Sunday, October 9, 2011

Dk Mwakyembe mgonjwa

Best Blogger Tips
Rais Kikwete alipomtembelea Dr Mwakyembe
AFYA ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, ni tete baada ya kuugua ugonjwa uliomsababisha kuvimba mwili wote.Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na yeye mwenyewe zinaeleza kuwa, alianza kuwashwa ngozi miezi mitatu iliyopita kabla ya hali kubadilika siku za karibuni na hatimaye kuvimba sehemu kubwa ya mwili wake.

Mwakyembe alilieleza gazeti hili jana kuwa, baada ya  hali yake kubadilika alianza kupata matibabu katika hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam akiwa nyumbani kwake Kunduchi Beach.Akizungumza na gazeti hili kwa shida, Dk Mwakyembe alisema hajui chanzo cha ugonjwa huo wa ngozi, daktari wake ndiye anaweza kuelezea kwa usahihi.

“Ni kweli naumwa nipo nyumbani, hata sura yangu imebadilika. Sasa hivi namsubiri daktari wangu, nilisikia natakiwa kupelekwa India kwa matibabu, nasubiri kauli yake si mimi niamue,” alisema na kuongeza;
“Siwezi kusema nimelishwa sumu, ninachosema mimi nimevimba kweli mwili mzima naumwa kweli hapa nimelala na sijui umenipataje kwa simu kwa sababu huwa siiwashi muda huu una bahati kweli”.

Mke wa Dk Mwakyembe  Mkewe Linah Mwakyembe alipozungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Jumapili, alisema kwa mujibu wa daktari wake, Dk mumewe  anasumbuliwa na ugonjwa wa ngozi unaojulikana kitaalamu kama Exfoliative Dermatitis.
 “Alianza kuugua muda mrefu kidogo, kama miezi mitatu iliyopita, hali hiyo ilikuwa inatokea na kupotea hadi sasa ambapo hali imekuwa mbaya zaidi,” alisema.

Alisema madaktari waliomfanyia uchunguzi kwa nyakati tofauti katika kipindi hicho walitoa majibu tofauti na kuongeza kuwa wapo waliosema hali hiyo ilisababishwa na kisukari na mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kulikuwa na chembechembe za sumu katika damu yake.

“Baada ya ngozi yake kubadilika sana na hali kuwa mbaya, tulienda hospitali na madaktari walitupa majibu tofauti, wapo waliosema ni kisukari na kuna mwingine alisema kuna chembechembe za sumu,” alisema Linah na kufafanua  kuwa daktari aliyedai hivyo hakuwapa maelezo zaidi.
Kwa mujibu wa Linah, ngozi ya Dk Mwakyembe inawasha na inakuwa kama inatoa mba mwili mzima hadi kichwani.

Aliongeza kuwa daktari wake ameshauri ufanyike uchunguzi wa kina zaidi ili kujua kama atahitajika kupatiwa matibabu nje ya nchi.
“Walipendekeza afanyiwe uchunguzi zaidi, hivyo kama kutakuwa na ulazima wa kupatiwa matibabu zaidi nje ya nchi basi watatueleza,” alisema Linah.
Alisema kuwa leo ndio watapata  jibu kama atahitajika kwenda nje au kuendelea  na matibabu hapa nchini.

Alisema kumekuwa na uvumi mwingi juu ya ugonjwa wa Dk Mwakyembe na kusisitiza kuwa wao kama familia wanasikiliza kinachosemwa na madaktari na kile watakachoshauri.
“Sisi tunaendelea kusubiri kile kitakachogundulika baada ya uchunguzi huo na kama kutakuwa na mengine tutajulishwa na kujua hatua itakayofuata,” alisema Linah.

Exfoliative Dermatitis Kwa mujibu wa maelezo ya kitabibu, ugonjwa huu huweza kusababisha madhara makubwa ya mwili na matatizo mengine hivyo kuhitaji uangalizi wa karibu wa kitabibu.
Ugonjwa huu ukikomaa husababisha ngozi ‘kuwaka moto’ na huathiri wanawake na wanaume  lakini zaidi wanaume wenye umri kuanzia miaka 55.
Dalili  Dalili za ugonjwa huu ni kuwashwa, mwili kuishiwa nguvu pia sehemu ya juu ya ngozi hupukutika.

Chanzo  kwa mujibu wa maelezo ya kitabibu, sababu za ugonjwa huo bado hajizulikani, hata hivyo matukio ya ugonjwa huu mara nyingi yanahusishwa na magonjwa mbalimbali ya ngozi, madhara ya dawa kama penicillin, sulfonamides, isoniazid na phenytion.

Rais Kikwete amtembelea Baadaye mchana Rais Jakaya Kikwete alifika nyumbani kwa Dk Mwakyembe Kunduchi Beach kumjulia hali.
Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela mwaka 2008, aliongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Mkataba wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond.

Katika baraza jipya la mawaziri ambalo Rais Kikwete aliliunda mwaka jana, alimteua Dk Mwakyembe kuwa Naibu waziri wa Ujenzi akimsaidia Dk John Magufuli.

Mikasa ya Mwakyembe

Mei 21 mwaka 2009  Dk Mwakyembe alinusurika kufa katika  ajali mbaya ya gari eneo la Ihemi kilomita 40 kutoka Iringa mjini akiwa safari kutokea Mbeya kwenda Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za Polisi, gari alilokuwa akisafiria Toyota Landcruiser T362ACH,   liliacha njia  saa moja asubuhi baada ya kukanyaga shimo na tairi ya upande wa kulia kuchomoka na dereva wake, Joseph Msuya (30), kupoteza mwelekeo kabla ya gari hilo kutoka nje ya barabara upande wa kushoto na kuparamia mti kisha kupinduka.

Ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa Dk Mwakyembe akijaribu kulipita lori kabla ya kukanyaga shimo hilo.

Dk Mwakyembe na abiria wengine waliokolewa na Wasamaria wema pamoja na trafiki wawili  waliokuwa kwenye basi dogo wakisafiri kutoka Iringa kwenda Njombe.

Baada ya ajali hiyo alilazwa  katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa. Ilifahamika kuwa aliumia taya kisha alihamishiwa Dar es Salaam kwa matibabu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)  aliunda tume iliyoongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakati huo, Kamanda James Kombe,  kuchunguza chanzo cha ajali hiyo. Matokeo yalionesha kwamba ilisababishwa na uzembe wa dereva wake, Msuya.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits