BAADHI ya maghorofa
yanayochipuka kama uyoga jijini Dar es Salaam na kwingineko nchini,
yanatokana na shughuli za usafishaji wa fedha haramu.
Shughuli hiyo inafanyika kwa wafanyabiashara hao kuingiza fedha
haramu kutoka nje ya nchi na kununua bidhaa na huduma na kuziuza
kihalali nchini kwa muda kabla ya kuzibadilisha katika fedha za kigeni
na kuondoka nazo.
Akichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Udhibiti wa Fedha
Haramu wa Mwaka 2012 bungeni jana, Kabwe Zitto alidai hata upandaji
holela wa bei za viwanja katikati ya miji umekuwa ukisababishwa na
wafanyabiashara wa fedha chafu.
Alidai mabilioni ya fedha yalitoroshwa nchini kati ya mwaka 2000
hadi mwaka juzi kwa njia mbalimbali ambapo zinakadiriwa kufikia dola
bilioni 2.9 za Marekani. Hali hiyo alidai inachangia pia upandaji holela
wa bei za viwanja vya kujenga katikati ya miji hususan Dar es Salaam.
Alidai kuanguka kwa sarafu ya Tanzania kati ya Septemba na Novemba
mwaka jana, ni matokeo ya shinikizo la wasafishaji hao wa fedha, ambao
walinunua fedha nyingi za kigeni na kuondoka nazo. Muswada huo ambao
ulisomwa kwa mara ya pili jana na kuanza kuchangiwa na Zitto kati ya
wachangiaji sita walioruhusiwa kabla ya kuhitimishwa, umelenga kufanya
marekebisho katika vifungu kadhaa na kutoa adhabu kali kwa wahusika.
Hata hivyo, pamoja na mchango wa Zitto, kambi rasmi ya upinzani
katika hotuba yake, ilisema sifa ya Tanzania na nchi jirani kuwa
wasafishaji wa fedha haramu inatokana na Taifa kutotumia sheria
iliyotungwa mwaka 2006 inavyostahili. Kwenye hotuba hiyo iliyosomwa na
Naibu Waziri wa Fedha Kivuli, Christina Mughwai, Upinzani ulihoji
Serikali kutaka kufanya mabadiliko katika sheria ambayo haijaona
utekelezaji wake.
Mwaka 2006, Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Kuzuia Fedha
Haramu lakini haikutungiwa kanuni za utekelezaji. “Kwa mfano sheria
iliyopo kifungu cha 23 (1) iliweka utaratibu wa fedha ambazo zinaingia
na kutoka nje ya nchi, lakini la kustaajabisha, tangu wakati huo kwa
kipindi cha miaka sita sasa, mipaka ya nchi imekuwa ‘wazi’ na fedha
nyingi zinatoka bila kujulikana, kutokana na kukosekana kwa utekelezwaji
wa kifungu hiki cha sheria,“ alisema Waziri Kivuli.
Alisisitiza, kwamba kifungu hicho kilimpa Waziri mwenye dhamana ya
fedha, mamlaka ya kuamua ni kiasi gani cha fedha kinaweza kusafirishwa
nje ya nchi kikiwa ni kiasi taslimu, ambacho mtu anapaswa kuwa nazo,
lakini hakuna kilichofanyika mpaka sasa. Katika hotuba hiyo pamoja na
kupendekeza kikomo cha fedha za kigeni anazoruhusiwa mtu kubeba zikiwa
taslimu kuwa dola 10,000, walihoji kama kweli Serikali ina dhamira ya
kutekeleza sheria hiyo.
Walidai kuwa hata kwenye mkutano wa Maseru (Lesotho), Serikali
ilikataa kusaini mkataba wa fedha haramu kwa tuhuma kwamba Tanzania na
Malawi ndizo zinatumika sana kusafisha fedha.
Mkutano huo wa Agosti 2009 ulikuwa na lengo la kuangalia namna bora
za kukabiliana na fedha haramu ambazo zinatishia uchumi wa nchi za
Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Upinzani pia ulizungumzia vifungu kadhaa vinavyotakiwa kubadilishwa na kusema vingine havina uhalisia.
Ulitolea mfano kifungu cha 28B kinachopendekeza adhabu ya jumla kwa
mtu kuwa faini ya juu Sh milioni 500 na kiwango cha chini Sh milioni 100
au kifungo kisichozidi miaka mitatu jela, wakati kwa kampuni au
taasisi kiwango cha adhabu ni kuwa faini isiyo chini ya Sh milioni 500 .
“Utaratibu huu wa kutoza faini ni dhahiri kuwa haukufikiwa kwa
kuzingatia kigezo chochote kile, kwani haijabainisha kuwa ni kiwango
gani cha fedha kitapaswa kulipiwa faini hiyo na hivyo kinaweza kutumika
kama kishawishi katika kuvutia wahalifu na hasa kampuni kutumia mwanya
huu kupitisha fedha nyingi haramu,“ alisema Mughwai.
Alisema Kambi ya Upinzani, inaona faini hizo haziko kiuhalisia,
hivyo kutaka faini ziwekwe kwa kutumia asilimia ya fedha atakazotuhumiwa
nazo na kiwango kiwekewe jedwali.
Muswada huo una marekebisho mbalimbali manane yaliyoombwa na
Serikali yashughulikiwe, yakiwamo ya Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu,
sura ya 423 ili iweze kutumika Tanzania Bara pekee na kurekebisha
sheria ili kuwezesha Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU)
kujitegemea.
Chanzo: HabariLeo
Saturday, February 4, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment