Friday, September 9, 2011

Hatimaye BAE yakubali kuilipa Tanzania fedha za Rada

Best Blogger Tips
Kampuni ya kutengeneza silaha za kijeshi ya Uingereza BAE Systems, hatimaye imekubali kuilipa moja kwa moja serikali ya Tanzania dola milioni 47.

Fedha hizo ni malipo ya ziada yaliyotokana na mauzo ya Rada ambayo yalikuwa ni zaidi ya fedha halisi ya ununuzi wa rada hiyo .

Uamuzi huo unahitimisha mvutano wa muda mrefu kuhusu ununuzi wa rada hiyo ambao ulifanyika katika mazingira ya rushwa na kusababisha mahakama nchini Uingereza kuamuru fedha hizo zirejeshwe Tanzania
Kampuni ya BAE Systems ilishutumiwa na wabunge wa Uingereza kwa kujivuta kutekeleza amri ya mahakama iliyotolewa zaidi ya mwaka mmoja uliopita .

Serikali ya Uingereza ilisema imeiambia BAE kuwa hawana budi kulipa malipo hayo na kutarajia kuwa suala hilo lingefikiwa muafaka kwa faida ya watanzania.

Awali katika taarifa yake rasmi BAE ilisema inafanya kazi na serikali ya Uingereza kupitia wizara yake ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) kutoa malipo hayo kulingana na utaratibu wao.

BAE haikuwa tayari kuilipa serikali ya Tanzania fedha hizo na ilitaka ilipe kupitia misaada yake kwa mashirika ya hisani ya Uingereza yanayofanya kazi nchini Tanzania.

Akizungumza na BBC Idhaa ya Kiswahili kutoka Kongwa Dodoma, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai alisema ‘huku Tanzania tumeupokea uamuzi huo kwa furaha kubwa sana sana sana, kwa sababu ni jambo ambalo kwa upande wetu tukuwa tunaona kuwa si haki na kwa kuwa sasa fedha hizo zinarudi Tanzania,
‘Ni matumaini yetu kuwa fedha hizi zitatumika vizuri, kupitia serikali yetu kwa manufaa ya watanzania wote kama ilivyokusudiwa.’ Aliongeza Bw Ndugai.

Naibu Spika Job Ndugai miezi michache iliyopita aliongoza ujumbe wa wabunge wa Tanzania mjini London kufuatilia malipo hayo, baada ya kutokea mvutano wa muda mrefu kati ya serikali Tanzania na kampuni hiyo ya BAE.
Chanzo: BBC

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits