MISRATA, Libya
MWILI wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Kanali Maummar
Gaddafi umezikwa katika sehemu ya siri jana, baada ya kuuawa kwake na
wapiganaji waliokuwa wakimpinga wiki iliyopita.
Mmoja wa
waopiganaji hao alijitokeza kwa mara ya kwanza jana kupitia mkanda wa
video akieleza kwamba yeye ndiye aliyechukua uamuzi wa kufyatua risasi
na kumuua Gaddafi, kwa kuwa hakuona haja ya kumshikilia akiwa hai.
Maziko
hayo yamefanyika baada ya kuwapo kwa mvutano baina ya wanafamilia wa
Kanali Gaddafi na uongozi wa sasa wa Libya ambao ni Baraza la Mpito la
Nchi hiyo (NTC) ambalo lilitangaza kuzika mwili huo kwa siri, ili
kuficha mahali lilipo kaburi la kiongozi huyo wa Libya kwa miaka 42.
Mwili
huo ulichukuliwa na kupelekwa kuzikwa kusikojulikana, baada ya ndugu na
watu wake kadhaa wa karibu kuruhusiwa kushiriki katika sala maalum na
taratibu zote za Kiislamu.
Mmoja wa wasemaji wa NTC alisema jana
kuwa mwili wa Gaddafi, mwanae Mutassim pamoja na mmoja wa wasaidizi wake
imezikwa, licha ya kuwapo kwa utata kuhusu pale ilipostahili kuzikwa.
Mvutano
uliokuwapo ulitokana na ombi la ndugu wa kabila la Kanali Gaddafi ambao
walikuwa wakitaka wapewe mwili wa kiongozi huyo ili wauzike mjini
Sirte, alipozaliwa, lakini viongozi wa baraza la kitaifa la mpito
walipinga ombi hilo.
Taarifa nyingine zinamnukuu msemaji wa NTC,
Ibrahim Beitalmal akisema ndugu wachache wa familia ya Gaddafi
walishiriki katika taratibu za ibada ya mazishi ya kiongozi huyo na dua,
vilivyofanyika kwa kuzingatia taratibu za dini ya Kiislamu.
Hata
hivyo, habari zaidi zinadai kuwa, baada ya sala hiyo, ndugu wa Gaddafi
hawakuruhusiwa kuona sehemu ambayo kiongozi huyo amezikwa ambako
kunadaiwa kuwa ni katikati ya jangwa.
Baadhi ya watu mjini
Misrata wanasema miili ya watu hao watatu iliondolewa usiku kutoka
sehemu ilipokiuwa imehifadhiwa katika harakati za kupanga mazishi hayo.
Raia
wa Libya wamekuwa wakitembelea eneo hilo la bucha katika mji wa Misrata
ambako miili hiyo ilipelekwa na kuhifadhiwa baada ya tangazo la kifo
cha kiongozi huyo na baadhi ya walinzi wake, kujionea mwili wake ili
kuthibitisha ukweli kuwa ameuawa.
Viongozi wa NTC walikuwa
wanahofia kuwa huenda Kanali Gaddafi akizikwa katika sehemu ya wazi,
kaburi lake litabadilishwa kuwa pahali patakatifu na wafuasi wake.
Pamoja
na hilo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishinikiza
uchunguzi ufanyike kubainisha jinsi alivyouawa Kanali Gaddafi, kwani
picha za awali zilionyesha kuwa alikamatwa akiwa hai.
Kiongozi wa
NTC, Mustafa Abdul Jalil, ametangaza kuwa uchunguzi utafanyika kuhusu
hilo. Hata hivyo, kuna wale wanaohoji ikiwa kweli uchunguzi huo utakuwa
wa wazi ikiwa mashirika ya kujitegemea hayakuhusishwa.
Katika
video iliyotolewa jana, kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza,
kijana mpiganaji anayedai kumuua Kanali Gaddafi baada ya kukamatwa
akiwa hai kwenye mtaro wa majitaka, alisema hakuona sababu ya kumuacha
aendelee kuwa hai na kumkabidhi kwa uongozi wa NTC.
“Tulimkamata,
nilimpiga katika paji la uso. Baadhi ya wapiganaji wenzangu walikuwa
wakilazimisha kutaka tumpeleke na kumkabidhi akiwa hai. Niliamua kumpiga
risasi mbili. Moja kichwani na nyingine kifuani,” alisema.
Katika
kutaka kuthibitisha hilo, kijana huyo alionyesha kipande cha nguo ya
Gaddafi kikiwa kimetapakaa damu na pete ya dhahabu ambayo alimvua baada
ya kumuua.
Tuesday, October 25, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment