Sunday, October 7, 2012

Sumaye: Lowassa hawezi kunizuia kugombea urais

Best Blogger Tips
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema endapo ataamua kugombea urais, hata kama jina la Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa litakuwepo haitamsumbua kwa kuwa hatafanya hivyo kwa ajili ya mtu yeyote, bali Watanzania.

Vilevile, amesema kuanguka kwake katika nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kupitia Wilaya ya Hanang', kumempa nguvu zaidi na kwamba hakujamdhoofisha kama baadhi ya watu wanavyodhani.

Sumaye aliangushwa katika nafasi hiyo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu(Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sumaye pia alikana kukutana na viongozi wa Chadema kujadili hatima yake ya kisiasa baada ya uchaguzi huo... “Kama ningekuwa nimekutana na viongozi wa chama hicho ningesema kwa kuwa hata wengine wanaoutafuta urais kwa udi na uvumba huwa wanakutana nao,” alisema Sumaye bila kufafanua.

Hivi karibuni, mjumbe mmoja wa Kamati Kuu ya Chadema, alikaririwa akidai kwamba Sumaye alikutana na viongozi wa chama hicho mara baada ya kuangushwa na Nagu.

Jana, Sumaye alisema kwamba atabaki kuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na kwamba hayuko katika chama hicho kwa ajili ya cheo.

Hata hivyo alitoa angalizo kuhusu upinzani akisema: “Nadhani tufikie kwenye ustaarabu kuwa vyama vya upinzani siyo maadui wala viongozi wao siyo maadui wa viongozi wa CCM.”
Alisema kukosa kwake nafasi ya Nec hakumnyimi usingizi na wala hajawahi kufikiria kukihama chama hicho kwa sababu hiyo.

“Hakuninyimi usingizi na hakusababishi au kunizuia kugombea urais kama nikiamua. Sijatangaza kugombea urais, nikiamua kugombea nitapita humohumo CCM kwa kuwa kuangushwa Hanang’ hakujanisumbua kabisa.”

Alisema hana uhasama na Lowassa na kwamba hajawahi kusema kwamba atapambana naye wala kumtangazia vita. Alisisitiza kwamba endapo atachukua uamuzi wa kugombea nafasi hiyo kuu ya uongozi nchini, haitakuwa kwa ajili ya mtu yeyote, bali Watanzania.

“Kama nikiamua kugombea, hata kuwe na wagombea 20 au agombee Lowassa, nikiamua kugombea nitagombea,” alisema Sumaye.

Uchaguzi ulijaa rushwa
Akizungumzia uchaguzi huo wa ndani wa CCM, Sumaye alisema yaliyotokea Hanang’ yametokea maeneo mengi nchini na kwamba uchaguzi unaoendelea umegubikwa na rushwa.

Hata hivyo, alisema hatakata rufaa wala kupeleka malalamiko popote kwa kuwa yaliyokuwa yakitendeka yanafahamika.

Alisema uchaguzi huo licha ya kutawaliwa na rushwa ulijaa vitendo vingi viovu vikiwemo, vitisho na uharamia wa kuhamisha wapiga kura usiku.

Alisema pia kulikuwepo rushwa ya kimtandao na kwamba hajui fedha zilizokuwa zikitolewa kama rushwa kwa wajumbe ni nani aliyekuwa akizitoa.

“Uchaguzi ulikuwa kivumbi kwelikweli, hivi sasa hapa nchini inaonekana ni vigumu kushinda uchaguzi bila kutoa rushwa.”

Alisema watu wanatoa rushwa ya kimtandao kuhakikisha wapambe wao wanachaguliwa katika nafasi mbalimbali nchini ili kujiwekea wawakilishi kwa ajili ya faida yao ya baadaye.
“Viongozi wa aina hii hufanya kazi kwa manufaa ya wale waliowapa fedha na si kwa manufaa ya wananchi,” alisema Sumaye.

Alisema hazungumzii rushwa kwa kuwa ameshindwa nafasi ya Nec Hanang’, bali hayo ni mapambano yake ya muda mrefu katika kuhakikisha rushwa inatokomea.
Alisema tatizo la rushwa si la ndani ya CCM pekee, bali ni la nchi nzima akisema viongozi wanatoa rushwa ili wapate nafasi kitu ambacho si sawa.

“Kiongozi mtoa rushwa ni mali ya watu fulani na hawezi kutenda haki akiwa madarakani, kazi yake itakuwa ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuwahonga tena wapiga kura ili arudi madarakani,” alisema Sumaye na kuongeza:
“Rushwa ni adui wa haki na ni tatizo kubwa nchini kwetu hivyo lazima tulikatae tatizo hilo.”
Huku akitanabahisha kwamba anayoyasema siyo mazuri kwa baadhi ya watu, Sumaye alisema ni muhimu amani ya nchi ikalindwa isichafuke kutokana na uroho wa madaraka.

Sumaye alisema ana imani na CCM, lakini kilichopo ni kwamba bado chama hicho hakijasimama vya kutosha kukabiliana na tatizo la rushwa.

“CCM kama chama hakina tatizo, bali kuna maeneo kadhaa ya kurekebisha ili kiweze kubadilika kwa kuwa kina uwezo huo,” alisema Sumaye.
Alisema endapo mtu ataona kuna tatizo katika chama jibu lake ni kujitoa, hiyo itakuwa ni tatizo la mtu kwa kuwa anakohamia anaweza kukuta nako kuna tatizo ikawa tatizo ni kuhama hama.

“Nitapigana na rushwa labda ifike sehemu nichoke niamue kutoka na kuwa mwananchi wa kawaida au kwenda sehemu nyingine kwani mapambano dhidi ya rushwa ni ya kudumu kwangu na nitaendelea nayo popote nitakapokuwepo,” alisema na kuongeza: “Kama mtu ana mambo mabaya katika chama ni lazima aadhibiwe na aadabishwe na ndiyo maana mwenyekiti wetu aliposema watu wajivue gamba nilifurahi. Ni bora CCM tukajirekebisha kabla watu hawajasema sasa basi.”
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits