Thursday, September 8, 2011

Mbuzi mwenye miguu nane azaliwa Bunda

Best Blogger Tips
KATIKA  hali isiyokuwa ya kawaida mbuzi mmoja katika Kijiji cha Nafuba kilichoko Kata ya Nansimo wilayani hapa, amezaa mapacha  huku mmojawao akiwa na miguu minane, mikia miwili na kichwa kimoja.

Habari zilizopatikana kutoka kijijini hapo na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kilomo, kulikotokea tukio hilo, Fabian Kamanyi zinasema tukio hilo la kustaajabisha lilitokea jana mnamo  saa 1:45 asubuhi wakati mbuzi huyo aliyekuwa ametimiza miezi tisa ya ujauzito wake kuzaa mapacha hao kikiwamo kiumbe hicho ambacho hata hivyo kilikufa saa mbili baadaye.

Fabian alisema kabla ya kuzaa mbuzi huyo ambaye hiyo ni mara yake ya tatu kuzaa usiku, alikuwa akilia kama ishara ya kutaka kuzaa  hali iliyomfanya mmiliki wake Silvanus Bernado, asubuhi yake  kumtenganisha na wenzake kwa kumfunga jirani na nyumbani ili ampatie uangalizi wa pekee.

Alisema hatimaye ulipotimia muda wake wa kuzaa (usiku), mbuzi huyo alizaa mapacha hao akiwamo huyo mmoja wa ajabu ambaye alikuwa wa kwanza kuzaliwa akiwa haonyeshi jinsi  ya aina yoyote tofauti  na mwenzake ambaye alikuwa ana jinsi ya kiume.

Ingawa mwenye mbuzi huyo (Bernado), alilielezea tukio hilo kama kitu cha kawaida, lakini baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ambacho ni moja ya Visiwa ndani ya Ziwa Victoria eneo la Wilaya ya Bunda wanaliona kama moja ya matendo ya ushirikina hali iliyosababisha wazee wa kisiwa hicho kulikemea kwa kumtaka aliyefanya hivyo aache mara moja.

Kwa upande wake daktari wa mifugo wa wilaya hiyo, Dk Ndyanabo Tibaijuka alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo licha ya kusema hakuwa hajapata taarifa rasmi, lakini alisema kama limetokea ni jambo la kawaida katika maisha ya viumbe linalojitokeza wakati wa hatua za awali za uchanga wa mimba pindi viungo mbalimbali vya mwili vinapogawanyika ili kujiumba katika umbo linalotakiwa.

“Sijapata taarifa rasmi za tukio hilo; lakini kama limetokea hilo ni jambo la kawaida linalotokea katika hatua za awali za uchanga wa mimba viungo vinapojigawanyisha,”alisema Dk Ndyanabo.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits