POLISI mkoani Dar es Salaam na wale wa Kisiwani Zanzibar, jana walitumia
mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kusambaratisha makundi ya watu
wanaodaiwa kuwa waumini wa Dini ya Kiislamu, waliopanga maandamano
kushinikiza kuachiwa kwa viongozi wao.
Kisiwani Zanzibar vurugu
kubwa ziliibuka baada ya kusambaa taarifa kuwa Kiongozi wa Kundi la
Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed alitekwa nyara juzi saa 3 usiku akiwa
kwenye gari lake na dereva wake.
Vurugu hizo zilisababisha
uharibifu wa mali kadhaa ikiwamo Maskani Kaka ya Kisonge inayomilikiwa
na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo ilichomwa moto na waandamanaji.
Waandamanaji
hao pia walichoma moto baa za Darajani na Mbawala eneo la Mikunguni na
baadhi ya nyumba za kulala wageni, kabla Vikosi vya Kutuliza Ghasia
(FFU) na Kikosi cha Zima Moto kudhibiti vurugu hizo kwa mabomu ya kutoa
machozi.
Pia magari kadhaa yalichomwa moto na kuharibiwa vibaya
yakiwa yameegeshwa katika maeneo mbalimbali, huku mipira na matairi
vikichomwa katika barabara kadhaa.
Katika maeneo ya Mjini baadhi
ya njia zilifungwa na watu waliokuwa wakitoka kazini walishindwa kwenda
nyumbani. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni yale ya Malindi, Darajani hadi
Michenzani ambako njia zilifungwa na mabomu yalisikika yakipigwa
mfululizo.
Katibu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheik Abdallah Said alisema,
“Taarifa
tulizonazo ni kwamba Sheikh Farid ametoweka katika mazingira ya
kutatanisha…Alitoka kwake Mbuyuni katika gari yeye na kijana wake wa
hapo nyumbani, lakini baadaye kuna gari ikamfuata na kusimama na ndipo
alipoingia katika hilo gari jingine na hakuonekana tena. Hatujui ni kina
nani waliomchukua na hatujui ilikuwaje akaingia katika hilo gari ...”
Polisi
waliimarisha ulinzi katika baadhi ya maeneo hasa Msikiti wa Mbuyuni
ambao uko jirani na makazi ya Sheikh Farid. Kamishna wa Polisi Zanzibar,
Mussa Ali Mussa alisema polisi halihusiki na kukamatwa kwa Farid,
lakini wao wanaamini kwamba ‘amejipoteza’ mwenyewe na kujificha.
Kamishna Mussa alisema polisi watawasaka wote waliosababisha vurugu hizo, na kwamba hadi sasa hawafahamu chanzo chake bado.
“Tunafanya
uchunguzi zaidi kujua chanzo cha fujo hizo ingawa mimi sijui habari za
kutekwa Farid, sasa tunasema tunachunguza chanzo cha vurugu hizo na
tukishapata uthibitisho na waliosababisha tutawafikisha mahakamani
kujibu mashtaka,” alisema kamishna huyo.
Ilivyokuwa Zanzibar
Vurugu
hizo zilianza katika maeneo mbalimbali muda mfupi baada ya vijana
kadhaa kukusanyika katika eneo la Darajani kando ya Soko Kuu majira ya
asubuhi, kutokana na kuzagaa kwa taarifa kwamba Sheikh Farid alikuwa
haonekani.
Idadi ya vijana hao ilikuwa ikiongezeka kadiri muda
ulivyosonga, huku wengi wao wakiwa na silaha za aina mbalimbali zikiwamo
magongo na mawe, hali iliyoibua hofu kwa wafanyabiashara wa eneo hilo,
hivyo baadhi yao waliamua kufunga maduka.
Maeneo yalioharibiwa ni
pamoja na baadhi ya nyumba za kulala wageni ambazo zimechomwa moto
katika eneo la Amani, huku baadhi ya vijana wakionekana wakikimbia na
kreti za pombe.
Katika eneo la Darajani, vijana kadhaa
wakishirikiana na Wamachinga, walionekana wakivunja kisha kuingia katika
moja ya maghala ya kuhifadhia bia, ambako walipora bidhaa zote zikiwamo
kreti kadhaa za bia zilizokuwa zimehifadhiwa humo.
Baadhi ya
wenye maduka walifunga na kutoweka, lakini waporaji waliiba baadhi ya
bidhaa vikiwamo vyakula, kisha kutokomea navyo kusikojulikana.
Katika
maeneo ya Ng’ambo ambayo ni Amani, Mikunguni, Kwerekwe na Daraja Bovu
vijana walioonekana kuwa na hamasa, waliingia kwenye makazi ya watu na
kuiba vitu kadhaa, na kila mabomu yalipopigwa walikimbilia vichochoroni
na baada ya muda walirejea tena.
Maeneo ya Malindi, Michenzani
na Rahaleo, kulikuwa na vurugu za urushaji mawe na kusababisha
uharibifu mkubwa wa miundombinu katika maeneo hayo.
Matawi ya
miti ilikatwa na kuunganishwa na magari mabovu kuwekwa barabarani kisha
kuchomwa moto. Hali hiyo ilisabababisha uharibifu mkubwa katika baadhi
ya barabara, na katika fujo hizo baadhi ya vijana walikamatwa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma Mohammed alithibitisha
kutokea kwa fujo hizo na kusema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi
kujua chanzo chake na taarifa kamili zitatolewa baada ya kukamilika
uchunguzi huo.
Ponda Dar
Jijini Dar es Salaam, baadhi ya
watu walipanga kufanya maandamano hadi Makao Makuu ya Polisi, kupinga
kukamatwa kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda
Issa Ponda aliyekamatwa juzi usiku na kushikiliwa kutwa nzima ya jana
katika Kituo Kikuu cha Polisi.
Ponda alitiwa mbaroni kwa tuhuma
za kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani jijini Dar es Salaam, na
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
alisisitiza kuwa polisi wamechoka kuvumilia harakati zake za kutaka
“nchi isitawalike”.
“Kuanzia leo uvumilivu kwa Jeshi la Polisi
dhidi ya watu wasiofuata sheria za nchi umekwisha. Kwa kuwa Ponda ni mtu
anayepotosha watu waliopo chini yake wanaotaka kuandamana bila
utaratibu wasitulaumu kwa lolote lile litakalotokea,” alisema Kova.
Kova
alisema hadi jana Ponda alikuwa bado anahojiwa katika Kituo Kikuu cha
Polisi, Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba ushahidi ukijitosheleza,
atafikishwa mahakamani wakati wowote.
Alisema taasisi anayoingoza
Sheikh Ponda haijasajiliwa kwa mujibu wa sheria kufanya shughuli za
dini. Hivyo basi shughuli zote zinazoendesha na taasisi hiyo si halali.
"Natoa
wito pia kwa wafuasi wa kiongozi huyo, walioshiriki katika vurugu
mbalimbali za hivi karibuni, wajisalimishe haraka kwa kuwa sasa tupo
katika mchakato wa kuwasaka, kuwakamata na baadaye kuwafikisha mbele ya
sheria," alisema.
Tuhuma za Ponda
Kamanda Kova alidai kuwa
Sheikh Ponda amekuwa akichochea vurugu na kuwashawishi wafuasi wake
kuidharau Serikali na vyombo vya usalama.
“Ponda amekuwa ni mtu
ambaye amefanya nchi hii, hasa katika Jiji la Dar es Salaam kukaa katika
hali ya wasiwasi. Ijumaa imekuwa siku ya fujo badala ya kuwa siku ya
amani,” alisema Kova.
Alisema vurugu hizo zinazoongozwa na Sheikh
Ponda zimekuwa zikisababisha baadhi ya watu kushindwa kwenda kazini
siku za Ijumaa na hali hiyo haivumiliki tena.
Kamanda Kova
alitaja tuhuma nyingine dhidi ya Sheikh Ponda kuwa ni kuongoza kundi la
watu kwenda kuvamia kiwanja namba 311/3/4 eneo la Chang’ombe ambacho
kinamilikiwa na kampuni Agritanza.
