Saturday, October 13, 2012

Mshtuko mauaji ya RPC Mwanza

Best Blogger Tips
 SIMANZI imegubika Jiji la Mwanza na vitongoji vyake baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (55),  kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa  manane wa kuamkia jana.Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Said Mwema alithibitisha tukio hilo akieleza kuwa amemwagiza Kamishna wa Makosa ya Jinai nchini, Robert Manumba kwenda kuchunguza mauaji hayo.

“Tunasikitishwa kwa mauaji hayo na ninawaomba Watanzania wawe watulivu wakati tukishughulikia kuwakamata watu waliohusika katika tukio hilo,” alisema IGP Mwema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Mbali ya kumuua Kamanda Barlow, wauaji hao waliokuwa wamevalia makoti yanayovaliwa na watu wa ulinzi shirikishi (Polisi Jamii), walichukua na bastola ya kamanda huyo, simu mbili za mkononi pamoja na ‘radio call’ ya Jeshi la Polisi.

Hili ni tukio la tatu kwa Ofisa wa juu wa Polisi kuuawa mkoani Mwanza. Tukio la awali lilitokea mwaka 2007, ambapo aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza, ASP Mahende aliuawa kwa kupiga risasi eneo la Bugando saa 4:00 usiku wakati akifuatilia majambazi waliokuwa wakijitayarisha kuvamia.

Mwaka 1987, Inspekta Gamba aliuawa na majambazi katikati ya Jiji la Mwanza.
Kamanda Barlow aliuawa wakati akiendesha gari lake binafsi, aina ya Toyota Hilux Double Cabin na wakati wa tukio hilo hakuwa na mlinzi wake kwa kuwa kamanda huyo alikuwa katika shughuli binafsi.

Hata hivyo, mauaji hayo yamezua hisia tofauti huku wengine wakieleza kuwa ni kifo cha bahati mbaya na kwamba, wauaji walidhani ni mwananchi wa kawaida na wengine wakisema huenda ulikuwa mpango maalumu uliolenga kumwangamiza kwa kulipiza kisasi.

Taarifa ya Mkuu wa Mkoa
Akizungumza na waandishi wa habari jana saa 2:57 asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa kifo cha Kamanda Barlow kimetokea saa 8:00 usiku katika eneo la Kitangiri, Barabara ya Kona ya Bwiru karibu na Hoteli ya Tai Five.

Alisema kuwa kamanda huyo aliuawa alipokuwa akimrejesha mmoja wa wanawake waliokuwa nao katika kikao cha maandalizi ya harusi ya ndugu yake.

Mkuu huyo wa mkoa alimtaja mwanamke huyo aliyekuwa na marehemu kuwa ni Doroth Asasia Moses ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyamagana B.

 “Marehemu alikuwa katika kikao cha harusi ya anayedaiwa kwamba ni mtoto wa dada yake, Semburi Moleto kilichofanyika katika Hoteli ya Florida, Mtaa wa Rufiji. Kikao kilipomalizika tunaambiwa majira ya kati ya saa 4 hadi 5 usiku, alimchukua mwanamke huyo kama ‘lift’ ili kumsaidia kufika nyumbani kwake,”alieleza.

Alisema kuwa alipofika nyumbani kwa mwanamke huyo aliona watu waliokuwa wakimulika tochi  waliokuwa wakilalamika kuwa wameumizwa na mwanga wa taa za gari lake.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema walipofika katika gari, aliwauliza iwapo wanamfahamu na waliposhindwa kumjibu Kamanda Barlow alichukua radio ya mawasiliano ya kipolisi ili kuwasiliana na askari wake, ndipo wauaji hao walimpiga risasi eneo la shingo na kufariki papohapo.

“Kamanda wetu inaonekana amefariki kutokana risasi hiyo, ambayo imemvunja shingo yake na imepigwa kutokea upande wa kiti cha abiria na kumpitia begani na kuingia shingoni,” alisema Ndikilo na kufafanua:

“Baada ya kumuua, watu hao walipora bastola yake, ‘radio call’ hiyo pamoja na simu zake mbili za mkononi na mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mahojiano na kusaidia upelelezi.”

Kilichomponza RPC
Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinamkariri shuhuda wa tukio hilo (Dorah) akieleza  kwamba, kilichomponza Kamanda Barlow ni kuwadharau wauaji hao baada ya kuona wamevalia vikoti vyenye rangi ya kijani vilivyokuwa na maandishi ya Polisi Jamii, alidhani kuwa na watu wa ulinzi shirikishi.

Baadhi ya maofisa wa polisi wameeleza kuamini kuwa watu hao walikuwa ni Polisi Jamii ndiko kulikomponza marehemu Barlow kwa kuwa aliamini kuwa alikuwa katika mikono salama, hali ambayo ilimfanya kutojiandaa kupambana nao.

Mwalimu Doroth
Mwalimu Doroth aliyekuwa na marehemu wakati wa tukio hilo, ambaye kwa sasa anashikiliwa kuhusiana na mauaji hayo ni mjane wa marehemu Modest Lyimo ambaye zamani alikuwa ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), aliyefariki mwaka 1997 wakati huo Kamanda Barlow akiwa na OCD wa Kituo cha Kati.

Lyimo alifariki na kumwacha Doroth akiwa na mtoto mmoja, lakini baadaye mwalimu huyo alizaa watoto wawili na mwanamume mwingine hivyo kuwa na watoto watatu (majina yanahifadhiwa kwa sasa).

Eneo la mauaji
Mwandishi wa gazeti hili alipofika nyumbani kwa Mwalimu Moses alikuta askari watatu wa jeshi la polisi wakilinda na kumkagua kila mtu aliyekuwa akiingia katika nyumba hiyo  na kutoka.

Mauaji yalivyotokea
Mmoja wa watoto wa mwalimu huyo, Kenrogers Edwin, ambaye alishuhudia tukio hilo la kuuawa kwa Kamanda Barlow, aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa siku hiyo usiku kabla ya tukio, alipigiwa simu na mama yake aliyemwarifu kuwa alikuwa amefika na kumtaka amfungulie mlango.
Edwin alisema kuwa anakumbuka pia katika maongezi ya simu mama yake alimweleza kwamba alikuwa akija na mgeni kwa ajili ya kutambua nyumbani anapoishi.

Alisema kuwa wakati akifungua geti ili gari alilokuwamo mama yake (Doroth), pamoja na mgeni wao (Kamanda Barlow) liingie ndani, aliona watu wakiwa wamezunguka gari hilo.

“Ilikuwa saa 8 usiku, nilipofungua geti ili aingie, niliona watu watatu wakiwa upande wa dereva wa gari na wawili upande mwingine aliokaa,” alisema na kuongeza:
“Niliona wakimnyang’anya mama mkoba na simu na nilisikia wakibishana, lakini baadaye nilisikia mlio wa risasi.”

Alieleza kwamba anakumbuka kuwa baada ya mlio huo wa risasi alilazimika kulala chini kwa kuogopa na kwamba baada ya Kamanda Barlow kupigwa risasi, wauaji hao walikimbia walipoona pikipiki ikija eneo hilo kwa kasi.

Aliyemhudumia  Baa
Mhudumu wa baa, Benard Kanyabukala, ambaye alimhudumia Kamanda Barlow katika kikao hicho alisema kuwa baada ya kikao hicho kumalizika, kamanda huyo aliagiza sanduku moja la bia kwa ajili ya wajumbe waliokuwapo katika kikao hicho na yeye (mhudumu) alinunuliwa kinywaji aina ya Alivaro.

“Aliomba bili na nilipompa alinifokea akidai nimemzidishia bei. Awali nilimweleza kuwa bei ya kreti ni Sh36,000, lakini kutokana na baadhi ya watu kutokunywa bia na kubadilisha vinywaji bei ilizidi na kuwa Sh40,700, ingawa baada ya kumwelewesha alilipa na kuongeza bia nyingine kwa raundi ya mwisho zenye thamani ya Sh 30,800,” alisema Kanyabukala.

Alieleza kwamba, wakati wa kikao hicho Kamanda Barlow alikuwa akinywa bia aina ya Serengeti, lakini mara ya mwisho alipoagiza vinywaji alikunywa maji ya Kilimanjaro na waliondoka hapo saa 8:30 usiku akiwa na mwanamke mmoja.

Mmiliki wa baa
Mmiliki wa baa ya Florida, kilipofanyika kikao hicho, Ritha Mosha alielezea kuwa, Kamanda Barlow alifika katika baa hiyo kwa mwaliko wa Semburi Moleto, ambaye yeye na Kamanda Barlow wote ni Wachaga waliozaliwa Kijiji cha Kiyou, Tarafa ya Vunjo Marangu, mkoani Kilimanjaro.

“Mimi ilikuwa ni mara yangu ya pili kuonana naye siku hiyo.  Kijana anayetarajia kuoa alinieleza kuwa, alimwomba Kamanda Barlow amsimamie kama mzazi wake katika arusi yake na ndiye aliyesimamia kikao hicho,  ndiyo aliyeongoza sala ya kufungua kikao hicho,” alieleza Ritha.

Alisema kuwa kikao hicho kilichelewa kuanza kutokana na wajumbe kuchelewa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jijini hapo.

Alifahamisha kuwa kikao hicho kilianza saa 2:21 usiku na kwamba kamanda huyo alikuwa msemaji wa familia.

Idadi ya wanawake
Ritha alifahamisha kuwa, kikao hicho kilitarajiwa kuwa na  wajumbe 100, lakini walifika kati ya 55 hadi 60 na kati ya hao kulikuwa na wanawake wawili ambao  aliwataja kwa majina ya Christina Mosha, mkazi wa Nyakato na Doroth ambaye alisindikizwa na kamanda huyo.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits