Mabingwa wapya wa soka wa Afrika, Chipolopolo wa Zambia wamepokelewa kwa shangwe katika mji mkuu Lusaka.
Mwandishi wa BBC anasema mashabiki waliokuwa
wakisubiri, walilipuka kwa kelele za shangwe, wakati nahodha Christopher
Katongo alipotoka kwenye ndege akiwa amelibeba Kombe la dhahabu la
Mataifa ya Afrika.
Zambia waliwashinda Ivory Coast kwa mikwaju ya penati 8-7, katika mchezo
wenye msisimko hasa baada ya dakika za kawaida na za nyongeza
kumalizika.
Ushindi huu una umuhimu wa kipekee hasa kwa sababu miaka 19 iliyopita
karibu kikosi kizima cha Zambia kiliteketea katika ajali ya ndege nchini
Gabon.
Mwandishi wa BBC Mutuna Chanda anasema barabara ya kwenda uwanja wa
ndege wa Lusaka imetapakaa rangi ya ijani, nyekundu, machungwa na
nyeusi, huku maelfu ya mashabiki wakijipanga kutaka kuwaona wachezaji
wakirejea rasmi.
Kutakuwa na sherehe katika viwanja vya wazi mjini Lusaka.
Kutuza
Takriban watu 1,000, wengi wao wakiwa wametembea kilomita 25, walikuwepo uwanjani kuwalaki wachezaji wa timu ya taifa.
Shughuli hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na rais wa
zamani Rupiah Banda na Kenneth Kaunda, ambao wote ni mashabiki wakubwa
wa kandanda.
Wananchi wengi wa Zambia wamejipa likizo hii leo
ili kusherekea ushindi wa kwanza kabisa wa Zambia wa Kombe la Mataifa
ya Afrika.
Kikosi hiki kilichoibuka na ushindi, kiliondoka
katika uwanja ule ule wa ndege wa Libreville, ambao ndege ya kijeshi
iliongeza mafuta ikielekea Senegal kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe
la Dunia mwezi Machi 1993 - na ndege hiyo kuanguka muda mfupi baada ya
kupaa.
Wachezaji wa Zambia, maarufu kama Chipolopolo
Boys (yaani risasi za shaba), walitoa heshima zao kwa wachezaji 18
waliokufa katika ajali hiyo ya ndege - na kutuza ushindi huu kwa kikosi
hicho kilichopotea.
Amani
"Wachezaji waliokufa katika ajali ya ndege
nchini Gabon ndio walitupa hamasa, na nguvu katika michuano hiyo,"
amesema golikipa Kennedy Mweene akiwaambia waandishi wa habari kabla ya
kuondoka Libreville.
"Hatukutaka kuondoka mikono mitupu," alisema.
Winga Felix Katongo aliwaambia waandishi wa
habari: "Tulitaka kushinda kombe hili ili wananchi wa Zambia wajivunie
na kwa wale waliokufa, kupumzika kwa amani. Sasa roho zao zitakuwa na
amani."
Chanzo: BBC
Monday, February 13, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment