Thursday, October 25, 2012

Buriani Julius Kambarage Nyerere

Best Blogger Tips
Jenerali Ulimwengu
 MWALIMU Julius Kambarage Nyerere amefariki. Baba kaondoka. Jua limekuchwa. Mbuyu mkuu uliotanda katikati ya kijiji umenyauka. Zama zimefikia tamati. Watanzania ni yatima.

Ilani ilitolewa kwa muda wa kutosha. Wiki kadhaa za mateso ya maradhi ya Mwalimu katika Hospitali ya Mtakatifu Tomaso, mjini London, ingetakiwa iwe ni taarifa ya mapema ili watu wake wajiandae kwa lolote ambalo lingetokea. Kwa hakika taarifa za siku za mwisho zilionyesha wazi kwamba hakuwa mgonjwa wa kupona.

Hata hivyo, tangazo rasmi la kifo chake limeweza kuwashitua Watanzania, kama vile lilikuwa jambo lisilotarajiwa. Hali hii inaelezeka kwa utambuzi wa uhusiano maalumu kati ya Mwalimu na Watanzania, ambao walikataa kulizoea wazo la kifo chake.

Hadi jana asubuhi (Oktoba 14, 1999) wengi waliamini kwamba hata pale sayansi ya juu ilipokomea bado muujiza ungetokea na baba yao akainuka kitandani na kupanda ndege kurejea nchini.

Haiwezekani kuwalaumu hata wale walioshawishika kuegemea hisia za ushirikina. Watanzania walitaka mzee wao apone, na hawakukata tamaa hadi dakika ya mwisho. Ukweli ni kwamba hawakujua ni vipi wangeweza kuishi kama taifa bila Nyerere.

Haishangazi. Kwa muda wa nusu karne, nchi hii imetambulika na kujitambulisha kwa jina la Julius Kambarage Nyerere. Tangu alipojiunga na harakati za kudai uhuru mwanzoni mwa miaka ya 1950, Nyerere hajawahi kuondoka katika hisia za Watanzania.

Aliongoza kampeni ya uhuru kwa ujasiri mkubwa na kwa kufanya kazi bila kuchoka. Alitembelea kila kona ya nchi hii, akiwahamasisha wananchi kukataa ukoloni na kujiunga naye kudai uhuru. Kwa jinsi hii alijipatia fursa muhimu ya kuielewa nchi na watu wake, ujuzi ambao ulimfanya kuwa kiongozi aliyekuwa karibu na wananchi wake kuliko viongozi wengi wa Afrika na dunia.

Hata baada ya uhuru, alipokuwa kiongozi wa dola, hakuacha mtindo wake wa kwenda hadi vijijini, si katika sherehe na ngoma, bali kupiga kambi na kufanya kazi za sulubu bega kwa bega na wanavijiji, huku akiwafundisha alichokijua juu ya kilimo, au afya au ujenzi wa nyumba bora na huku akijifunza kutokana na uzoefu wa wananchi.

Baadhi yetu bado wanakumbuka kambi za Mwalimu katika mikoa ya Dodoma na Kigoma. Alikuwa mwalimu wa kweli, na alipenda kulifundisha taifa lake. Alijua kueleza dhana ngumu na tata kwa lugha nyepesi. Aidha alikuwa na kipaji cha ucheshi kilichomrahisishia mawasiliano.

Pia alikuwa ni msikilizaji makini aliyeweza kuhifadhi taarifa za maelezo marefu na misururu ya takwimu. Watanzania walimjua Nyerere kama kiongozi shupavu aliyeweza kukemea uovu, hasa dhidi ya wanyonge.

Alikuwa mtetezi asiyechoka wa watu wasiokuwa na uwezo na alipingana na kila aina ya unyanyasaji uliofanywa na watu wenye utajiri au vyeo. Alichukia rushwa na alipigana nayo hadi mwisho wa maisha yake.

Alikuwa safu ya mbele katika kupambana na ukoloni, ubeberu na ubaguzi na hakusita kuwakemea wakubwa wa dunia hii kila walipoonyesha dalili za kuwaonea au kuwapuuza wanyonge.

Mwalimu alikuwa miongoni mwa miamba wachache waliotetea haki za nchi ndogo na masikini katika mahafali yote ya kimataifa.

Alikuwa kiongozi asiyetetereka katika misimamo yake na uthabiti huo ulimwezesha kuwaongoza vyema Watanzania katika raha na katika taabu, katika amani na katika vita, Idi Amin alipovamia nchi yetu mwaka 1978 Nyerere alionyesha maana halisi ya cheo cha Amiri-Jeshi Mkuu kwa kusimamia mwenyewe maandalizi ya kivita ya kumwadhibu Amin na kujenga mawasiliano ya mara kwa mara na wananchi ili kuwaeleza kuhusu maendeleo ya vita. Kwa kumwondoa Amin madarakani, Nyerere alikuwa amesaidia dunia kuondokana na mwendawazimu hatari.

Mwalimu aliishi maisha ya kawaida, akakataa mbwembwe na ukwasi unaowatambulisha viongozi wengi wa nchi masikini. Alikwepa anasa na akajijengea mazingira yaliyowasuta wapenda makuu hapa nchini na nje ya nchi. Watu wa nchi nyingine walimstaajabu kwa mwenendo wake wa kujinyima katika mavazi na itifaki, tofauti kabisa na wenzake.

Katika mambo ambayo tungeweza kujifunza kutoka kwa Mwalimu Julius Nyerere ni ari yake ya kutaka kujua na kujiendeleza kila wakati. Wasomi wengi wameziacha bongo zao zikaota magugu kwa sababu ya kutojisomea. Mwalimu alisoma wakati wote, hata wakati akionekana kachoka. Jinsi hii aliweza kujipatia ujuzi na taarifa ambavyo vilimfanya awe na uwezo wa hali ya juu wa kuelewa masuala mbalimbali ya dunia.

Fursa ya kukaa na Mwalimu kwa muda wa saa moja wakati wowote ilikuwa ni fursa ya kunywa maji kutoka kisima cha elimu. Si bure kwamba Mwalimu Nyerere aliendelea kuenziwa na wananchi wa Tanzania, hata miaka mingi baada ya kuwa ameondoka madarakani. Kila wakati Mwalimu alipoitisha mkutano na waandishi wa habari, waandishi na wahariri waliingiwa na shauku kubwa ya kujua anataka kusema nini. Na kila alilosema lilichukuliwa kwa uzito mkubwa.

Si rahisi kufikiria mtu yeyote mwingine ambaye angeweza, kama Mwalimu, kufuta azimio la Bunge la kutaka iwepo serikali ya Tanganyika, mwaka 1993. Wala si rahisi kumfikiria mtu ambaye angeweza, kama Nyerere, kusema fulani hafai kugombea urais, na huyo fulani asigombee. Watu waliokuwa na bahati mbaya ya kukemewa na Nyerere hadharani walijikuta wanatembea na aibu muda mrefu.

Nguvu zake hazikuishia nchini. Kila alikokwenda Mwalimu Nyerere aliwavuta waandishi wa habari, wasomi na viongozi wakuu. Walimsikiliza kwa sababu walitambua kwamba ni mtu makini, mwenye akili na anayetetea maslahi ya watu wake na watu wa dunia ya tatu walio wanyonge na kwamba hakutafuta kujitajirisha binafsi.

Kwamba Rais wa Marekani, Bill Clinton na Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair walitaka wamlipie gharama za matibabu ni ishara ya jinsi alivyokuwa akithaminiwa na viongozi wa nchi za nje.

Heshima yote hii alipewa kwa sababu alitambulika kama mmoja wa Waafrika wachache walioweza kuongoza nchi zao kwa misingi ya ubinadamu na bila kuwaibia watu wao katika Bara lililojaa majambazi wanaojiita wakuu wa nchi, hii si sifa ndogo.

Hakuwa mtu wa kawaida. Sikuwahi kufanya kazi naye kwa muda mrefu, lakini mara chache nilipopata nafasi ya kuwa naye niligundua kwamba watu walioishi naye kwa muda mrefu halafu wakashindwa kujifunza kufikiri walikuwa na matatizo makubwa.

Ukali wa ubongo wake ulikuwa wa kusisimua na wenye uwezo wa kutekenya ubongo wako nao ufanye kazi. Mwalimu Nyerere ameliongoza taifa hili tangu mwaka 1954 na kwa muda wote huo, Watanzania wamemjua kwamba ndiye kiongozi namba moja.

Wako watu waliojaribu kubeza jina la “Baba wa Taifa” katika miaka ya karibuni, lakini sasa wametulia. Kwa karibu kila mtu, hilo ndilo jina lake na hiyo ndiyo hadhi yake.

Haishangazi, basi, kwamba wapo watu wenye wasiwasi kutokana na kifo chake. Wako wanaodhani kwamba baada ya kuondoka kwake, nchi itaingia kipindi cha mashaka makubwa, hata kuvurugika kwa amani.

Wako wanaodhani kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utavunjika kwa sababu mwasisi wake ametoweka. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwalimu hakusita kumkemea mtu yeyote, wa Bara au Visiwani, aliyemwona kama anataka kuuvunja Muungano.

Sasa ni dhahiri kwamba hakuna mtu atakayekuwa na uzito wa kuweza kuwakemea wachafuzi, na hawa ni wengi. Aidha yako makundi ya watu nchini yanayodhani kwamba kifo cha Mwalimu kinawaacha katika hali inayoweza kuwaletea matatizo, wakaonewa, kunyanyaswa au kudhuriwa kwa namna nyingine.

Watanzania wenye asili ya nje wanao wasiwasi wa aina hiyo. Baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani kadhalika wanaamini kwamba katika uhai wake, Mwalimu alikuwa ni kinga dhidi ya matumizi ya mabavu dhidi ya wapinzani.

Inawezekana hisia zote hizi hazina msingi na kwamba watu wanahofu zinazotokana na kukojua mustakabali wa taifa hili utakuwaje. Kila taifa hupata mashaka kama haya linapoondokewa na kiongozi wake mwasisi. Waasisi ni watu adimu. Hutokea mara moja katika maisha ya taifa. Mwalimu ni miongoni mwa hao. Anachangia nafasi na George Washington, Simon Bolivar, Jose Marti, Mahtma Gandhi/Jawaharlal Nehru na wengine kama hao.

Kwa sababu kufa ni lazima, waasisi nao hufa. Wanapokufa huacha majonzi na hofu, lakini wanaobaki baada yao wanatakiwa kuwa na moyo mkuu, kuelewa kwamba kifo cha mwasisi, kiwe na majonzi kiasi gani, si mwisho wa dunia.

Maisha lazima yaendelee. Njia moja muhimu ya kumuenzi Nyerere kama Baba wa Taifa na mwalimu wetu ni kudhihirisha kwa vitendo kwamba ni kweli alikuwa baba mwema aliyelea vizuri, na mwalimu mahiri aliyetufundisha tukaelimika na tukawa na busara. Tujitahidi kuepuka chokochoko na ukorofi unaoweza kuleta mfarakano katika jamii.

Tukifanya hivyo tutakuwa tumeheshimu wasia wake. Vinginevyo, tutaruhusu migawanyiko isiyo na maana. Au tukianza kuwaonea wanyonge na kuruhusu mambo ya hovyo katika jamii yetu tutakuwa tunamtukana baba yetu na kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajitukana wenyewe.

Taifa hili sasa linahitaji moyo mkuu na mshikamano wa hali ya juu, pamoja na ukomavu unaotakiwa kwa kila mwana ampotezaye mzazi wakati amekwishakukomaa.

Mola ailaze roho ya Mwalimu mahali pema peponi. Amina.

Makala hii ya tanzia iliyoandikwa na Jenerali Ulimwengu ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa gazetyi hili la Raia Mwema, ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Mtanzania, Oktoba 15, mwaka 1999, siku moja baada ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Tumeichapisha hapa kutokana ujumbe wake mzito kwa Watanzania-Mhariri Mkuu.
Chanzo: Raia Mwema

Wednesday, October 17, 2012

Vurugu kubwa Dar, Zanzibar

Best Blogger Tips
 POLISI mkoani Dar es Salaam na wale wa Kisiwani Zanzibar, jana walitumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kusambaratisha makundi ya watu wanaodaiwa kuwa waumini wa Dini ya Kiislamu, waliopanga maandamano kushinikiza kuachiwa kwa viongozi wao.

Kisiwani Zanzibar vurugu kubwa ziliibuka baada ya kusambaa taarifa kuwa Kiongozi wa Kundi la Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed alitekwa nyara juzi saa 3 usiku akiwa kwenye gari lake na dereva wake.

Vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa mali kadhaa ikiwamo Maskani Kaka ya Kisonge inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo ilichomwa moto na waandamanaji.


Waandamanaji hao pia walichoma moto baa za Darajani na Mbawala eneo la Mikunguni na baadhi ya nyumba za kulala wageni, kabla Vikosi vya Kutuliza Ghasia (FFU) na Kikosi cha Zima Moto kudhibiti vurugu hizo kwa mabomu ya kutoa machozi.

Pia magari kadhaa yalichomwa moto na kuharibiwa vibaya yakiwa yameegeshwa katika maeneo mbalimbali, huku mipira na matairi vikichomwa katika barabara kadhaa.

Katika maeneo ya Mjini baadhi ya njia zilifungwa na watu waliokuwa wakitoka kazini walishindwa kwenda nyumbani. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni yale ya Malindi, Darajani hadi Michenzani ambako njia zilifungwa na mabomu yalisikika yakipigwa mfululizo.

Katibu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheik Abdallah Said alisema,
“Taarifa tulizonazo ni kwamba Sheikh Farid ametoweka katika mazingira ya kutatanisha…Alitoka kwake Mbuyuni katika gari yeye na kijana wake wa hapo nyumbani, lakini baadaye kuna gari ikamfuata na kusimama na ndipo alipoingia katika hilo gari jingine na hakuonekana tena. Hatujui ni kina nani waliomchukua na hatujui ilikuwaje akaingia katika hilo gari ...”

Polisi waliimarisha ulinzi katika baadhi ya maeneo hasa Msikiti wa Mbuyuni ambao uko jirani na makazi ya Sheikh Farid. Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema polisi halihusiki na kukamatwa kwa Farid, lakini wao wanaamini kwamba ‘amejipoteza’ mwenyewe na kujificha.

Kamishna Mussa alisema polisi watawasaka wote waliosababisha vurugu hizo, na kwamba hadi sasa hawafahamu chanzo chake bado.

“Tunafanya uchunguzi zaidi kujua chanzo cha fujo hizo ingawa mimi sijui habari za kutekwa Farid, sasa tunasema tunachunguza chanzo cha vurugu hizo na tukishapata uthibitisho na waliosababisha tutawafikisha mahakamani kujibu mashtaka,” alisema kamishna huyo.

Ilivyokuwa Zanzibar
Vurugu hizo zilianza katika maeneo mbalimbali muda mfupi baada ya vijana kadhaa kukusanyika katika eneo la Darajani kando ya Soko Kuu majira ya asubuhi, kutokana na kuzagaa kwa taarifa kwamba Sheikh Farid alikuwa haonekani.

Idadi ya vijana hao ilikuwa ikiongezeka kadiri muda ulivyosonga, huku wengi wao wakiwa na silaha za aina mbalimbali zikiwamo magongo na mawe, hali iliyoibua hofu kwa wafanyabiashara wa eneo hilo, hivyo baadhi yao waliamua kufunga maduka.

Maeneo yalioharibiwa ni pamoja na baadhi ya nyumba za kulala wageni ambazo zimechomwa moto katika eneo la Amani, huku baadhi ya vijana wakionekana wakikimbia na kreti za pombe.

Katika eneo la Darajani, vijana kadhaa wakishirikiana na Wamachinga, walionekana wakivunja kisha kuingia katika moja ya maghala ya kuhifadhia bia, ambako walipora bidhaa zote zikiwamo kreti kadhaa za bia zilizokuwa zimehifadhiwa humo.

Baadhi ya wenye maduka walifunga na kutoweka, lakini waporaji waliiba baadhi ya bidhaa vikiwamo vyakula, kisha  kutokomea navyo kusikojulikana.

Katika maeneo ya Ng’ambo ambayo ni Amani, Mikunguni, Kwerekwe na Daraja Bovu vijana walioonekana kuwa na hamasa, waliingia kwenye makazi ya watu na kuiba vitu kadhaa, na kila mabomu yalipopigwa walikimbilia vichochoroni na baada ya muda walirejea tena.

Maeneo ya Malindi, Michenzani na  Rahaleo, kulikuwa na vurugu za urushaji mawe na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika maeneo hayo.

Matawi ya miti ilikatwa na kuunganishwa na magari mabovu kuwekwa barabarani kisha kuchomwa moto. Hali hiyo ilisabababisha uharibifu mkubwa katika baadhi ya barabara, na katika fujo hizo baadhi ya vijana walikamatwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma Mohammed alithibitisha kutokea kwa fujo hizo na kusema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi kujua chanzo chake na taarifa kamili zitatolewa baada ya kukamilika uchunguzi huo.

Ponda Dar
Jijini Dar es Salaam, baadhi ya watu walipanga kufanya maandamano hadi Makao Makuu ya Polisi, kupinga kukamatwa kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda aliyekamatwa juzi usiku na kushikiliwa kutwa nzima ya jana katika Kituo Kikuu cha Polisi.

Ponda alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani jijini Dar es Salaam, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisisitiza kuwa polisi wamechoka kuvumilia harakati zake za kutaka “nchi isitawalike”.

“Kuanzia leo uvumilivu kwa Jeshi la Polisi dhidi ya watu wasiofuata sheria za nchi umekwisha. Kwa kuwa Ponda ni mtu anayepotosha watu waliopo chini yake wanaotaka kuandamana bila utaratibu wasitulaumu kwa lolote lile litakalotokea,” alisema Kova.

Kova alisema hadi jana Ponda alikuwa bado anahojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba ushahidi ukijitosheleza, atafikishwa mahakamani wakati wowote.

Alisema taasisi anayoingoza Sheikh Ponda haijasajiliwa kwa mujibu wa sheria kufanya shughuli za dini. Hivyo basi shughuli zote zinazoendesha na taasisi hiyo si halali.

"Natoa wito pia kwa wafuasi wa kiongozi huyo, walioshiriki katika vurugu mbalimbali za hivi karibuni, wajisalimishe haraka kwa kuwa sasa tupo katika mchakato wa kuwasaka, kuwakamata na baadaye kuwafikisha mbele ya sheria," alisema.

Tuhuma za Ponda
Kamanda Kova alidai kuwa Sheikh Ponda amekuwa akichochea vurugu na kuwashawishi wafuasi wake kuidharau Serikali na vyombo vya usalama.

“Ponda amekuwa ni mtu ambaye amefanya nchi hii, hasa katika Jiji la Dar es Salaam kukaa katika hali ya wasiwasi. Ijumaa imekuwa siku ya fujo badala ya kuwa siku ya amani,” alisema Kova.

Alisema vurugu hizo zinazoongozwa na Sheikh Ponda zimekuwa zikisababisha baadhi ya watu kushindwa kwenda kazini siku za Ijumaa na hali hiyo haivumiliki tena.

Kamanda Kova alitaja tuhuma nyingine dhidi ya Sheikh Ponda kuwa ni kuongoza kundi la watu kwenda kuvamia kiwanja namba 311/3/4 eneo la Chang’ombe ambacho kinamilikiwa  na kampuni Agritanza.

"Kiwanja alichokwenda kukivamia kilikuwa mali ya Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) na kiliuzwa kihalali kwa kampuni hiyo," alisena.

Alitaja tuhuma nyingine kuwa ni kufanya maandamano kinyume cha sheria, ikiwamo kuweka kambi Makao Makuu ya Polisi bila kibali cha jeshi hilo wiki kadhaa zilizopita.

Kamanda huyo alisema Ponda anashikiliwa pia kwa kuwa mstari wa mbele kupambana na vyombo vya dola  na Serikali, ikiwa ni pamoja na kushawishi wafuasi wake kumdharau Rais wa nchi.

“Vilevile amekuwa akiendesha maandamano na kukusanyika Kiwanja cha Kidongo Chekundu, huku wakijitapa kuwa wana nguvu zaidi ya Jeshi la Polisi,” alieleza Kova.

Polisi pia wanamtuhumu Ponda kwa kuanzisha vurugu na vitisho dhidi ya Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mufti Shaaban Bin Simba na kutaka kumtoa madarakani kwa nguvu pamoja na kutaka kuvamia ofisi yake.

Alikamatwaje?
Kamanda Kova alisema Ponda alikamatwa na askari waliomuwekea mtego kutokana na yeye kuwa bingwa wa kutoroka kila akifanya matukio.

“Askari waliowekwa maalumu kwa ajili ya kumkamata walifanikiwa kumtia nguvuni saa 4:00 usiku karibu na eneo la maficho yake ambako alipelekwa na pikipiki,” alisema Kova.

“Hivi Ponda ni nani mpaka awe na uwezo wa kumpa Rais aliyechaguliwa na wananchi siku saba kuwaachia watu waliopo mahakamani yeye amechaguliwa na nani kuongoza taasisi aliyonayo na anatoa wapi nguvu za kufanya mambo yote hayo?,” alihoji Kova.

Alisema kulingana na matukio anayoyaongoza Ponda, wananchi wameanza kuona kama anaogopwa na vyombo vya dola, jambo ambalo siyo kweli.

Aliongeza kuwa polisi wana uwezo wa kumdhibiti, isipokuwa walikuwa wanatumia busara tangu alipoanza vurugu na kwa sasa uvumilivu umewashinda, hivyo wataanza kumshughulikia.

Vurugu zazuka
Kukamatwa kwa Sheikh Ponda kulizua vurugu jijini Dar es Salaam na kufanya baadhi ya wakazi wake hasa maeneo ya Mnazi Mmoja na Kariakoo, kuingiwa kiwewe baada ya polisi kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha ili kuwasambaratisha watu waliokuwa wanataka kuandamana kwa lengo la kushinikiza kiongozi huyo aachiwe.

Hali hiyo ilisababisha watu kukimbia ovyo katikati ya iji na kuongezeka kwa misongamano ya magari, jambo lililofanya usafiri wa daladala kuwa mgumu kwenda na kutoka katikati ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam.

Baadhi ya wafanyabiashara walifunga maduka yao wakihofia kuporwa mali wakati wa vurugu hizo, baada ya vibaka kujichanganya wakijaribu kufanya uhalifu huo.

Katika eneo la Mnazi Mmoja, polisi walirusha maji ya kuwasha kusambaratisha kundi la watu hao, huku wengine wakiwa wanadhibitiwa walipokuwa wakienda Makao Makuu ya Polisi ili kumtoa kiongozi huyo.

Baadhi ya mashuhuda walisema, mbali na Ponda watu hao walikuwa wanataka kwenda polisi kuwatoa watu waliokuwa wanashikiliwa kituoni hapo kwa tuhuma za kufanya vurugu na kuharibu makanisa katika Kata ya Mbagala wilayani Temeke.
Chanzo: Mwananchi

Saturday, October 13, 2012

Mshtuko mauaji ya RPC Mwanza

Best Blogger Tips
 SIMANZI imegubika Jiji la Mwanza na vitongoji vyake baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (55),  kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa  manane wa kuamkia jana.Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Said Mwema alithibitisha tukio hilo akieleza kuwa amemwagiza Kamishna wa Makosa ya Jinai nchini, Robert Manumba kwenda kuchunguza mauaji hayo.

“Tunasikitishwa kwa mauaji hayo na ninawaomba Watanzania wawe watulivu wakati tukishughulikia kuwakamata watu waliohusika katika tukio hilo,” alisema IGP Mwema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Mbali ya kumuua Kamanda Barlow, wauaji hao waliokuwa wamevalia makoti yanayovaliwa na watu wa ulinzi shirikishi (Polisi Jamii), walichukua na bastola ya kamanda huyo, simu mbili za mkononi pamoja na ‘radio call’ ya Jeshi la Polisi.

Hili ni tukio la tatu kwa Ofisa wa juu wa Polisi kuuawa mkoani Mwanza. Tukio la awali lilitokea mwaka 2007, ambapo aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza, ASP Mahende aliuawa kwa kupiga risasi eneo la Bugando saa 4:00 usiku wakati akifuatilia majambazi waliokuwa wakijitayarisha kuvamia.

Mwaka 1987, Inspekta Gamba aliuawa na majambazi katikati ya Jiji la Mwanza.
Kamanda Barlow aliuawa wakati akiendesha gari lake binafsi, aina ya Toyota Hilux Double Cabin na wakati wa tukio hilo hakuwa na mlinzi wake kwa kuwa kamanda huyo alikuwa katika shughuli binafsi.

Hata hivyo, mauaji hayo yamezua hisia tofauti huku wengine wakieleza kuwa ni kifo cha bahati mbaya na kwamba, wauaji walidhani ni mwananchi wa kawaida na wengine wakisema huenda ulikuwa mpango maalumu uliolenga kumwangamiza kwa kulipiza kisasi.

Taarifa ya Mkuu wa Mkoa
Akizungumza na waandishi wa habari jana saa 2:57 asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa kifo cha Kamanda Barlow kimetokea saa 8:00 usiku katika eneo la Kitangiri, Barabara ya Kona ya Bwiru karibu na Hoteli ya Tai Five.

Alisema kuwa kamanda huyo aliuawa alipokuwa akimrejesha mmoja wa wanawake waliokuwa nao katika kikao cha maandalizi ya harusi ya ndugu yake.

Mkuu huyo wa mkoa alimtaja mwanamke huyo aliyekuwa na marehemu kuwa ni Doroth Asasia Moses ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyamagana B.

 “Marehemu alikuwa katika kikao cha harusi ya anayedaiwa kwamba ni mtoto wa dada yake, Semburi Moleto kilichofanyika katika Hoteli ya Florida, Mtaa wa Rufiji. Kikao kilipomalizika tunaambiwa majira ya kati ya saa 4 hadi 5 usiku, alimchukua mwanamke huyo kama ‘lift’ ili kumsaidia kufika nyumbani kwake,”alieleza.

Alisema kuwa alipofika nyumbani kwa mwanamke huyo aliona watu waliokuwa wakimulika tochi  waliokuwa wakilalamika kuwa wameumizwa na mwanga wa taa za gari lake.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema walipofika katika gari, aliwauliza iwapo wanamfahamu na waliposhindwa kumjibu Kamanda Barlow alichukua radio ya mawasiliano ya kipolisi ili kuwasiliana na askari wake, ndipo wauaji hao walimpiga risasi eneo la shingo na kufariki papohapo.

“Kamanda wetu inaonekana amefariki kutokana risasi hiyo, ambayo imemvunja shingo yake na imepigwa kutokea upande wa kiti cha abiria na kumpitia begani na kuingia shingoni,” alisema Ndikilo na kufafanua:

“Baada ya kumuua, watu hao walipora bastola yake, ‘radio call’ hiyo pamoja na simu zake mbili za mkononi na mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mahojiano na kusaidia upelelezi.”

Kilichomponza RPC
Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinamkariri shuhuda wa tukio hilo (Dorah) akieleza  kwamba, kilichomponza Kamanda Barlow ni kuwadharau wauaji hao baada ya kuona wamevalia vikoti vyenye rangi ya kijani vilivyokuwa na maandishi ya Polisi Jamii, alidhani kuwa na watu wa ulinzi shirikishi.

Baadhi ya maofisa wa polisi wameeleza kuamini kuwa watu hao walikuwa ni Polisi Jamii ndiko kulikomponza marehemu Barlow kwa kuwa aliamini kuwa alikuwa katika mikono salama, hali ambayo ilimfanya kutojiandaa kupambana nao.

Mwalimu Doroth
Mwalimu Doroth aliyekuwa na marehemu wakati wa tukio hilo, ambaye kwa sasa anashikiliwa kuhusiana na mauaji hayo ni mjane wa marehemu Modest Lyimo ambaye zamani alikuwa ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), aliyefariki mwaka 1997 wakati huo Kamanda Barlow akiwa na OCD wa Kituo cha Kati.

Lyimo alifariki na kumwacha Doroth akiwa na mtoto mmoja, lakini baadaye mwalimu huyo alizaa watoto wawili na mwanamume mwingine hivyo kuwa na watoto watatu (majina yanahifadhiwa kwa sasa).

Eneo la mauaji
Mwandishi wa gazeti hili alipofika nyumbani kwa Mwalimu Moses alikuta askari watatu wa jeshi la polisi wakilinda na kumkagua kila mtu aliyekuwa akiingia katika nyumba hiyo  na kutoka.

Mauaji yalivyotokea
Mmoja wa watoto wa mwalimu huyo, Kenrogers Edwin, ambaye alishuhudia tukio hilo la kuuawa kwa Kamanda Barlow, aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa siku hiyo usiku kabla ya tukio, alipigiwa simu na mama yake aliyemwarifu kuwa alikuwa amefika na kumtaka amfungulie mlango.
Edwin alisema kuwa anakumbuka pia katika maongezi ya simu mama yake alimweleza kwamba alikuwa akija na mgeni kwa ajili ya kutambua nyumbani anapoishi.

Alisema kuwa wakati akifungua geti ili gari alilokuwamo mama yake (Doroth), pamoja na mgeni wao (Kamanda Barlow) liingie ndani, aliona watu wakiwa wamezunguka gari hilo.

“Ilikuwa saa 8 usiku, nilipofungua geti ili aingie, niliona watu watatu wakiwa upande wa dereva wa gari na wawili upande mwingine aliokaa,” alisema na kuongeza:
“Niliona wakimnyang’anya mama mkoba na simu na nilisikia wakibishana, lakini baadaye nilisikia mlio wa risasi.”

Alieleza kwamba anakumbuka kuwa baada ya mlio huo wa risasi alilazimika kulala chini kwa kuogopa na kwamba baada ya Kamanda Barlow kupigwa risasi, wauaji hao walikimbia walipoona pikipiki ikija eneo hilo kwa kasi.

Aliyemhudumia  Baa
Mhudumu wa baa, Benard Kanyabukala, ambaye alimhudumia Kamanda Barlow katika kikao hicho alisema kuwa baada ya kikao hicho kumalizika, kamanda huyo aliagiza sanduku moja la bia kwa ajili ya wajumbe waliokuwapo katika kikao hicho na yeye (mhudumu) alinunuliwa kinywaji aina ya Alivaro.

“Aliomba bili na nilipompa alinifokea akidai nimemzidishia bei. Awali nilimweleza kuwa bei ya kreti ni Sh36,000, lakini kutokana na baadhi ya watu kutokunywa bia na kubadilisha vinywaji bei ilizidi na kuwa Sh40,700, ingawa baada ya kumwelewesha alilipa na kuongeza bia nyingine kwa raundi ya mwisho zenye thamani ya Sh 30,800,” alisema Kanyabukala.

Alieleza kwamba, wakati wa kikao hicho Kamanda Barlow alikuwa akinywa bia aina ya Serengeti, lakini mara ya mwisho alipoagiza vinywaji alikunywa maji ya Kilimanjaro na waliondoka hapo saa 8:30 usiku akiwa na mwanamke mmoja.

Mmiliki wa baa
Mmiliki wa baa ya Florida, kilipofanyika kikao hicho, Ritha Mosha alielezea kuwa, Kamanda Barlow alifika katika baa hiyo kwa mwaliko wa Semburi Moleto, ambaye yeye na Kamanda Barlow wote ni Wachaga waliozaliwa Kijiji cha Kiyou, Tarafa ya Vunjo Marangu, mkoani Kilimanjaro.

“Mimi ilikuwa ni mara yangu ya pili kuonana naye siku hiyo.  Kijana anayetarajia kuoa alinieleza kuwa, alimwomba Kamanda Barlow amsimamie kama mzazi wake katika arusi yake na ndiye aliyesimamia kikao hicho,  ndiyo aliyeongoza sala ya kufungua kikao hicho,” alieleza Ritha.

Alisema kuwa kikao hicho kilichelewa kuanza kutokana na wajumbe kuchelewa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jijini hapo.

Alifahamisha kuwa kikao hicho kilianza saa 2:21 usiku na kwamba kamanda huyo alikuwa msemaji wa familia.

Idadi ya wanawake
Ritha alifahamisha kuwa, kikao hicho kilitarajiwa kuwa na  wajumbe 100, lakini walifika kati ya 55 hadi 60 na kati ya hao kulikuwa na wanawake wawili ambao  aliwataja kwa majina ya Christina Mosha, mkazi wa Nyakato na Doroth ambaye alisindikizwa na kamanda huyo.
Chanzo: Mwananchi

Serikali yafikishwa mahakama ya The Hague

Best Blogger Tips
 KITUO  cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeipeleka Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), kutokana na matukio 24 ya mauaji yanayokiuka haki za binadamu yaliyotokea nchini kati ya Januari na Septemba mwaka huu.

Mbali na hilo, LHRC kimepeleka taarifa hizo kwa Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Kimataifa, anayeshughulika na masuala ya mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo vya dola.

Hatua hiyo ya LHRC inatokana na ripoti tatu zilizotolewa  hivi karibuni kuchunguza kifo cha aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi kilichotokea katika Kijiji cha Nyololo, Mkoa wa Iringa, Septemba 2 mwaka huu.

Ripoti hizo ni ile ya Kamati ya Kuchunguza Mauaji hayo iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi iliyokuwa chini ya Jaji Steven Ihema; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyokuwa chini ya Jaji Kiongozi Mstaafu, Amir Manento na ile ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), iliyoongozwa na John Mirenyi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba alisema kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, jumla ya watu 24 wameuawa na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama.

“Tumepeleka mashtaka 24 ICC tangu Septemba 28 mwaka huu, ambayo yanahitajika kufanyiwa uchunguzi na kuchukua hatua kali dhidi ya Serikali ya Tanzania ambayo imekuwa ikiwalinda viongozi wake wanaokiuka haki za binadamu,” alisema Dk Bisimba.

Alisema taarifa hizo pia wamezipeleka kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu katika kikao kinachoendelea huko Ivory Coast, lengo likiwa ni kuchunguza na kuchukua hatua katika Mahakama ya Afrika.

“Tunatarajia kuona uwajibikaji wa viongozi wote wa Serikali na vyombo vya dola waliohusika kwa njia yoyote ile. Hatua hizo au uwajibikaji huo ni pamoja na kujiuzulu, kuachishwa kazi na kufikishwa Mahakamani, ” alisema.

Aliitaka Serikali kuacha propaganda zinazotaka kuchochea vurugu katika taifa huku akisema inapaswa itambue kuwa hivi sasa nchi iko katika zama za vyama vingi vya siasa na kuacha kutumia vyombo vya dola kuleta chuki na mafarakano.

Dk Bisimba alisema baada ya kupitia taarifa zote tatu, LHRC kimesikitishwa na taarifa ya Kamati ya Dk Nchimbi... “LHRC hakijashangazwa sana pale taarifa hiyo ilipoonyesha wazi nia ya kuwalinda watuhumiwa kwa kuwa Serikali yetu bado haijajenga mfumo wa kujichunguza na kujiwajibisha yenyewe.”

“Serikali imeudhihirishia umma kuwa haikuwa na nia ya dhati ya kuchunguza suala la mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi, bali ilikuwa na lengo la kulisafisha Jeshi la Polisi na kuwalinda maofisa wake.”

Dk Bisimba alisema tangu mwaka 2001 hadi sasa, kituo hicho kimekuwa kikifuatilia kwa karibu matukio mbalimbali ya mauaji yanayoendelea kufanywa na vyombo vya dola na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika.

Werema ashangaa, mawakili watofautiana
Akizungumzia suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema hana taarifa za Serikali kushtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague.

“Kwa nini wameamua kutushtaki katika Mahakama ya The Hague? Kwani hapa nchini hakuna mahakama au wameona ni bora wavuke mipaka... Kwa sasa siwezi kulizungumzia zaidi suala hilo.”

Wakili wa Kujitegemea, Gaudioz Ishengoma alipotakiwa kuzungumzia hilo alisema anaunga mkono uamuzi wa kituo hicho kuipeleka Serikali kwenye Mahakama ya Kimataifa.

Alisema hilo ndilo eneo sahihi ambalo Serikali inatakiwa kupelekwa kwa sababu ya ukiukaji wa haki za binadamu na kwamba huko ndiko ambako haki inaweza kupatikana.

Hata hivyo, Wakili mwingine wa Kujitegemea, Majura Magafu alipinga hatua hiyo akisema kituo hicho kimekosea kuipeleka Serikali The Hague kwa kuwa imekuwa ikichukua hatua za kisheria dhidi ya makosa mbalimbali ya mauaji ambayo yamekuwa yakitokea.

“Kwa mawazo yangu, hawa LHRC wamekosea nadhani wamefanya hivyo kwa masilahi yao binafsi hasa ili kuonyesha kwamba wanafanya kazi,” alisema.

Alisema hata kama Serikali itakuwa imeshindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wauaji, kituo hicho kilitakiwa kuishtaki Serikali katika mahakama za hapa nchini.

“Hawa sijui wanataka kutupeleka wapi kwa sababu wananchi wengi wa Afrika wakiwemo wa Kenya wamekuwa wakitaka mashtaka yasipelekwe nje ya nchi, hivi kila kitu tunawategemea Wazungu kwa sababu gani hasa?”

Utaratibu wa mashtaka
Kwa mujibu wa Mahakama hiyo, nchi mwanachama au Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ndiyo wanaoweza kuelezea hali ya uhalifu ndani ya mipaka ya Mahakama hiyo na maelezo hayo hupelekwa kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC.
 
Mwendesha mashtaka mkuu atayapitia na kuanza uchunguzi isipokuwa pale tu atakapoona kuwa hakuna haja ya uchunguzi kwa maana ya kuwa kuna ushahidi wa kutosha juu ya uhalifu husika.

Uchunguzi wa mwendesha mashtaka utahusisha taarifa zote na ushahidi unaotakiwa kutathmini uhalifu unaotajwa huku ukizingatia haki zote za anayetuhumiwa.

Katika kipindi chote cha uchunguzi, mwendesha mashtaka atakuwa akitoa taarifa anazopata kwa Baraza la Awali la Mahakama (Pre-Trial Chamber) ambalo litakuwa na wajibu kwa maelekezo ya mwendesha mashtaka mkuu kutoa hati ya kukamatwa kwa wahusika au hati ya kuitwa mahakamani hapo. Mtuhumiwa anapofika mahakamani hapo, husomewa mashtaka yake ambayo yatakuwa msingi wa kesi nzima.

Baada ya kuthibitishwa kwa mashtaka, kesi hiyo itasikilizwa na Baraza la Awali la Mahakama chini ya majaji watatu na kutoa uamuzi wake wa ama kuwaachia au kuwatia hatiani watuhumiwa.

Tayari ICC imeshawapandisha kizimbani wanasiasa maarufu wa Kenya kutokana na kutuhumiwa kuhusika kuchochea vurugu za uchaguzi nchini Kenya mwaka 2008 ambazo zilisababisha vifo vya watu 1,133.

Wanasiasa hao ni Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta, Mbunge wa Eldoret Kaskazini, William Ruto, aliyekuwa Mkuu wa utumishi, Francis Muthaura na Mtangazaji wa Redio ya Kass FM, Joshua Sang.
Chanzo:Mwananchi

Thursday, October 11, 2012

Lowassa hashikiki

Best Blogger Tips
 WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa amezidi kuwatimulia vumbi wapinzani wake ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kutokana na wajumbe wanaounga mkono kambi yake kuzidi kupeta katika uchaguzi.

Katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha uliomalizika jana, kambi mbili zinazowaunga mkono Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe katika mbio za urais 2015, zilionekana kutifuana vikali.

Msuguano huo ulianza kujitokeza tangu juzi kwenye uchaguzi wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa huo, ambapo juhudi za Katibu wa Mkoa, Mary Chatanda kutaka kuihujumu kambi ya Lowassa, ziligonga mwamba na kunusurika kipigo.

Chatanda ambaye alikuwa akifanya juhudi za kuhakikisha mshindi anakuwa Dk. Harold Adamson, aliambulia patupu baada ya Robinson Meitinyiku anayedaiwa kuungwa mkono na Lowassa, kushinda kwa kura 247 dhidi ya 188 za mpinzani wake.

Katika mwendelezo huo huo wa msuguano wa kambi hizo mbil, jana Katibu huyo CCM Mkoa wa Arusha, Chatanda, alijikuta akiaibishwa na wajumbe wa mkutano Mkuu wa chama baada ya kujifanya amesahau kumtambulisha Lowassa.

Chatanda aliufanya ukumbi mzima kupiga kelele kubwa wakisema bado! bado! Bado Eddo! Eddo! Eddo! Na ndipo kwa aibu kubwa, katibu huyo akameza mate na kumtambulisha Lowassa.

Hata hivyo, hatua hiyo ilitafsiriwa tofauti na baadhi ya wajumbe ambapo wengine walisema ni tukio la bahati mbaya, lakini wengi wao wakidai kuwa Chatanda alifanya makusudi kutokana na kundi analoliunga mkono kuanguka kwenye uchaguzi wa UVCCM.

Katika mkutano huo mkuu wa mkoa uliohudhuriwa na wajumbe 833, nafasi ya Mwenyekiti ilirudi tena kwa Onesmo ole Nangole ambaye anadaiwa kuunga mkono na Lowassa, akiwaacha kwa mbali washindani wake wawili.

Nangole alijizolea kura 604 huku akifuatiwa kwa mbali na Adam Choro wakati Dk. Salash Toure aliyedondoshwa na Lowassa kwenye uchaguzi wa ujumbe wa NEC Taifa kupitia wilayani Monduli akiambulia kura 13.

Akitangaza matokeo hayo, msaimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, alisema kura zilizopigwa ni 833 ambapo kura halali zilikuwa 830 na tatu ziliharibika.
Mapema akifungua mkutano huo kabla ya uchaguzi, Prof. Maghembe, aliwataka wajumbe kuacha kuzomea au kushangilia wagombea pindi watakapofika mbele yao kujinadi.

Alisema lengo la uchaguzi huo ni kupata viongozi watakaojenga chama kwa kuhakikisha wanavunja makundi na kuwaunganisha wanachama wote ili kuvirejesha viti vya udiwani na ubunge walivyovipoteza mkoani humo.

“Msichague viongozi watakaobweteka na kutugawa, hawa hawatufai, tuepuke viongozi wa aina hii, tuchague watakaokisaidia chama,” alisema Maghembe.

Naye Lowassa, akizungumza baada ya kuchaguliwa na wajumbe kuwa mwenyekiti wa muda wa mkutano huo, aliwashukuru wote kwa imani waliyompa huku akishangiliwa kwa kishindo.

“Wajumbe nimewaelewa na sitawaangusha, nimewaelewa ndugu zangu sitawaangusha, nawashukuru kwa kunishangilia, ila sasa tusishangilie tusije kuharibu utaratibu,” alisema Lowassa.

Akijinadi kwa wajumbe hao, Nangole aliwaomba wamchague ili aweze kusimamia dosari zilizopo na kushughulika na watu wote wanaoleta makundi ndani ya chama kwa mgawanyiko kuanzia wilayani mpaka Mkoa.

Naye Dk. Toure, aliwaomba wajumbe hao kuwa akichaguliwa, atamaliza makundi yaliyopo ambayo yamekiathiri chama hicho kwani wanachama wamegawanyika kila ngazi na kuwasihi wawabwage wagombea waliotumia fedha kuomba kura kwenye uchaguzi huo.

Mgawanyiko ndani ya chama ulionekana kuzungumzwa na kila mtu kwani hata Chora, naye aliwaomba wajumbe wamchague ili tatizo hilo alilodai kuwa limewapotezea majimbo.
Chanzo: Tanzania Daima

Wednesday, October 10, 2012

Ripoti ya Mwangosi yazua mazito

Best Blogger Tips
KAMATI  iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi kuchunguza kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi imeweka hadharani ripoti yake inayoeleza madudu yaliyofanywa na pande zote; polisi na Chadema na kusababisha mauaji hayo.

Wakati hayo yakibainika katika ripoti ya Kamati ya Waziri Nchimbi, Baraza la Habari Tanzania (MCT) nalo limeanika ripoti yake kuhusu kifo hicho. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mauaji hayo, yalitokana na uhasama uliopo baina ya polisi mkoani Iringa na waandishi wa habari wa mkoa huo.

Kamati hizo ziliundwa kwa nyakati tofauti kutokana na vurugu zilizotokea Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho.

Wajumbe katika kamati ya Nchimbi ni Mwenyekiti Jaji Steven Ihema, Makamu Mwenyekiti, Theophil Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike.

Wengine ni Ofisa aliyesomea masuala ya milipuko kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kanali Wema W. Wapo pamoja na Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Isaya Ngulu.

Kamati ya MCT ilikuwa ikiongozwa na John Mirenyi kutoka MCT, Hawra Shamte kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Simon Berege.

Ripoti ya Nchimbi

Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imesema nguvu iliyotumika na polisi kuwatawanya wafuasi wa Chadema siku ya tukio, ni kubwa na bomu lililomuua Mwangosi, lilipigwa kutoka umbali mdogo badala ya mita 80 zinazotakiwa kitaalamu, tena bila kumwelekezea mtu.

Imesema utaratibu wa matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45 na umbali wa mita 80 mpaka mita 100.

"Hakukuwa na umuhimu wa kutumia bomu hilo kwa sababu hata ingekuwa kwa sababu ya kuwakamata watu, tayari askari polisi wapatao sita walikuwapo eneo la tukio walitosha kwani operesheni haikuwa kubwa," imesema ripoti hiyo iliyokuwa ikisomwa na Jaji Ihema.

Jaji Ihema alisema kamati imependekeza nafasi za wakuu wa wilaya na mikoa ziangaliwe upya kwa kuwa zinatumika kisiasa.

Hata hiyo, Jaji Ihema alisema kinachozungumzwa kuhusu ripoti hiyo ni muhtasari tu wa ripoti nzima na wamefanya hivyo kuepuka kugusa mambo mengine ambayo yataingilia mwenendo wa kesi iliyopo mahakamani.

Hata hivyo, akaeleza kuwa ripoti nzima inayoelezea kitu kilichotokea anaijua Dk Nchimbi ambaye ndiye aliyeunda kamati hiyo.

Jaji Ihema alieleza kuwa kamati yake ilipewa hadidu sita za rejea ambazo ni kuangalia kama mkusanyiko wa Chadema ulikuwa halali na kama kulikuwa hakuna uvunjifu wa amani.

“Pia kuangalia kama nguvu iliyotumiwa na polisi ilikuwa sawa, mazingira yaliyosababisha polisi kutumia nguvu na kusababisha mauaji ya Mwangosi, kama kuna uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa,” alisema Jaji Ihema na kuongeza;

“Kuangalia kanuni na taratibu za polisi kuzuia mikutano ya siasa na uhusiano wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa.”

Chadema nao walikuwa tatizo

Jaji Ihema alisema Chadema ndiyo chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani kijijini Nyololo hasa kutokana na uamuzi wa kung’ang’ania kukusanyika isivyo halali eneo hilo.

"Ikizingatiwa kuwepo kwa ujumbe wa SMS kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho Dk Willibrod Slaa uliosema, “IGP nasubiri simu yako. Wajulishe Polisi wako waandae risasi za kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya Hague. Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya,” alisema Jaji Ihema na kuendelea.

“Ujumbe huu ukiashiria umwagaji wa damu ni ushaidi tosha kuwepo kwa uvunjifu wa amani.”

Polisi tatizo

Alisema kuhusu nguvu iliyotumika na polisi, kamati imebaini kuwa ilikuwa ni kubwa kutokana na maelezo ya viongozi wa kijijini hapo.

“Mwangosi aliuawa wakati amri ya askari kuondoka kwenye eneo la tukio ilishatolewa,” alisema Jaji Ihema na kuongeza;.

"Kamati imebaini kuwa ushirikiano wa polisi na waandishi wa habari mkoani Iringa si mzuri hivyo ikapendekeza uangaliwe." Pia uhusiano kati ya polisi na baadhi ya vyama vya siasa hauridhishi, hivyo ni muhimu kukawa na jukwaa la kushughilikia hali hiyo, alisema Jaji Ihema.

Mapendekezo

Alisema kamati imeshauri kuwa sheria zinazotoa mamlaka za kuchunguza matukio ya vifo kwenye mkusanyiko ziangaliwe kwa kuwa lililotokea Nyololo lina ushahidi wa kutosha.

Jaji Ihema alisema kwa kuwa Jeshi la Polisi litabaki kuwa mlinzi wa wananchi, siasa za ubabe na uhasama ziachwe.

Aliendelea kusema kuwa kamati inapendekeza utulivu uendelee kuwepo ili kuweza kuondoa purukushani na pia viongozi waelimishwe juu ya  umuhimu wa kutii sheria.

“Kuwepo na programu mahususi ya uzalendo na kukuza maadili, elimu ya uraia iimarishwe  na mafunzo ya JKT yarudishwe mapema,” alisema.

Mapendekezo mengine ni kuboresha ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa kuanzisha ofisi wilayani na mikoani kwa kuwa imelemewa

“Kwa upande wa vyama vya siasa viongozi wajifunze kuwa wavumilivu na kutii sheria,” alisema Jaji Ihema.

Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Daud Mwangosi kabla.

Ripoti ya MCT

Ripoti ya Timu Maalumu iliyoundwa na MCT na TEF, kuchunguza tukio hilo imesema mauaji hayo yalifanywa makusudi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi wa Iringa, Michael Kamuhanda.

“Matokeo ya uchunguzi ya mazingira yaliyopelekea mauaji ya Daudi Mwangosi, awali ya yote umethibitisha polisi kwa makusudi kabisa waliwashughulikia waandishi wa habari wa Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za Chadema katika Kijiji cha Nyololo,” inasema na kuongeza:

“Pia  Daudi Mwangosi aliuawa mikononi mwa polisi chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda. Matokeo haya yanathibitishwa na maelezo pamoja na ushahidi uliokusanywa kwa kutumia picha za video na ushahidi mwingine muhimu wa taarifa za vyombo vya habari.”

Katibu wa MCT, Kajubi Mukajanga aliyesoma ripoti hiyo alisema kuwa utafiti huo ulibaini kuwa taarifa za mauaji wa Mwangosi zimekuwa zikikinzana kuanzia hatua za awali jitihada za kuficha ukweli zilipojidhihirisha.

Ikifafanua juu ya uhusiano mbaya kati ya viongozi wa Serikali ya  Mkoa huo na Jeshi la Polisi dhidi ya waandishi, ilisema  baadhi ya waandishi waliwahi kupigwa na kuharibiwa vyombo vyao vya kazi.

“Novemba 2011, mwandishi Laurent Mkumbata anayefanya kazi ITV, alipigwa vibaya na kamera yake ilivunjwa kwa makusudi na aliyekuwa Mkuu wa Polisi (OCD) wa Iringa Mohamed Semunyu wakati akiwa kazini,” ilisema:

“Waandishi wa habari wa Iringa pia, walitendewa vibaya na viongozi wa mkoa wakati wa ziara ya Makamu wa Rais mwishoni mwa Februari 2011. Waandishi katika ziara hiyo walilazimika kulala kwenye basi walilosafiria kutokana na viongozi kupuuza kuwapatia hoteli ya kulala.”

Kwa mujibu wa Mukajanga, Machi sita mwaka huu, polisi mkoani Iringa waliwapa Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa (IPC), kibali cha kufanya maandamano ya amani kulalamikia kukua kwa uhusiano usio mzuri kati ya waandishi wa habari na viongozi wa mkoa.

Mukajanga alisema tukio hilo waliwalenga zaidi waandishi wa Iringa ambao walikuwa wanawafahamu zaidi na kuwaacha wale waliotoka  Dar es Salaam.

Kabla ya kusomwa kwa ripoti hiyo, Mukajanga alitahadharisha juu ya tabia aliyosema imeibuka ya watu kufungwa midomo kwa kisingizio cha kuwa kesi ipo mahakamani.

Alisema kwamba, ana imani kuwa mahakimu na majaji nchini, ni watu wenye sifa ambao wanaweza kufanya shughuli zao kwa kuzingatia ushahidi unaotolewa mahakamani bila ya kuathiriwa na maneno ya mitaani. 
Chanzo: Mwananchi

Tuesday, October 9, 2012

Mzee Mwinyi aibiwa sh milioni 37/-

Best Blogger Tips
 RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi, ameibiwa sh milioni 37.4 na hivyo kulazimika kupanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutoa ushahidi wake.

Kwa hatua hiyo, Mzee Mwinyi anafuata nyayo za Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliyepanda kizimbani hivi karibuni kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin.

Mzee Mwinyi ambaye alipanda kizimbani jana, anadai kuibiwa sh 37,440,000 na Abdallah Nassoro Mzombe (39) ambaye ni wakala wake.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Genivitus Dudu, mshtakiwa huyo, mkazi wa Kinondoni Mkwajuni, anashtakiwa kwa makosa ya kumuibia Mzee Mwinyi kiasi hicho cha kodi ya pango ya nyumba mbili zinazomilikiwa na Rais huyo mstaafu.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ambayo Tanzania Daima Jumatano ina nakala yake, Mzombe anadaiwa kufanya makosa hayo kinyume na kifungu cha 258 na 273 (b) (e) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya Sura ya 16 ya mwaka 2002.

Siku hiyo ya Agosti 21, mwaka huu, ilidaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai 2012 huko Mikocheni, Mzombe akiwa wakala wa Rais huyo mstaafu, alimwibia sh 17,640,000 ambazo ni pato la kodi ya nyumba yake iliyoko eneo la Mikocheni, wilaya ya Kinondoni.

Iliendelea kudai kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho Mzombe alimwibia Rais Mwinyi kilikuwa ni kodi ya pango la nyumba namba 481, iliyoko kwenye ploti A huko Mikocheni ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013.

Aidha anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai 10, mwaka huu huko Msasani Village wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa huyo alimwibia tena Rais huyo mstaafu sh 19,800,000 ambazo zilikuwa ni kodi ya nyumba namba 55 iliyoko kwenye Kitalu C .

Kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni kodi ya pango la nyumba hiyo la mwaka 2011/2012 na 2012/2013.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alikana mashtaka yote na yuko rumande hadi Oktoba 22 kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Rais Mwinyi jana alitua katika mahakama hiyo huku akiongozwa na maofisa Usalama wa Taifa (TISS) kuja kutoa ushahidi katika kesi hiyo ya jinai Na. 201/2012 iliyofunguliwa na serikali dhidi ya wakala wa Mwinyi, Abdallah Nassoro Mzombe (39).

Kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, Mwinyi alihifadhiwa kwa muda kwenye chumba namba moja cha mahakama hiyo ili kutoa muda kwa wakili wa serikali, Charles Anindo, kumuandaa.

Waandishi wa habari waliokuwepo mahakamani hapo kwa ajili ya kuripoti kesi hiyo, walizuiliwa kuingia, jambo ambalo lililalamikiwa vikali na wana habari hao.

“Msiingie humu ndani haiwahusu,” alisema ofisa habari mmoja, akiwazuia waandishi kuingia ndani ya mahakama hiyo.
Mzee Mwinyi aliondoka katika viwanja vya mahakama hiyo majira ya saa 6:21 mchana na kisha kupanda gari aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili T 914 BJT.

Hati ya mashtaka ya kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Agosti 21 mwaka huu.

Mei 7 mwaka huu Rais Mkapa alifika mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Elvin Mugeta, kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, na Grace Martin. Mahalu aliachiwa huru katika kesi hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima

Sunday, October 7, 2012

Sumaye: Lowassa hawezi kunizuia kugombea urais

Best Blogger Tips
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema endapo ataamua kugombea urais, hata kama jina la Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa litakuwepo haitamsumbua kwa kuwa hatafanya hivyo kwa ajili ya mtu yeyote, bali Watanzania.

Vilevile, amesema kuanguka kwake katika nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kupitia Wilaya ya Hanang', kumempa nguvu zaidi na kwamba hakujamdhoofisha kama baadhi ya watu wanavyodhani.

Sumaye aliangushwa katika nafasi hiyo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu(Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sumaye pia alikana kukutana na viongozi wa Chadema kujadili hatima yake ya kisiasa baada ya uchaguzi huo... “Kama ningekuwa nimekutana na viongozi wa chama hicho ningesema kwa kuwa hata wengine wanaoutafuta urais kwa udi na uvumba huwa wanakutana nao,” alisema Sumaye bila kufafanua.

Hivi karibuni, mjumbe mmoja wa Kamati Kuu ya Chadema, alikaririwa akidai kwamba Sumaye alikutana na viongozi wa chama hicho mara baada ya kuangushwa na Nagu.

Jana, Sumaye alisema kwamba atabaki kuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na kwamba hayuko katika chama hicho kwa ajili ya cheo.

Hata hivyo alitoa angalizo kuhusu upinzani akisema: “Nadhani tufikie kwenye ustaarabu kuwa vyama vya upinzani siyo maadui wala viongozi wao siyo maadui wa viongozi wa CCM.”
Alisema kukosa kwake nafasi ya Nec hakumnyimi usingizi na wala hajawahi kufikiria kukihama chama hicho kwa sababu hiyo.

“Hakuninyimi usingizi na hakusababishi au kunizuia kugombea urais kama nikiamua. Sijatangaza kugombea urais, nikiamua kugombea nitapita humohumo CCM kwa kuwa kuangushwa Hanang’ hakujanisumbua kabisa.”

Alisema hana uhasama na Lowassa na kwamba hajawahi kusema kwamba atapambana naye wala kumtangazia vita. Alisisitiza kwamba endapo atachukua uamuzi wa kugombea nafasi hiyo kuu ya uongozi nchini, haitakuwa kwa ajili ya mtu yeyote, bali Watanzania.

“Kama nikiamua kugombea, hata kuwe na wagombea 20 au agombee Lowassa, nikiamua kugombea nitagombea,” alisema Sumaye.

Uchaguzi ulijaa rushwa
Akizungumzia uchaguzi huo wa ndani wa CCM, Sumaye alisema yaliyotokea Hanang’ yametokea maeneo mengi nchini na kwamba uchaguzi unaoendelea umegubikwa na rushwa.

Hata hivyo, alisema hatakata rufaa wala kupeleka malalamiko popote kwa kuwa yaliyokuwa yakitendeka yanafahamika.

Alisema uchaguzi huo licha ya kutawaliwa na rushwa ulijaa vitendo vingi viovu vikiwemo, vitisho na uharamia wa kuhamisha wapiga kura usiku.

Alisema pia kulikuwepo rushwa ya kimtandao na kwamba hajui fedha zilizokuwa zikitolewa kama rushwa kwa wajumbe ni nani aliyekuwa akizitoa.

“Uchaguzi ulikuwa kivumbi kwelikweli, hivi sasa hapa nchini inaonekana ni vigumu kushinda uchaguzi bila kutoa rushwa.”

Alisema watu wanatoa rushwa ya kimtandao kuhakikisha wapambe wao wanachaguliwa katika nafasi mbalimbali nchini ili kujiwekea wawakilishi kwa ajili ya faida yao ya baadaye.
“Viongozi wa aina hii hufanya kazi kwa manufaa ya wale waliowapa fedha na si kwa manufaa ya wananchi,” alisema Sumaye.

Alisema hazungumzii rushwa kwa kuwa ameshindwa nafasi ya Nec Hanang’, bali hayo ni mapambano yake ya muda mrefu katika kuhakikisha rushwa inatokomea.
Alisema tatizo la rushwa si la ndani ya CCM pekee, bali ni la nchi nzima akisema viongozi wanatoa rushwa ili wapate nafasi kitu ambacho si sawa.

“Kiongozi mtoa rushwa ni mali ya watu fulani na hawezi kutenda haki akiwa madarakani, kazi yake itakuwa ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuwahonga tena wapiga kura ili arudi madarakani,” alisema Sumaye na kuongeza:
“Rushwa ni adui wa haki na ni tatizo kubwa nchini kwetu hivyo lazima tulikatae tatizo hilo.”
Huku akitanabahisha kwamba anayoyasema siyo mazuri kwa baadhi ya watu, Sumaye alisema ni muhimu amani ya nchi ikalindwa isichafuke kutokana na uroho wa madaraka.

Sumaye alisema ana imani na CCM, lakini kilichopo ni kwamba bado chama hicho hakijasimama vya kutosha kukabiliana na tatizo la rushwa.

“CCM kama chama hakina tatizo, bali kuna maeneo kadhaa ya kurekebisha ili kiweze kubadilika kwa kuwa kina uwezo huo,” alisema Sumaye.
Alisema endapo mtu ataona kuna tatizo katika chama jibu lake ni kujitoa, hiyo itakuwa ni tatizo la mtu kwa kuwa anakohamia anaweza kukuta nako kuna tatizo ikawa tatizo ni kuhama hama.

“Nitapigana na rushwa labda ifike sehemu nichoke niamue kutoka na kuwa mwananchi wa kawaida au kwenda sehemu nyingine kwani mapambano dhidi ya rushwa ni ya kudumu kwangu na nitaendelea nayo popote nitakapokuwepo,” alisema na kuongeza: “Kama mtu ana mambo mabaya katika chama ni lazima aadhibiwe na aadabishwe na ndiyo maana mwenyekiti wetu aliposema watu wajivue gamba nilifurahi. Ni bora CCM tukajirekebisha kabla watu hawajasema sasa basi.”
Chanzo: Mwananchi

Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits