MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM, Samuel Sitta amekiponda Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akidai kuwa muda wake wa kutawala
nchi bado, kwa kuwa hakina viongozi wa kutosha wa kufanya kazi za
Serikali ukimwondoa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa.
Sitta
ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema hayo
jana alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa CCM wa Wilaya ya
Karagwe, Kagera, alikokuwa katika ziara ya kutembelea ofisi za CCM.
Alisema
kuna upungufu mwingi katika safu ya uongozi wa chama hicho, kutokana na
kutokuwa na watu wenye uzoefu wa kufanya kazi za Serikali, badala yake
akidai kuwa kina baadhi ya viongozi wenye uzoefu wa kuongoza kumbi za
muziki... “Wote hapa mnasikia kwamba Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ni
mjuzi wa disko za usiku, sasa huwezi kulinganisha na CCM hata akitoka
mtu mmoja chama chetu hakiwezi kuyumba.”
Dk Slaa na Mbowe
hawakupatikana jana kuzungumzia kauli hiyo ya Sitta baada ya taarifa
kueleza kuwa Mbowe yuko nje ya nchi na alikuwa hapatikani kupitia simu
yake ya mkononi kama ilivyokuwa kwa Dk Slaa.
Hata hivyo, Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alipinga kauli hiyo akimtaka Sitta
aachane na chama hicho kikuu cha upinzani na atumie muda wake kukijenga
chama chake ambacho alidai kuwa kina makundi zaidi ya sita.
“Mwaka
2005 tuliweka mgombea Mbowe, mwaka 2010 tukamweka Dk Slaa, mwaka 2015
anaweza akarudi Mbowe, Dk Slaa au mwanachama yeyote wa Chadema,” alisema
Zitto.
Alisema Chadema ni taasisi na si chama cha makundi kama
ilivyo kwa CCM hivyo hakiwezi kumtegemea mtu mmoja... “Sitta asigombane
na Chadema, ajenge chama chake ili tukutane mwaka 2015.”
Akizungumza
na viongozi hao wa CCM Karagwe, Sitta alisema hakuna kiongozi mwingine
anayeweza kufanya kazi ya kukiongoza Chadema na kukifanya chama
kikubalike kwa umma.
“Hawa jamaa hawana hazina ya viongozi kama
tulionayo CCM, ambapo tunaweza kusimamisha wagombea 20 wa urais wenye
sifa zinazofanana tofauti na wao wanaye Dk Slaa tu ambaye inasemekana
aliukimbia upadri.”
Kuhusu CCM
Akizungumzia chama chake, Sitta
aliwataka viongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kutokaa kimya na badala yake
wajitoe na kujibu hoja za upinzani wanazozitoa kuikosoa Serikali iliyopo
madarakani ili ionekane haijafanya mambo ya maendeleo tangu kupatikana
kwa uhuru.
“Serikali ya CCM imefanikiwa katika maeneo mengi ya
huduma za jamii kama elimu, barabara, afya na mawasiliano, sasa
inashangaza kuona viongozi wa chama mnashindwa kufanya mikutano ya
kuwaeleza wananchi mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa sera na
ilani ya chama chetu.”
Sitta aliwataka viongozi chama hicho
nchini kuepuka mapambano na chuki miongoni mwao lakini akasisitiza
kwamba kinaendelea na mkakati wake wa kuwaondoa viongozi wanaodaiwa kuwa
ni mafisadi maarufu kwa jina la “magamba”.
Alisema chuki na
mapambano yanayoendelea ndani ya chama hicho ndiyo yanayochangia
kukidhoofisha na kuwapa la kusema wapinzani na hata kusababisha baadhi
ya wanachama kukihama.
“Mapambano ndani ya CCM ndiyo chanzo cha
migogoro na mitafaruku inayosababisha viongozi na wanachama wetu
kuombeana mambo mabaya na kutoa mwanya kwa watu wetu kuhamia upinzani.”
Sitta
yupo katika ziara ya siku tano ya kiserikali mkoani Kagera kukagua
miradi mbalimbali inayohusiana na mwingiliano wa uchumi na kijamii kwa
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Chanzo: Mwananchi
Thursday, August 30, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment