Saturday, October 1, 2011

Hukumu ya Igunga leo

Best Blogger Tips
MACHO na masikio ya Watanzania, leo yanaelekezwa Jimbo la Igunga mkoani Tabora, ambako wananchi watapiga kura kumchagua mgombea mmoja kati ya wanane wanaoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge, kuwa mbunge wao.Mgombea atakayechaguliwa atamrithi Rostam Aziz, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, ambaye alijiuzulu katika tukio lililohusishwa na mchakato wa kujivua gamba ndani ya chama hicho.

Rostam alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 15 mfululizo kuanzia mwaka 1994 hadi alipojiuzulu Julai 13, mwaka huu.Wagombea wanaowania nafasi hiyo ni Leonard Mahoma wa CUF Joseph, Dk Dalaly Kafumu wa CCM na Kashindye wa Chadema.

Wagombea wengine wanaoshiriki uchaguzi huo na vyama vyao kwenye mabano ni Said Cheni (DP), Heme Dedu (UPDP), Hassan Rutegama (Chausta), John Maguma (Sau), na Steven Mahuyi (AFP).
 
Wagombea wote mbali na kujinadi kwa sera za kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo tangu kampeni hizo zilipoanza Septemba 7, mwaka huu walikuwa wakipigana vijembe wakati wote wa kampeni.

Kazi ya wagombea hao na vyama vyao kunadi sera imekamilika jana na leo wakazi wa Igunga, wataamua nani awawakilishe bungeni kama mbunge wao.

Polisi waimarisha ulinzi Igunga

Msemaji wa Jeshi la Polisi katika uchaguzi huo, Isaya Mngulu aliliambia gazeti hili kuwa, jeshi hilo limejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakamilika katika mazingira ya amani.

“Hadi leo (jana) tunapozungumza hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani na tunaamini hali itaendelea kuwa shwari na tunavitaka vyama viwaelimishe wanachama na mashabiki wao umuhimu wa amani,” alisema.

Mngulu alisema wapo polisi wa kutosha Igunga, kikiwamo Kikosi Maalumu cha Kutuliza ghasia (FFU) na kuonya watu kujaribu kuvuruga akisema watapambana na mkono wa dola.

“Nataka niwahakikishie wapiga kura kuwa wajitokeze kwa wingi na waende kupiga kura, ulinzi ni imara hakuna mtu atakayeletewa vurugu au kuzuiwa kupiga kura… kwa kweli tuko kamili,” alisisitiza Mngulu.

Alisema katika kuimarisha ulinzi huo, polisi wamefungua komandi ndogo nane, maeneo yenye wananchi wengi ya Simbo, Mwisi, Nkinga, Sungwisi, Ziba, Mwanshimba, Igurubi na Itumba ambazo zitakuwa katika utayari wa kukabiliana na chokochoko yeyote.

Polisi wapeperusha  bendera nyekundu
Magari ya polisi yanayotumika kusimamia ulinzi na usalama katika uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga, yameonekana yakirandaranda mitaani usiku na mchana huku yakipeperusha bendera nyekundu.

Mengi ya magari hayo aina ya Toyota Land Cruicer rangi ya bluu yameonekana yakizunguka mitaani na askari wa FFU, hali inayotafsiriwa kuwa ni kudhihirisha kuwa, atakayeleta chokochoko atakiona cha moto.

Juzi gari lililosheheni lita 80,000 za maji ya kuwasha, nalo lilionekana likitoka mafichoni katika kituo cha polisi Igunga na kuzunguka mitaani, katika kile kinachotafsiriwa kuwa ni kutoa ujumbe wa kuzatiti kwa jeshi hilo.

Msimamizi wa uchaguzi anena
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Igunga, Protas Magayane, alilsema jana kuwa vifaa vyote vya kupigia kura vilianza kusambazwa jana asubuhi.

Magayane alisema jimbo hilo lina kata 26 na wapigakura waliojiandikisha 170,077 na kwamba ili kuharakisha usambazaji wa vifaa unaenda vizuri, wamekodi malori 52 yatakayokwenda kila kata mawili kusambaza vifaa hivyo.

Magayane aliwataka wapigakura wafike mapema vituoni wakiwa na vitambulisho halali vya kupigia kura na si fotokopi na kwamba, watakapomaliza kupiga kura waondoke maeneo hayo wakisubiri matokeo.

“Kuna wapigakura wali-scan vitambulisho vyao au kutengeneza fotokopi, Hivyo havitaruhusiwa bali waje na vitambulisho 'original' (halisi) na waepuke kuvaa sare yoyote ya chama au kufanya kampeni vituoni,” alisema.

Hekaheka zatawala Igunga
Kumekuwa na hekaheka katika Jimbo la Igunga kwa siku mbili mfululizo sasa huku magari makubwa na madogo, baiskeli, bajaji, pikipiki na hata mikokoteni, ikipeperusha bendera za vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo.

Lakini kubwa ni magari ya viongozi na wafuasi wa vyama vikubwa vitatu vinavyoonekana kukabana koo vya CUF, Chadema na CCM ambayo yamekuwa yakiporomosha muziki unaosifu vyama na wagombea wao.

Tambo za hapa na pale baina ya wafuasi wa vyama vya Chadema CCM na CUF zinaonekana wazi kwenye vijiwe, nyumba za burudani na makazi ya watu.

Mbali pilikapilika hizo, helikopta za vyama hivyo nazo zilipasua anga kuanzia asubuhi jana kuelekea maeneo ya mikutano ya hadhara ya kuhitimisha kampeni hizo zilizodumu takribani siku 25.

Igunga yaelemewa na wageni
MJI wa Igunga unaelekea kulemewa na wageni wengi wakiwa ni viongozi na makada wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo mdogo wa ubunge.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa nafa za kulala katika nyumba za kulala wageni sasa hivi zimekuwa adimu kutokana na wingi wa wageni hao huku baadhi ya wamiliki wakipandisha gharama za malazi kwa siku.

Kila nyumba ya wageni utakayopita sasa utakutana na kibao chenye maandishi “hakuna nafasi” kutokana na vyumba kujaa kunakochangiwa na kuwapo kwa nyumba hizo chache ikilinganishwa na idadi ya wageni waliopo.

Inakadiriwa kuwa wageni kati ya 3,000 na 6,000 wako Jimboni Igunga hivi sasa. Wengi wao ni viongozi wa kisiasa wakiwamo viongozi wa kitaifa, wabunge, makada, wapiga debe wa vyama na wanahabari.

Ujio huo wa wageni unaonekana kuwanufaisha zaidi wamiliki wa nyumba hizo ambao baadhi wamelazimika kupandisha gharama za malazi kwa kati ya asilimia 10 na 20 ikilinganishwa na bei za awali.

Baadhi ya madereva na wapiga debe wa vyama vya siasa hivi sasa wanalazimika kulala kwenye magari na wengine wa jinsia moja kulala wawili kwenye chumba kimoja kutokana na upungufu wa vyumba.

Lakini ujio huo wa wageni umeongeza mzunguko wa fedha katika jimbo hilo ambapo mama lishe mmoja alisema: “Kimsingi, uchaguzi huu ni neema kwetu, tunatamani ufanyike kila mwezi.”

Wafanyabiashara wote, awe mama lishe, mmachinga, maduka ya nguo, migahawa na nyumba za starehe kama baa na kumbi za muziki wanaonekana kunufaishwa na ongezeko hilo la mzunguko wa fedha wilaya humo hivi sasa.
Source: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits