RAIS Jakaya Kikwete amewateua wakuu wa mikoa wapya 15, kuwabadilisha
vituo vya kazi wakuu wa mikoa watano huku wengine saba wakielezwa kwamba
wamestaafu kwa mujibu wa taratibu. Katika uteuzi huo, wa wakuu wa mikoa
21, kati yao 11 walikuwa wakuu wa wilaya na ni Perseko Ole Kone pekee
aliyebaki katika kituo chake cha kazi cha Mkoa wa Singida.
Mbali
ya idadi kubwa ya wakuu wa wilaya waliopandishwa vyeo, katika uteuzi
huo, Rais Kikwete pia amewateua waliokuwa Manaibu Waziri watatu,
Mwantumu Mahiza, Ludovick Mwananzila na Joel Bendera, kuwa wakuu wapya
wa mikoa.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa Dar es
Salaam jana iliwataja wakuu hao wa wilaya waliopandishwa vyeo na mikoa
yao katika mabano kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, John Tupa (Mara), DC
wa Morogoro, Saidi Mwambungu (Ruvuma), Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Chiku
Gallawa (Tanga), DC wa Ilala, Leonidas Gama (Kilimanjaro), DC wa Newala,
Dk Rehema Nchimbi (Dodoma), Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Elaston Mbwillo
(Manyara).
Wengine ni DC wa Karagwe, Kanali Fabian Massawe
(Kagera), DC wa Mvomero, Fatma Mwassa (Tabora), DC wa Manyoni, Ali
Rufunga (Lindi), DC wa Kilombero, Mhandisi Ernest Ndikillo (Mwanza), DC
wa Bagamoyo, Magesa Mulongo (Arusha). Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mkoa
wa Ruvuma, Mhandisi Stella Manyanya ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Rukwa.
Katika uteuzi huo, Mahiza anakwenda Mkoa wa Pwani, Bendera
ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mwananzila Shinyanga. Kabla
ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Mahiza alikuwa ni Naibu Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Mwananzila huku Bendera akiwa ni Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.
Waliobadilishwa vituo vya
kazi ni Abbas Kandoro anayekwenda Mbeya akitokea Mwanza, Said Mecky
Sadiki anayehamia Dar es Salaam akitokea Lindi, Christine Ishengoma
anayekwenda Iringa akitokea Ruvuma, Luteni Kanali Issa Machibya kutoka
Morogoro kwenda Kigoma na Kanali Joseph Simbakalia anakwenda Mtwara
akitokea Kigoma.
Wakuu wa mikoa waliostaafu ni Mohammed Babu
aliyekuwa Kagera; Isidore Shirima (Arusha), Kanali Anatory Tarimo
(Mtwara), John Mwakipesile (Mbeya), Kanali Enos Mfuru (Mara), Brigedia
Jenerali Dk Johanes Balele (Shinyanga) na Meja Jenerali Said Kalembo
(Tanga).
Wakuu wa wanne wa mikoa waliostaafu ambao watapangiwa
vituo vingine vya kazi ni Amina Mrisho aliyekuwa Pwani, Dk James Msekela
aliyekuwa Dodoma, Abeid Mwinyimusa aliyekuwa Tabora na Daniel Ole
Njoolay wa Rukwa.
Taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu imesema:
“Wakuu wa mikoa mipya minne ya Simiyu, Geita, Katavi na Njombe
itakayoundwa baada ya taratibu kukamilika watatangazwa baadaye.”
Taarifa
hiyo iliongeza: "Wakuu wote wa mikoa waliopo sasa wameagizwa kuandaa
hati za makabidhiano katika muda wa siku 14 kuanzia siku ya kuapishwa
kwa wakuu wapya wa mikoa. Aidha, wakuu wa wilaya ambao wamepandishwa
vyeo kuwa wakuu wa mikoa nao wanapaswa kufanya hivyohivyo kwa ajili ya
wakuu wa wilaya watakaopangiwa vituo vitakavyokuwa vimeachwa wazi
kutokana na uteuzi wao.”
"Makabidhiano hayo lazima yahusishe pia
kutembelea kwa pamoja baadhi ya maeneo na miradi ambayo ni muhimu kama
sehemu ya makabidhiano yao," ilisisitiza taarifa hiyo na kuongeza:
"Wakuu
wote wa mikoa walioteuliwa na wakuu wa mikoa minne mipya watakaoteuliwa
pamoja na wakuu wote wa wilaya watakaoteuliwa baada ya zoezi kukamilika
watatakiwa kuhudhuria mafunzo ya wiki tatu kwenye Chuo cha Serikali za
Mitaa Hombolo, Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi wa kiuongozi
na kiutendaji.”
Wakuu hao wapya wa mikoa wataapishwa na Rais Kikwete kesho saa 4.00 asubuhi kwenye Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.
Chanzo: Mwananchi
Wednesday, September 14, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment