JK: Masauni kajimaliza mwenyewe
Via Mwananchi
MWENYEKITI wa CCM Rais Jakaya Kikwete, amepiga msumari wa mwisho kwa aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM Hamad Yusuph Masauni, akisema alijimaliza mwenyewe kwa kutokuwa mkweli kuhusu umri wake na watu wasitafute mchawi.
*ADAI HATUA ALIYOCHUKULIWA KAMA YA NAPE, BENNO MALISA ASEMA NI USHUJAA KUWANG’OA VIGOGO
Leon Bahati, Iringa
Kauli hiyo ya mwenyekiti wa CCM taifa ilizidi kummaliza kijana huyo ambaye tayari alijikuta katika tuhuma nzito za kughushi umri ili achaguliwe mwaka 2008.
Rais Kikwete aliweka bayana hilo mjini hapa wakati akifunga mkutano tete wa Baraza Kuu la UVCCM, ambao ulifanya vigogo wawili wa juu wote kutoka Tanzania Zanzibar, ambao ni Masauni na Naibu Katibu Mkuu Nassoro Moyo, kujiuzulu.
Mwenyekiti huyo wa CCM, awali katika hotuba yake hakutaka kuzungumzia kwa undani sakata hilo, lakini baada ya kumaliza aliruhusu maswali na ndipo baadaye akauliuza wajumbe:, "Hivi mlielezwa vizuri kilichomfanya Masauni ajiuzulu?"
Baada ya swali hilo ukumbi ulipuka kwa wajumbe kusema:, "hatujuiii...hatujuiii...hatujuiii."
Jibu hilo lilimfanya Rais kuanza kufafanua kwa kifupi na kuwambia wajumbe:, " Kilichomponza Masauni ni kutokuwa mkweli kuhusu umri wake...Alikuwa na tuhuma za kughushi umri uliomwezesha kushinda uchaguzi mwaka 2008."
"Tulipochunguza ilibainika ni kweli alighushi, wakati wa uchaguzi alisema alizaliwa mwaka 1979, lakini ukweli alizaliwa mwaka 1973 na alianza darasa la kwanza mwaka 1979."
Rais Kikwete alisisitiza:, "Kwa hiyo hakuna aliyeonewa, aliyefitini na wala watu wasitafute mchawi katika hili. Hatua kama hii ilikwishafanyika kwa watu kama akina Nape (Nnauye)." Nape naye alienguliwa katika uchaguzi wa UVCCM uliopita.
Alisema taratibu za UVCCM mtu akishakuwa na umri wa zaidi ya miaka 31, hawezi kugombea nafasi kutaka kuchaguliwa kwani anakuwa amepoteza sifa inayohusika.
Endelea kusoma habari hii..................
Wednesday, May 19, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment