatambua hilo.
No comments:
Post a Comment