"Kiwanja alichokwenda
kukivamia kilikuwa mali ya Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) na
kiliuzwa kihalali kwa kampuni hiyo," alisena.
Alitaja tuhuma
nyingine kuwa ni kufanya maandamano kinyume cha sheria, ikiwamo kuweka
kambi Makao Makuu ya Polisi bila kibali cha jeshi hilo wiki kadhaa
zilizopita.
Kamanda huyo alisema Ponda anashikiliwa pia kwa kuwa
mstari wa mbele kupambana na vyombo vya dola na Serikali, ikiwa ni
pamoja na kushawishi wafuasi wake kumdharau Rais wa nchi.
“Vilevile
amekuwa akiendesha maandamano na kukusanyika Kiwanja cha Kidongo
Chekundu, huku wakijitapa kuwa wana nguvu zaidi ya Jeshi la Polisi,”
alieleza Kova.
Polisi pia wanamtuhumu Ponda kwa kuanzisha vurugu
na vitisho dhidi ya Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(Bakwata), Mufti Shaaban Bin Simba na kutaka kumtoa madarakani kwa nguvu
pamoja na kutaka kuvamia ofisi yake.
Alikamatwaje?
Kamanda
Kova alisema Ponda alikamatwa na askari waliomuwekea mtego kutokana na
yeye kuwa bingwa wa kutoroka kila akifanya matukio.
“Askari
waliowekwa maalumu kwa ajili ya kumkamata walifanikiwa kumtia nguvuni
saa 4:00 usiku karibu na eneo la maficho yake ambako alipelekwa na
pikipiki,” alisema Kova.
“Hivi Ponda ni nani mpaka awe na uwezo
wa kumpa Rais aliyechaguliwa na wananchi siku saba kuwaachia watu
waliopo mahakamani yeye amechaguliwa na nani kuongoza taasisi aliyonayo
na anatoa wapi nguvu za kufanya mambo yote hayo?,” alihoji Kova.
Alisema
kulingana na matukio anayoyaongoza Ponda, wananchi wameanza kuona kama
anaogopwa na vyombo vya dola, jambo ambalo siyo kweli.
Aliongeza
kuwa polisi wana uwezo wa kumdhibiti, isipokuwa walikuwa wanatumia
busara tangu alipoanza vurugu na kwa sasa uvumilivu umewashinda, hivyo
wataanza kumshughulikia.
Vurugu zazuka
Kukamatwa kwa Sheikh
Ponda kulizua vurugu jijini Dar es Salaam na kufanya baadhi ya wakazi
wake hasa maeneo ya Mnazi Mmoja na Kariakoo, kuingiwa kiwewe baada ya
polisi kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha ili kuwasambaratisha
watu waliokuwa wanataka kuandamana kwa lengo la kushinikiza kiongozi
huyo aachiwe.
Hali hiyo ilisababisha watu kukimbia ovyo katikati
ya iji na kuongezeka kwa misongamano ya magari, jambo lililofanya
usafiri wa daladala kuwa mgumu kwenda na kutoka katikati ya maeneo ya
Jiji la Dar es Salaam.
Baadhi ya wafanyabiashara walifunga maduka
yao wakihofia kuporwa mali wakati wa vurugu hizo, baada ya vibaka
kujichanganya wakijaribu kufanya uhalifu huo.
Katika eneo la
Mnazi Mmoja, polisi walirusha maji ya kuwasha kusambaratisha kundi la
watu hao, huku wengine wakiwa wanadhibitiwa walipokuwa wakienda Makao
Makuu ya Polisi ili kumtoa kiongozi huyo.
Baadhi ya mashuhuda
walisema, mbali na Ponda watu hao walikuwa wanataka kwenda polisi
kuwatoa watu waliokuwa wanashikiliwa kituoni hapo kwa tuhuma za kufanya
vurugu na kuharibu makanisa katika Kata ya Mbagala wilayani Temeke.
Chanzo: Mwananchi
Wednesday, October 17, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment