SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi kudai Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk
Harrison Mwakyembe hajalishwa sumu, kiongozi huyo ameibuka na kusema
amekerwa na jeshi hilo kutoa taarifa za uongo kwa wananchi ikiwa ni
pamoja na kuingilia utaratibu wa matibabu bila ya idhini yake.
Mwakyembe
alifafanua kuwa sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, bali inaweza
kudhuru hata kwa kugusishwa na kusisitiza kuwa, aliwahi kulieleza jeshi
hilo kwamba kuna kundi limejipanga kumdhuru, lakini lilifanya mzaha.
Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kyela, alisema tangu
alipoanza kutumiwa ujumbe wa vitisho na wabaya wake aliowaita ni
mafisadi mwanzoni mwa mwaka jana, alikuwa akitoa taarifa kwa jeshi hilo,
lakini mpaka sasa limeshindwa kuwachukua hatua zozote.
Kauli
hiyo ya Dk Mwakyembe inafuatia Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai(DCI),
Robert Manumba kuwaeleza waandishi wa habari juzi kwamba wananchi
wanatakiwa kupuuza madai yaliyotolewa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta kuwa Waziri Mwakyembe amelishwa sumu.
DCI Manumba alieleza kuwa waliwasiliana na Wizara ya Afya ili kubaini
chanzo cha ugonjwa wa Naibu Waziri huyo, lakini taarifa iliyowasilishwa
na wizara hiyo kwa Jeshi la Polisi imeonyesha kuwa, hajalishwa sumu.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Mwakyembe alisema anapata taabu
kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya
matatibabu yake, au walisoma taarifa nyingine na kama waliisoma, taarifa
hiyo wenyewe ama walisomewa.
Katika taarifa hiyo, alisema
alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari hakifanani kabisa na
picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo ya nchini India
anakotibiwa. “Ripoti inatamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow
(ndani ya ute wa mifupa) kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho
mabingwa wanahangaikia kukijua,” “Lakini vyombo vyetu vya dola
vinapelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu
kwamba ‘sikulishwa sumu’, sikulishwa sumu,” alisema Mwakyembe katika
taarifa hiyo.
Aliongeza kuwa,“Nimelazimika leo Jumamosi (jana)
kutoa taarifa hii kwa vyombo vya habari kufuatia mkutano wa DCI Robert
Manumba na waandishi wa habari uliofanyika jana (juzi) kuongelea, pamoja
na mambo mengine, hali yangu ya afya na kuhitimisha, kienyejienyeji tu
kuwa, “sikunyweshwa sumu”. Mwakyembe alisema taarifa hiyo ya DCI
Manumba imeshindwa kufafanua ugonjwa wake wa ngozi umesababishwa na
nini. Waziri huyo alisema msimamo huo wa Jeshi la Polisi umemkera
katika hali aliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato wa
matibabu yake na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake unaoendelea
Hospitali ya Apollo ambako bado anatibiwa.
Alisema kuna ufinyu
wa uelewa uliojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi
uliosisitiza kuwa ’hakunyweshwa sumu’ wakati sumu si lazima unyweshwe
ili imdhuru mtu, bali inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa. Waziri huyo
alisema kuwa ni hatari kwa Jeshi hilo kujiingiza kwenye suala ambalo kwa
takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa
au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.
Alifafanua kwamba Februari 9, mwaka jana, alimwandikia barua Mkuu wa
Jeshi la Polisi(IGP) Said Mwema, kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa
maisha yake na ya viongozi wengine. Alisema kuwa kwa kutambua kuwa
Polisi wa Tanzania husisitiza kuletewa ushahidi kwanza ndipo wafanye
kazi, alihakikisha ameainisha katika barua hiyo kila ushahidi alioupata
au kupewa.
Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema anashangazwa na
utaratibu unaotumiwa na Jeshi hilo wa kusubiri ushahidi mezani bila ya
kuchunguza na kuwafananisha na mahakimu wanavyosubiri ushahidi
mahakamani. Alisema utaratibu huo haupo popote duniani ila ni Tanzania
peke yake, kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni kutafuta
ushahidi. “ Polisi duniani kote wanachohitaji ni kupata clue au tetesi
tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika,” Mwakyembe
alisema katika taarifa hiyo. Naibu waziri huyo alisema pamoja na
kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi aliokuwa nao, yapo mambo manne
yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na dhamira ya
dhati ya kupeleleza suala hilo.
Mambo manne Akifafanua mambo
hayo katika taarifa hiyo, alisema siku chache baada ya kumkabidhi IGP
Mwema barua hiyo, alitumiwa timu ya wapelelezi ofisini kwake ili
kuchukua maelezo yake ya ziada. Alifafanua kuwa timu hiyo ilikuwa
inaongozwa na Ofisa wa polisi ambaye wiki chache zilizopita alikuwa
miongoni mwa askari waliotuhumiwa kupokea rushwa kwa lengo la
kumbambikizia dawa za kulevya mtoto wa mmoja wa wafanyabiashara maarufu
nchini, suala alilodai kuwa mpaka sasa uongozi wa Polisi umeshindwa
kulitolea maelezo ya kuridhisha.
Alisema kwa msingi huo, aliona
ameletewa mtuhumiwa wa rushwa na ujambazi kuendesha uchunguzi wa
watuhumiwa wengine wa ujambazi jambo ambalo haliwezekani na kwamba suala
lake limefanyiwa mzaha. Mwakyembe alisema wiki chache baada ya barua
yake kuwasilishwa kwa IGP na timu ya polisi kuanza kazi, Jeshi hilo
likachukua hatua ya kuwapongeza na kuwazawadia askari aliowatuhumu
kushirikiana na majambazi. “Huhitaji kuwa profesa wa falsafa kuelewa
kuwa huo ulikuwa ujumbe tosha wa kunipuuza,”ilibainisha taarifa hiyo.
Alisema
tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya ujambazi mkoani
Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari, wale aliowatuhumu kwenye
barua yake, walihamishiwa mikoa mingine. Mwakyembea alisema ili
kumkatisha tamaa kabisa, barua yake ya ‘siri’ kwa IGP ikavujishwa kwa
makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama habari iliyokebehi
na kukanusha taarifa nzima aliyoitoa “Sijui kwa faida ya nani,”
alihoji katika taarifa hiyo na kuongeza, “ Lakini huu ni mchezo wa
kawaida kwa Jeshi la Polisi. Akitoa mfano wa Waziri Sitta, kuwa hivi
karibuni, kiongozi huyo alihojiwa na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi
ofisini kwake, wakiwa wawili tu, lakini taarifa ya mahojiano
ikaonekana kwenye moja ya magazeti, ikikebehi ushahidi aliotoa Sitta na
kubainisha kuwa uadilifu wa uongozi wa Jeshi la Polisi, umefikia
pabaya.
Mwakyembe alisema, katika barua yake kwa IGP alieleza
kuwa kundi hilo la mauaji lilikuwa limeelekezwa kumuua kwa kutumia sumu,
taarifa ambayo kwa karibu mwaka mzima polisi hawakutaka kuifuatilia kwa
sababu wanazozijua wao. Waziri huyo alieleza kushangazwa na msukumo
mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama alipewa sumu au la na kuamua
kutoa tamko hata kabla ya kumchunguza alivyo.
Alisema polisi
hawajawahi kumhoji yeye wala wasaidizi wake ofisini na hata kuongea na
mabingwa wa Kihindi wanaomfanyia uchunguzi nchini India. Waziri huyo
aliwashangaa polisi badala ya kumshukuru, Waziri Sitta kwa sababu
amekuwa akiwapa tahadhari kuhusu afya yake ili suala hilo lichunguzwe
kwa kina, badala yake sasa anaonekana adui wao. “Nimesoma darasa moja
Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la Mlimani na DCI
Manumba.
Baadaye IGP Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa Sheria
Mlimani. Vigogo hawa wawili wa usalama wa raia nchini hawajanitendea
haki, nao wanajua,” alilalamika katika taarifa yake hiyo. Alisema
viongozi hao wanajua kuwa hawezi kukaa kimya au kumung’unya maneno pale
anapoona haki inakanyagwa bila ya kujali matokeo ya uamuazi huo. Katika
taarifa hiyo, Dk Mwakyembe aliwataka Watanzania kuombeana afya na uhai
ili waweze kutenda haki na waendelee kuitetea nchi yao ikiwemo kumalizia
viporo vinavyokera vya Dowans, EPA na Kagoda kwa maslahi mapana ya
Taifa. Historia ya ugonjwa wa Mwakyembe Dk Mwakymbe alianza kuumwa
Oktoba 9 mwaka jana na baadaye kupelekwa nchini India na kulazwa katika
Hospitali ya Apollo kwa matatibu. Alirejea nchini Desemba 11, mwaka jana
baada ya kulazwa hospitalini humo kwa takribani miezi miwili.
Msemaji
wa familia ya Dk Mwekyembe na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa,
alisema baada ya mbunge huyo kurejea nchini, afya yake ni njema ndio
maana ameruhusiwa kutoka hospitali.
Kauli za Waziri Sitta Mara
kadhaa Waziri Sitta amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza
kuwa ugonjwa wa Dk Mwakyembe, umetokana na kulishwa sumu. Akiwa kwenye
uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi
iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, jijini Dar es Salaam
Januari 28 mwaka huu, Sitta alisema:
“ Nasema Dk Mwakyembe
kapewa sumu, kama vyombo vya uchunguzi vinasema siyo, basi watueleze
ukweli, tena haraka,” alisisitiza Waziri Sitta katika hafla hiyo.
Sitta
alihoji “ Ni vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga
unamwagika chini, mhudumu anakuja kuufagia, lakini baada ya saa moja
unarudia tena, kitu hicho si cha kawaida.” Sitta alisema wamejaribu
wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni
kubwa kuliko yote.
Waziri Nahodha Akijibu moja ya kauli
hizo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nohodha alimtaka Waziri
Sitta awasilishe ushahidi wake ili ufanyiwe kazi badala ya kuzungumza
nje ya vyombo vya sheria. Hata hivyo, Sitta alisema hatapeleka ushahidi
wa madai aliyotoa kuwa Dk Mwakyembe alilishwa sumu kwa kuwa polisi
tayari wanao ushahidi.
Alisema wanachotakiwa kufanya Polisi ni
kufanya uchunguzi kuhusu madai hayo ya Dk Mwakyembe kulishwa sumu kwa
kuwa ushahidi wanao na wasianze kurushiana mpira.
“Waziri Nahodha
anataka ushahidi gani ikiwa taarifa za madaktari zinazomhusu Dk
Mwakyembe kuhusu sumu aliyopewa zilishapelekwa polisi, anataka mimi
nitoe ushahidi gani?” Alisema Waziri Sitta.
Source: Mwananchi
Saturday, February 18, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment