KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeipeleka Serikali ya
Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC),
kutokana na matukio 24 ya mauaji yanayokiuka haki za binadamu
yaliyotokea nchini kati ya Januari na Septemba mwaka huu.
Mbali na
hilo, LHRC kimepeleka taarifa hizo kwa Mjumbe Maalumu wa Umoja wa
Kimataifa, anayeshughulika na masuala ya mauaji ya raia yanayofanywa na
vyombo vya dola.
Hatua hiyo ya LHRC inatokana na ripoti tatu
zilizotolewa hivi karibuni kuchunguza kifo cha aliyekuwa Mwandishi wa
Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi
kilichotokea katika Kijiji cha Nyololo, Mkoa wa Iringa, Septemba 2 mwaka
huu.
Ripoti hizo ni ile ya Kamati ya Kuchunguza Mauaji hayo
iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi iliyokuwa
chini ya Jaji Steven Ihema; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
iliyokuwa chini ya Jaji Kiongozi Mstaafu, Amir Manento na ile ya Baraza
la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef),
iliyoongozwa na John Mirenyi.
Akizungumza na waandishi wa habari
Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba
alisema kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, jumla ya watu 24
wameuawa na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama.
“Tumepeleka
mashtaka 24 ICC tangu Septemba 28 mwaka huu, ambayo yanahitajika
kufanyiwa uchunguzi na kuchukua hatua kali dhidi ya Serikali ya Tanzania
ambayo imekuwa ikiwalinda viongozi wake wanaokiuka haki za binadamu,”
alisema Dk Bisimba.
Alisema taarifa hizo pia wamezipeleka kwenye
Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu katika kikao kinachoendelea huko
Ivory Coast, lengo likiwa ni kuchunguza na kuchukua hatua katika
Mahakama ya Afrika.
“Tunatarajia kuona uwajibikaji wa viongozi
wote wa Serikali na vyombo vya dola waliohusika kwa njia yoyote ile.
Hatua hizo au uwajibikaji huo ni pamoja na kujiuzulu, kuachishwa kazi na
kufikishwa Mahakamani, ” alisema.
Aliitaka Serikali kuacha
propaganda zinazotaka kuchochea vurugu katika taifa huku akisema
inapaswa itambue kuwa hivi sasa nchi iko katika zama za vyama vingi vya
siasa na kuacha kutumia vyombo vya dola kuleta chuki na mafarakano.
Dk
Bisimba alisema baada ya kupitia taarifa zote tatu, LHRC kimesikitishwa
na taarifa ya Kamati ya Dk Nchimbi... “LHRC hakijashangazwa sana pale
taarifa hiyo ilipoonyesha wazi nia ya kuwalinda watuhumiwa kwa kuwa
Serikali yetu bado haijajenga mfumo wa kujichunguza na kujiwajibisha
yenyewe.”
“Serikali imeudhihirishia umma kuwa haikuwa na nia ya
dhati ya kuchunguza suala la mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi,
bali ilikuwa na lengo la kulisafisha Jeshi la Polisi na kuwalinda
maofisa wake.”
Dk Bisimba alisema tangu mwaka 2001 hadi sasa,
kituo hicho kimekuwa kikifuatilia kwa karibu matukio mbalimbali ya
mauaji yanayoendelea kufanywa na vyombo vya dola na hakuna hatua
zinazochukuliwa dhidi ya wahusika.
Werema ashangaa, mawakili watofautiana
Akizungumzia
suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema hana
taarifa za Serikali kushtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya The
Hague.
“Kwa nini wameamua kutushtaki katika Mahakama ya The Hague?
Kwani hapa nchini hakuna mahakama au wameona ni bora wavuke mipaka...
Kwa sasa siwezi kulizungumzia zaidi suala hilo.”
Wakili wa
Kujitegemea, Gaudioz Ishengoma alipotakiwa kuzungumzia hilo alisema
anaunga mkono uamuzi wa kituo hicho kuipeleka Serikali kwenye Mahakama
ya Kimataifa.
Alisema hilo ndilo eneo sahihi ambalo Serikali
inatakiwa kupelekwa kwa sababu ya ukiukaji wa haki za binadamu na kwamba
huko ndiko ambako haki inaweza kupatikana.
Hata hivyo, Wakili
mwingine wa Kujitegemea, Majura Magafu alipinga hatua hiyo akisema kituo
hicho kimekosea kuipeleka Serikali The Hague kwa kuwa imekuwa ikichukua
hatua za kisheria dhidi ya makosa mbalimbali ya mauaji ambayo yamekuwa
yakitokea.
“Kwa mawazo yangu, hawa LHRC wamekosea nadhani
wamefanya hivyo kwa masilahi yao binafsi hasa ili kuonyesha kwamba
wanafanya kazi,” alisema.
Alisema hata kama Serikali itakuwa
imeshindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wauaji, kituo hicho
kilitakiwa kuishtaki Serikali katika mahakama za hapa nchini.
“Hawa
sijui wanataka kutupeleka wapi kwa sababu wananchi wengi wa Afrika
wakiwemo wa Kenya wamekuwa wakitaka mashtaka yasipelekwe nje ya nchi,
hivi kila kitu tunawategemea Wazungu kwa sababu gani hasa?”
Utaratibu wa mashtaka
Kwa
mujibu wa Mahakama hiyo, nchi mwanachama au Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa ndiyo wanaoweza kuelezea hali ya uhalifu ndani ya mipaka ya
Mahakama hiyo na maelezo hayo hupelekwa kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa
ICC.
Mwendesha mashtaka mkuu atayapitia na kuanza uchunguzi
isipokuwa pale tu atakapoona kuwa hakuna haja ya uchunguzi kwa maana ya
kuwa kuna ushahidi wa kutosha juu ya uhalifu husika.
Uchunguzi wa
mwendesha mashtaka utahusisha taarifa zote na ushahidi unaotakiwa
kutathmini uhalifu unaotajwa huku ukizingatia haki zote za
anayetuhumiwa.
Katika kipindi chote cha uchunguzi, mwendesha
mashtaka atakuwa akitoa taarifa anazopata kwa Baraza la Awali la
Mahakama (Pre-Trial Chamber) ambalo litakuwa na wajibu kwa maelekezo ya
mwendesha mashtaka mkuu kutoa hati ya kukamatwa kwa wahusika au hati ya
kuitwa mahakamani hapo. Mtuhumiwa anapofika mahakamani hapo, husomewa
mashtaka yake ambayo yatakuwa msingi wa kesi nzima.
Baada ya
kuthibitishwa kwa mashtaka, kesi hiyo itasikilizwa na Baraza la Awali la
Mahakama chini ya majaji watatu na kutoa uamuzi wake wa ama kuwaachia
au kuwatia hatiani watuhumiwa.
Tayari ICC imeshawapandisha
kizimbani wanasiasa maarufu wa Kenya kutokana na kutuhumiwa kuhusika
kuchochea vurugu za uchaguzi nchini Kenya mwaka 2008 ambazo
zilisababisha vifo vya watu 1,133.
Wanasiasa hao ni Naibu Waziri
Mkuu, Uhuru Kenyatta, Mbunge wa Eldoret Kaskazini, William Ruto,
aliyekuwa Mkuu wa utumishi, Francis Muthaura na Mtangazaji wa Redio ya
Kass FM, Joshua Sang.
Chanzo:Mwananchi
Saturday, October 13, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment