Saturday, September 24, 2011

Liyumba atoka jela

Best Blogger Tips
Hatimaye aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Amatus Liyumba (63), jana aliachiwa huru na Jeshi la Magereza, baada ya kumaliza kifungo chake cha miaka miwili kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi.

Liyumba aliachiwa jana asubuhi baada ya kutumikia kifungo cha miaka miwili alichohukumiwa na jopo la mahakimu wawili kati ya watatu waliosikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na NIPASHE jana majira ya saa 4:42 asubuhi, kwa njia ya simu, msemaji wa jeshi hilo, Kamishna Mwandamizi, Omary Mtiga, alisema kuwa Liyumba aliachiwa baada ya kumaliza kifungo chake mapema saa 3:00 asubuhi na kuongeza kuwa alikuwa huru rasmi nje ya gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam. 

“Ndiyo Liyumba ameachiwa leo (jana) asubuhi kwa sababu ameshamaliza kutumikia adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka miwili katika gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam,” alisema Kamishna Mtiga.

Mei 24, mwaka jana, mahakimu wawili, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa kati ya watatu walitoa hukumu iliyomtia hatiani bosi huyo wa zamani wa BoT, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

Liyumba alituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 221 kupitia kwenye mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo.

Hukumu ya Hakimu Edson Mkasimongwa ilimuona Liyumba ana hatia katika kosa hilo.

Mbali na kuachiwa huru, Liyumba yuko nje kwa dhamana kwa shtaka la kukutwa na simu gerezani kinyume na kifungu namba 86 kidogo cha kwanza na cha pili cha Sheria ya Jeshi la Magereza.

Ilidaiwa kuwa Julai 27, mwaka huu kinyume cha sheria hiyo ya magereza, Mkurugenzi huyo wa zamani, alikutwa na simu ya mkononi aina ya Nokia 1280 ya rangi nyeusi iliyokuwa inatumia laini namba 0653-004662 pamoja na namba ya utambulisho ya simu (IMEI) 356273/04/276170/3.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alikutwa na simu hiyo katika chumba chake cha magereza bila kuwa na kibali cha kufanya hivyo huku akijua ni kosa.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na mahakama ilimtaka kujidhamini kwa hati ya dhamana ya Sh. 50,000 na mdhamini mmoja ambaye ni mtumishi wa serikali au kutoka kwenye taasisi inayotambulika.

Mshtakiwa alitimiza masharti hayo na mahakama ilimuachia kwa dhamana hadi Septemba 29, mwaka huu.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits