WAZIRI Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya ameitahadharisha Serikali kuwa makini
na suala la mgawo wa umeme ambao amesema unaongeza ugumu wa maisha kwa
wananchi, kwani unaweza kusababisha matatizo makubwa kiasi cha nchi
kushindwa kutawalika.“Hali ikiendelea hivi tusishangae kutokea kwa mambo
kama yaliyotokea kwa nchi za Kiarabu ambazo wananchi wake wameshindwa
kuvumilia ugumu wa maisha na kuamua kuandamana.” Msuya alitoa tahadhari
hiyo, Dar es Salaam jana wakati wa mjadala wa kitaifa kuhusu
miundombinu, nishati na madini kwenye Wiki ya Maonyesho ya Miaka 50 ya
Uhuru yaliyoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Angalizo
la Msuya inakuja kipindi ambacho nchi ipo katika mgawo wa umeme
kutokana na uhaba mkubwa wa nishati hiyo hali ambayo inaathiri sekta
mbalimbali za uzalishaji na watumiaji wa kawaida.
Msuya alikuwa
Waziri Mkuu kati ya Novemba 7, 1980 hadi Februari 24, 1983 na kushika
tena wadhifa huo Desemba, 1994. Pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha,
Viwanda katika vipindi tofauti.
Ili kukabiliana na tatizo hilo,
Serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
ilitangaza mpango wa dharura wa Sh1.2 trilioni kukabiliana na mgawo,
lakini hadi sasa hakuna mabadiliko yoyote yanayoonekana tangu
ulipoasisiwa Agosti, mwaka huu.
Kauli ya Msuya
Msuya
alisema Tanzania inahitaji uchumi unaokua na kwamba Serikali
isipoangalia, tatizo la kushindwa kukua kwa uchumi, maendeleo ya nchi
hayatafanikiwa. “Kabla ya uhuru idadi ya watu ilikuwa milioni nane na
sasa tuko zaidi ya watu 53 milioni, kuna haja ya kuwa na uchumi unaokua
badala ya kuzalisha bila mafanikio, Serikali iwe makini katika
kuimarisha mambo muhimu kama nishati,” alisema na kuongeza:
“Serikali
inatakiwa kufikiri juu ya kuimarisha masuala ya umeme nchini wakati
wawekezaji wanapoingia ili kusaidia uchumi kukua haraka na kuepusha
kutokea kwa mambo yaliyozikumba nchi za Kiarabu.” Ingawa hakuzitaja
nchi hizo, lakini Misri, Tunisia, na Yemen ndizo zilikumbwa na
maandamano kupinga hali ngumu ya kiuchumi na kusababisha viongozi wa
Misri na Tunisia na kung’olewa madarakani.
Msuya alisema Serikali
ina jukumu la kuimarisha mazingira yatakayoendeleza uchumi na kwamba
ipo changamoto kubwa ya kuziunganisha sekta binafsi ili kuinua uchumi.
“Tatizo ni namna Serikali itakavyokubaliana na sekta binafsi katika
kuimarisha uchumi wake na kuwainua wananchi kibiashara kwa sababu
miundombinu ya uzalishaji hasa umeme bado haijasambaa katika mikoa
yote,” alisema.
Alisema Serikali itakapoiunganisha mikoa 26
katika kuzalisha biashara na kuipatia nguvu ya umeme, itakuwa njia
mojawapo ya kuimarisha mafanikio ya kila mwananchi na kuondokana na
umaskini. “Sasa hivi tunaambiwa kuwa kuna fungu la fedha la kutekeleza
kilimo, lakini bado kuna maswali mengi ya kujiuliza juu ya uwezeshwaji
wa kilimo, kwa sababu maeneo ya vijijini ambayo ndiyo
yanayojishughulisha na kilimo hayana umeme, Kilimo Kwanza
kitatekelezwaje?,” alihoji Msuya. Msuya alisema, ipo haja kwa Serikali
kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya kiutendaji ya halmashauri
mikoani ili kila mkoa uunganishiwe umeme kirahisi.
Kauli ya Ngeleja
Ngeleja
akizungumza kwenye hafla hiyo alisema, Serikali imetoa fursa kwa sekta
binafsi kuwekeza hasa katika masuala ya nishati ili kuzalisha, kusambaza
na kusafirisha.Alisema sekta binafsi imepewa jukumu hilo ili kuzalisha
zaidi na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kiwango kinachotakiwa na
kuboresha miundombinu yake.
“Tangu Serikali ilipofanya mageuzi ya
kisera katika uendeshaji uchumi wa nchi, sekta binafsi imekuwa
ikiongezewa nguvu ya biashara hivyo ni vyema sekta hiyo ikatumia fursa
ya kuwekeza zaidi katika sekta muhimu na kuzingatia sera ya nishati ya
mwaka 2008,” alisema.
Alisema matatizo ya umeme yaliyopo
yanatokana na mfumo wa kuunganisha umeme na kiwango kikubwa kinachopotea
kutokana na usambazaji kuanzia katika chanzo cha umeme.
“Uwekezaji
mdogo katika umeme unaochukua muda mrefu pia ni chanzo kikubwa katika
kuchangia umeme, tozo zinazotozwa hazikidhi mahitaji yaliyopo na gharama
kubwa za mafuta katika soko la dunia zinaongeza gharama za uzalishaji,”
alisema. Akizungumzia tatizo la mgawo wa umeme, Ngeleja alisema uchumi
wa nchi umeporomoka kwa asilimia 6.9 na kuwa megawati 236 za mgawo huo
kwa siku moja zinagharimu Dola za Marekani 400 milioni (takriban Sh500
bilioni).
Mgawo wa umeme umekuwa ukiitikisa nchi zaidi tangu
mwaka 2006 na hadi sasa Serikali imekuwa na mipango mingi ukiwamo ule
uliopitishwa na Bunge hivi karibuni, kuonekana kukosa tija. Katika
mpango huo wa dharura, Serikali ilitangaza kuwa itatumia kiasi hicho cha
Sh1.2 trilioni kwa ajili ya mpango huo wa ili kunusuru uchumi wa nchi
kuanzia Agosti hadi Desemba mwaka huu na Januari hadi Desemba mwakani.
Wiki
moja iliyopita, Waziri Ngeleja alitoa ahadi ya kupungua makali ya mgawo
huo lakini hadi sasa, hakuna nafuu iliyojitokeza.
Chanzo: Mwananchi
Wednesday, September 21, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment