Bwana Michael Sata |
Hata hivyo, ghasia kubwa ziliripotiwa kuibuka katika Jimbo la Kaskazini mwa Zambia la Ukanda wa Shaba, kwenye ngome kuu ya Sata, kufuatia kusitishwa kwa matokeo ya awali ya uchaguzi, yaliyokuwa yakionyesha kwamba kiongozi huyo anaongoza dhidi ya Rais anayemaliza muda wake, Rupiah Banda.
Matokeo ya awali ya uchaguzi huo uliofanyika Jumanne wiki hii, yalitangazwa jana jioni na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, yakionyesha kuwa Sata alikuwa akiongoza kwa kura 639,787 dhidi ya 542,362 za Banda, ambaye ni kiongozi wa Chama cha The Movement for Multi-party Democracy (MMD) kilichotawala taifa hilo tangu 1991.
Matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia, Irene Mambilima yalikuwa ni yale yaliyokusanywa katika majimbo 85 kati ya 150.
Hatua ya kusitishwa kwa matokeo yaliyokuwa yakimpa matumaini Sata (74) maarufu kwa jina la "King Cobra" kutokana na kauli zake kali, kumezusha ghasia kubwa kutokana na kuwapo kwa hisia za wizi wa kura.
Wakati matokeo ya uchaguzi huo yakisubiriwa kwa hamu, Mahakama Kuu ya nchi hiyo imevizuia vyombo vya habari kutangaza matokeo kabla ya kutolewa na Tume ya Uchaguzi.
Amri ya Mahakama Kuu ilitolewa kufuatia ombi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zambia. Jaji wa Mahakama Kuu, Jane Kabuka, alisema wanavizuia vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha matokeo yasiyo rasmi hadi yapate idhini ya Tume ya Uchaguzi.
Katika toleo lake la juzi, gazeti binafsi la The Post lilikuwa na kichwa cha habari kuwa Satta ameshinda uchaguzi huo. Na hata baada ya pingamizi hilo la Mahakama Kuu, jana tena gazeti hilo liliandika kuwa kiongozi huyo wa upinzani anaongoza kwa 59%.
Hatua hiyo ya Mahakama Kuu imekuja huku Tume ya Uchaguzi ikisema kuwa wezi wa mitandao wameingilia mtandao wao na kuweka matokeo ya uongo yanayoonyesha kuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha Patriotic Front, Satta, anaongoza.
Msemaji wa Tume hiyo, Cris Akufuna, alisema kutokana na hitilafu hiyo maofisa wake wanafanya kazi kuhakiki zaidi ya mara mbili matokeo kutoka maeneo mbalimbali.Alisema mchakato huo umesababisha kuchelewa kutolewa kwa matokeo, hali ambayo imeanza kuzua hofu ya kwamba matokeo ya uchaguzi huo yamefanyiwa hila.
Katika maeneo kadhaa tayari washabiki wa kiongozi huyo wa upinzani wameanza kusherehekea wakiamiani kuwa kiongozi wao ameshinda.Rais Banda anatarajiwa kupata kura nyingi katika maeneo ya mikoani, ambako kuna uwezekano wa matokeo kutolewa taratibu, kuliko maeneo ambayo ni ngome ya upinzani, ambayo ni mji mkuu Lusaka na maeneo ya Ukanda wa Shaba, ambako ndiko kitovu cha uchumi wa Zambia.
Hata hivyo, kwa mujibu wa duru za habari ni mapema mno kusema iwapo Satta, yuko katika nafasi nzuri ya kushinda na kukiondoa madaraka chama tawala kwa mara ya kwanza tokea kumalizika kwa mfumo wa chama kimoja mwaka 1991.Akufuna alisema bado wanaendelea kupokea matokeo kutoka maeneo mbalimbali na kwamba mpaka itakapofika leo jioni watatangaza matokeo rasmi.
Vurugu mpaka Mbeya
Mpaka wa Zambia na Tanzania katika eneo la Tunduma mkoani Mbeya umefungwa upande wa Zambia kutokana na vurugu zinazoendelea maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Maeneo hayo ni pamoja na mji wa Nakonde katika mpaka huo upande wa Zambia, ambako magari yanadaiwa kupigwa mawe.
Habari kutoka ndani ya vyombo vya usalama Mkoa wa Mbeya zinadai kuwa katika mji huo unaopakana na Tunduma, kumezuka vurugu ambapo wananchi wa Nakonde wamekuwa wakifanya vurugu kwa kupiga mawe magari, huku polisi nao wakituliza vurugu hizo kwa kurusha mabomu ya machozi.
"Vurugu hizi zipo mpakani upande wa Zambia kwani hata wenzetu Zambia wameamua kufunga mpaka, lakini siyo kiofisi ni kienyeji kwa ajili ya kuzuia vurugu zisiweze kuvuka upande wetu wa Tanzania na kuepusha mali, yakiwamo magari kuharibiwa na vurugu hizo,"inadai taarifa hiyo.
Taarifa hizo zilisema kuwa, magari yaliyopigwa mawe ni pamoja na basi aina ya Taqwa linalofanya safari zake kutoka Tanzania kwenda Zambia na lori la mkoani Iringa la kampuni ya Asasi ambapo yalipigwa mawe yakiwa mpakani upande wa Zambia.
Aidha, kwa upande wa Tanzania katika mji wa Tunduma hakuna kinachoendelea, kwani malori yote yaliyopo Tunduma yamezuiwa kuvuka mpaka hadi hapo vurugu hizo zitakapotulia.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment