Kwa
muda sasa nchi yetu imepitia kwenye tatizo kubwa la mgomo wa madaktari
katika hospitali nyingi hasa za umma ambao kwa kiasi kikubwa mgomo huo
umekuwa na madhara makubwa kwa watanzania masikini ambao ni wengi, kiasi
cha kugharimu hata maisha yao.
Chama
Cha Mapinduzi kinachukua nafasi hii kuwapa pole sana wale wote
walioathiriwa kwa namna moja ama nyingine na mgomo huu. Na kwakweli
tunasikitishwa sana na hali inayoendelea!
Chama
Cha Mapinduzi kinawapongeza na kuwashukuru madakitari walioonyesha
ubinadamu na uzalendo kwa kuamua kurudi kazini na ambao hawakugoma
kabisa. Tunawashukuru na kuwapongeza kwani hakuna masilahi yanayovuka
thamani ya uhai wa binadamu mwenzako!
Tunachukua
fursa hii pia kuwashukuru sana na kuwapongeza askari wetu wa jeshi la
wananchi wa Tanzania kwa uamuzi wao wa kizalendo wa kuamua kuitikia wito
wa serikali kwenda kwenye baadhi ya hospitali kusadia kuwatibu
watanzania wenzao. Moyo huu ni wa kizalendo na wa mfano. Tunajivunia
uzalendo wa jeshi letu!
Tunachukua
nafasi hii kuwaomba madaktari wanaoendelea na mgomo kurudi kazini huku
wakiendelea na mazungumzo na serikali. Tunaamini madai yao yanawezekana
kushughulikiwa ikiwa pande zote mbili zitaamua kukaa chini kwa dhati na
kuzungumza.
Serikali
kwa upande mmoja watafute kwa makini chanzo cha mgogoro huu na kutafuta
majibu, na madakitari nao kwa upande wa pili, wawe tayari kukaa mezani
na kuzungumza. Tunasisitiza thamani ya maisha ya binadamu ni kubwa
kuliko masilahi na madai wanayoyaomba!
Serikali
ni vizuri ikajenga utamaduni wa kushughulikia matatizo haya ambayo
yanaathiri wananchi wengi kwa uharaka na udharura unaostahili badala ya
kusubiri hali inapokuwa mbaya zaidi.
POSHO ZA WABUNGE
Kwa
upande mwingine Chama Cha Mapinduzi kinapenda kurudia wito kilioutoa
juu ya swala la posho za wabunge. CCM iliwaomba na kuwasihi wabunge na
mamlaka zinazohusika na mchakato wa swala hili kuliangalia upya na
kutumia busara, ikiwezekana kuachana nalo kwasasa.
CCM
inaupongeza na kuunga mkono msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kama ulivyonukuliwa na taarifa ya
Ikulu kwa vyombo vya habari, kuwa ni vizuri wabunge wakalitafakari upya
swala hili kwa masilahi mapana ya wale waliowapa dhamana ya
kuwawakilisha bungeni.
CCM
inaendelea kuwasihi waheshimiwa wabunge walitafakari upya swala hili na
busara itumike katika kuliamua huku wakifungua masikio kusikiliza sauti
za Watanzania kwani huko bungeni wana wawakilisha hawa Watanzania, ni
vizuri kusikiliza hiki kilio chao! Si busara kupuuza kilio cha waliokupa
dhamana ya kuwawakilisha.
Msimamo
wa Rais Kikwete kama sehemu moja ya mamlaka inayohusika na mchakato huo
ni uthibitisho wa usikivu wake kwa wananchi anaowaoongoza, yeye
katimiza wajibu wake, tunawasihi waheshimiwa wabunge wetu nao
walitafakari hili na kuona busara ya kuachana nalo kwasasa.
Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM
Itikadi na Uenezi
No comments:
Post a Comment