Mwinyi: Sikuishutumu awamu ya nne
RAIS mstaafu wa awamu ya pili, mzee Ali Hassani Mwinyi, maarufu kama Mzee Ruksa amesema kuwa hakuikandia serikali ya awamu ya nne wala kuihusisha na kukithiri kwa rushwa kwa kuwa rushwa ilianza tangu zamani.
Mzee Ruksa alisema hayo Ijumaa iliyopita alipozungungumza na wahariri wa gazeti hili nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam kufafanua alichozungumza katika mahafali ya 12 ya Chuo cha Teknologia ya Habari (IIT) alikoalikwa kama mgeni rasmi.
Mzee Mwinyi alisisitiza kwamba; alipotangaza zama za ruksa, takribani miongo miwili iliyopita hakuruhusu rushwa iwemo katika zama hizo, lakini wajanja wachache wasiokuwa na mapenzi mema na taifa waliingiza tafsiri zao na kutumia vibaya nafasi hiyo.
"Wakati ule (alipotangaza) ruksa kwa uhakika kabisa suala rushwa halikuwa miongoni mwa mambo yaliyoingia katika azma hiyo. Wabinafsi wachache wasiokuwa na mapenzi mema na nchi hii waliitumia ruksa hiyo vibaya. Ni lazima wakomeshwe, tuseme inatosha na lazima tushinde vita hivi," alisema Mzee Ruksa.
Aliwataka Watanzania wazalendo walioshikilia nafasi zozote na popote walipo kujiunga katika mapambano dhidi ya rushwa, kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, wafikirie juu ya Watanzania wenzao walioathiriwa na umasikini na kuwasaidia kuondokana na madhila hayo.
"Kuweni wazalendo kwa mustakabali wa vizazi vijavyo. Kuweni jasiri, pigeni kelele mkiweza. Neno litakaloongoza maisha yenu liwe uadilifu," alisema Mzee Mwinyi.
Aliwataka Watanzania kuwa raia wema na wawajibikaji wanaoipenda nchi yao na walio tayari kwa njia yoyote kuijenga nchi bila kuingiza ubinafsi.
"Nina uhakika juu ya mapambano yanayoendelea dhidi ya rushwa nchini Tanzania. Kwa muda sasa wananchi wetu wamekuwa wakilalamika maafisa wa serikali kuwaomba rushwa ili maafisa hao watekeleze wajibu wao. Inaonekana utamaduni wa rushwa unaota miziz taratibu katika jamii yetu," alisema.
Endelea kusoma habari hii..............
Monday, May 24, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment