KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi
kuchunguza kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, Daud
Mwangosi imeweka hadharani ripoti yake inayoeleza madudu yaliyofanywa na
pande zote; polisi na Chadema na kusababisha mauaji hayo.
Wakati
hayo yakibainika katika ripoti ya Kamati ya Waziri Nchimbi, Baraza la
Habari Tanzania (MCT) nalo limeanika ripoti yake kuhusu kifo hicho.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mauaji hayo, yalitokana na uhasama uliopo
baina ya polisi mkoani Iringa na waandishi wa habari wa mkoa huo.
Kamati
hizo ziliundwa kwa nyakati tofauti kutokana na vurugu zilizotokea
Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi
wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa
wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho.
Wajumbe
katika kamati ya Nchimbi ni Mwenyekiti Jaji Steven Ihema, Makamu
Mwenyekiti, Theophil Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania
(MCT), Pili Mtambalike.
Wengine ni Ofisa aliyesomea masuala ya
milipuko kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kanali Wema W. Wapo
pamoja na Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Isaya Ngulu.
Kamati
ya MCT ilikuwa ikiongozwa na John Mirenyi kutoka MCT, Hawra Shamte
kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Tumaini Iringa, Simon Berege.
Ripoti ya Nchimbi
Pamoja na
mambo mengine ripoti hiyo imesema nguvu iliyotumika na polisi
kuwatawanya wafuasi wa Chadema siku ya tukio, ni kubwa na bomu
lililomuua Mwangosi, lilipigwa kutoka umbali mdogo badala ya mita 80
zinazotakiwa kitaalamu, tena bila kumwelekezea mtu.
Imesema utaratibu wa matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45 na umbali wa mita 80 mpaka mita 100.
"Hakukuwa
na umuhimu wa kutumia bomu hilo kwa sababu hata ingekuwa kwa sababu ya
kuwakamata watu, tayari askari polisi wapatao sita walikuwapo eneo la
tukio walitosha kwani operesheni haikuwa kubwa," imesema ripoti hiyo
iliyokuwa ikisomwa na Jaji Ihema.
Jaji Ihema alisema kamati imependekeza nafasi za wakuu wa wilaya na mikoa ziangaliwe upya kwa kuwa zinatumika kisiasa.
Hata
hiyo, Jaji Ihema alisema kinachozungumzwa kuhusu ripoti hiyo ni
muhtasari tu wa ripoti nzima na wamefanya hivyo kuepuka kugusa mambo
mengine ambayo yataingilia mwenendo wa kesi iliyopo mahakamani.
Hata hivyo, akaeleza kuwa ripoti nzima inayoelezea kitu kilichotokea anaijua Dk Nchimbi ambaye ndiye aliyeunda kamati hiyo.
Jaji
Ihema alieleza kuwa kamati yake ilipewa hadidu sita za rejea ambazo ni
kuangalia kama mkusanyiko wa Chadema ulikuwa halali na kama kulikuwa
hakuna uvunjifu wa amani.
“Pia kuangalia kama nguvu iliyotumiwa
na polisi ilikuwa sawa, mazingira yaliyosababisha polisi kutumia nguvu
na kusababisha mauaji ya Mwangosi, kama kuna uhasama kati ya polisi na
waandishi Iringa,” alisema Jaji Ihema na kuongeza;
“Kuangalia kanuni na taratibu za polisi kuzuia mikutano ya siasa na uhusiano wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa.”
Chadema nao walikuwa tatizo
Jaji
Ihema alisema Chadema ndiyo chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani
kijijini Nyololo hasa kutokana na uamuzi wa kung’ang’ania kukusanyika
isivyo halali eneo hilo.
"Ikizingatiwa kuwepo kwa ujumbe wa SMS
kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho Dk Willibrod Slaa uliosema, “IGP
nasubiri simu yako. Wajulishe Polisi wako waandae risasi za kutosha,
mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha kusherehekea,
mjiandae kwa kwenda mahakama ya Hague. Ni afadhali tufe kuliko
manyanyaso haya,” alisema Jaji Ihema na kuendelea.
“Ujumbe huu ukiashiria umwagaji wa damu ni ushaidi tosha kuwepo kwa uvunjifu wa amani.”
Polisi tatizo
Alisema
kuhusu nguvu iliyotumika na polisi, kamati imebaini kuwa ilikuwa ni
kubwa kutokana na maelezo ya viongozi wa kijijini hapo.
“Mwangosi aliuawa wakati amri ya askari kuondoka kwenye eneo la tukio ilishatolewa,” alisema Jaji Ihema na kuongeza;.
"Kamati
imebaini kuwa ushirikiano wa polisi na waandishi wa habari mkoani
Iringa si mzuri hivyo ikapendekeza uangaliwe." Pia uhusiano kati ya
polisi na baadhi ya vyama vya siasa hauridhishi, hivyo ni muhimu kukawa
na jukwaa la kushughilikia hali hiyo, alisema Jaji Ihema.
Mapendekezo
Alisema
kamati imeshauri kuwa sheria zinazotoa mamlaka za kuchunguza matukio ya
vifo kwenye mkusanyiko ziangaliwe kwa kuwa lililotokea Nyololo lina
ushahidi wa kutosha.
Jaji Ihema alisema kwa kuwa Jeshi la Polisi litabaki kuwa mlinzi wa wananchi, siasa za ubabe na uhasama ziachwe.
Aliendelea
kusema kuwa kamati inapendekeza utulivu uendelee kuwepo ili kuweza
kuondoa purukushani na pia viongozi waelimishwe juu ya umuhimu wa kutii
sheria.
“Kuwepo na programu mahususi ya uzalendo na kukuza
maadili, elimu ya uraia iimarishwe na mafunzo ya JKT yarudishwe
mapema,” alisema.
Mapendekezo mengine ni kuboresha ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa kuanzisha ofisi wilayani na mikoani kwa kuwa imelemewa
“Kwa upande wa vyama vya siasa viongozi wajifunze kuwa wavumilivu na kutii sheria,” alisema Jaji Ihema.
Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Daud Mwangosi kabla.
Ripoti ya MCT
Ripoti
ya Timu Maalumu iliyoundwa na MCT na TEF, kuchunguza tukio hilo imesema
mauaji hayo yalifanywa makusudi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi
wa Iringa, Michael Kamuhanda.
“Matokeo ya uchunguzi ya mazingira
yaliyopelekea mauaji ya Daudi Mwangosi, awali ya yote umethibitisha
polisi kwa makusudi kabisa waliwashughulikia waandishi wa habari wa
Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za Chadema katika Kijiji
cha Nyololo,” inasema na kuongeza:
“Pia Daudi Mwangosi aliuawa
mikononi mwa polisi chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa RPC Michael
Kamuhanda. Matokeo haya yanathibitishwa na maelezo pamoja na ushahidi
uliokusanywa kwa kutumia picha za video na ushahidi mwingine muhimu wa
taarifa za vyombo vya habari.”
Katibu wa MCT, Kajubi Mukajanga
aliyesoma ripoti hiyo alisema kuwa utafiti huo ulibaini kuwa taarifa za
mauaji wa Mwangosi zimekuwa zikikinzana kuanzia hatua za awali jitihada
za kuficha ukweli zilipojidhihirisha.
Ikifafanua juu ya uhusiano
mbaya kati ya viongozi wa Serikali ya Mkoa huo na Jeshi la Polisi dhidi
ya waandishi, ilisema baadhi ya waandishi waliwahi kupigwa na
kuharibiwa vyombo vyao vya kazi.
“Novemba 2011, mwandishi Laurent
Mkumbata anayefanya kazi ITV, alipigwa vibaya na kamera yake ilivunjwa
kwa makusudi na aliyekuwa Mkuu wa Polisi (OCD) wa Iringa Mohamed Semunyu
wakati akiwa kazini,” ilisema:
“Waandishi wa habari wa Iringa
pia, walitendewa vibaya na viongozi wa mkoa wakati wa ziara ya Makamu wa
Rais mwishoni mwa Februari 2011. Waandishi katika ziara hiyo
walilazimika kulala kwenye basi walilosafiria kutokana na viongozi
kupuuza kuwapatia hoteli ya kulala.”
Kwa mujibu wa Mukajanga,
Machi sita mwaka huu, polisi mkoani Iringa waliwapa Klabu ya Waandishi
wa Habari Iringa (IPC), kibali cha kufanya maandamano ya amani
kulalamikia kukua kwa uhusiano usio mzuri kati ya waandishi wa habari na
viongozi wa mkoa.
Mukajanga alisema tukio hilo waliwalenga zaidi
waandishi wa Iringa ambao walikuwa wanawafahamu zaidi na kuwaacha wale
waliotoka Dar es Salaam.
Kabla ya kusomwa kwa ripoti hiyo,
Mukajanga alitahadharisha juu ya tabia aliyosema imeibuka ya watu
kufungwa midomo kwa kisingizio cha kuwa kesi ipo mahakamani.
Alisema
kwamba, ana imani kuwa mahakimu na majaji nchini, ni watu wenye sifa
ambao wanaweza kufanya shughuli zao kwa kuzingatia ushahidi unaotolewa
mahakamani bila ya kuathiriwa na maneno ya mitaani.
Chanzo: Mwananchi
Wednesday, October 10, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment