CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezindua kampeni zake za kuwania Jimbo la Igunga huku Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, akiwataka wananchi kumchagua mgombea wa chama hicho, Joseph Kashindye ili alinde rasilimali za wana Igunga.
Wakati Chadema wakizindua kampeni hizo kwa mtindo wa kumwaga tuhuma na kashfa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Rais wa Awamu ya Tatu, alitua Igunga tayari kwa uzinduzi wa kampeni za chama hicho na kuelezea furaha aliyonayo ya kusafiri kwa lami kutoka Dar es Salaam hadi Igunga.
Katika uzinduzi wa Chadema, Dk. Slaa aliwataka wananchi waliokuwa wamefurika katika Uwanja wa Sokoine mjini hapa, kumchagua Kashindye ili alinde rasilimali hizo na kupunguza aliowaita panya wanaozitafuna.
Alidai kuwa mgombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu, hawezi kuleta mabadiliko yoyote Igunga na kwa Taifa kutokana na alichoita kuwepo kwa mfumo mbovu wa CCM katika kusimamia maslahi ya wananchi.
Dk. Slaa alisema kuwa nchi inahitaji kutetewa na makamanda, ili ifanikiwe kwa kuwa CCM imeshindwa kazi ya kuwasaidia wananchi.
Aliwaambia polisi aliowaita wanaoagizwa kuwapiga mabomu wananchi, wasifanye hivyo kwa kuwa kazi ya Chadema, ni kuwatetea polisi wa vyeo vya chini ambao alidai wanapewa posho ndogo isiyokidhi mahitaji yao.
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kazi hivyo haifai kuwa madarakani wala kuongezewa wabunge kwa kuwa itazidi kuwadidimiza wananchi.
Kwa upande wake Kashindye alijinadi mbele ya wananchi hao kuwa wakiona mwalimu anaachia chaki na kwenda kwenye siasa, basi wajue hali ni mbaya kwa kuwa Taifa linahitaji ukombozi.
“Hata Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa Mwalimu Julius), aliachia chaki alipoona hali ni mbaya na akaamua kuingia kwenye siasa na kuikomboa Tanzania tunayoishi leo,” alisema.
Alidai kuwa CCM wanadhani kuwa watumishi wa Serikali ni mali yao kitu ambacho si kweli na ameamua kuingia Chadema ili awatetee wananchi wa Igunga na Taifa kwa ujumla.
“CCM ni chama kinachokufa nisingeweza kuondoka na kuingia CCM kuwa mbunge wa kusinzia kwa kuwa hawana hoja,” alidai.
Alidai kuwa fedha nyingi za kujenga barabara zimeliwa kitu ambacho kimesababisha wananchi kuteseka kutokana na mfumo mbovu wa CCM.
“Nawaombeni mnitume niende huko bungeni niende nikawe Spika ya Igunga; nikaseme yote na tupate mafanikio wote,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Susan Kiwanga alisema ni lazima Igunga wahakikishe chama hicho kinashinda kwa kumchagua Kashindye ili awatetee bungeni.
Alisema, ataweka kambi Igunga na kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kuwa Chadema ni chama cha kutetea wanyonge ambao wamekuwa wakinyonywa na CCM kwa miaka nenda rudi.
Mkapa atua Igunga Lakini Mkapa baada ya kutua Igunga, aliweka bayana kuwa amefika kupambana na kumnadi mgombea wa CCM kwa kuwa anajisikia faraja na matunda ya CCM yakiwemo kutembelea barabara ya lami kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza.
Akiwahutubia wananchi katika Kitongoji cha Makomero alisema kuwa ni muhimu kwa wana Igunga kupuuza vyama vingine kwa kuwa CCM ikitoa ahadi, inatimiza na viongozi wake ni makini.
“Kazi yetu ni moja tu, kila mtu ahakikishe Dk. Kafumu anashinda na kila mtu ambaye amejiandikisha aende kupiga kura ili mambo yawe poa,” alisema Mkapa.
Chanzo: HabariLeo
Thursday, September 8, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment